NA VERONICA ROMWALD
-DAR ES SALAAM
NOTISI ya siku 30 iliyotolewa na Wakala wa Hifadhi ya Barabara (Tanroad), kwa wananchi waliokuwa kando mwa barabara ya Morogoro, imemwibua Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema).
Mbunge huyo ambaye alikuwa hajaonekana jimboni kwa miezi kadhaa, hatimaye jana alilazimika kukatisha vikao vya Bunge mjini Dodoma na kwenda kusikiliza kilio cha wapigakura wake ambao nyumba zao zimewekewa alama ya X ambao wametakiwa kuzibomoa wenyewe kabla Mei 30, mwaka huu kwa ajili ya kupisha upanuzi wa barabara ya njia sita inayotoka Dar es Salaam hadi Chalinze mkoani Pwani.
Akiwasilisha malalamiko mbele ya mbunge huyo, mkazi wa Mbezi, Theresia Moses alisema alikabidhiwa barua hiyo inayomtaka kubomoa nyumba yake ndani ya siku 30 na kwamba hakuna malipo yoyote yatakayolipwa kama fidia.
Alisema hatua hiyo imemfanya aishi kwa mawazo huku akishindwa kujua hatima ya maisha yake kutokana na kuwa na familia kubwa ambayo inamtegemea.
Naye mkazi wa Kimara Stop Over, Adela Lyimo alisema barua hiyo inawataka kubomoa nyumba zao na kama hawatafanya hivyo zitabomolewa kwa nguvu na watatakiwa kulipa gharama za ubomoaji.
“Kwanza barua ile nililetewa na wahuni hawakuwa na barua yoyote ya utambulisho, hatupingi maendeleo, tunachotaka tusikilizwe kilio chetu, Serikali itulipe fidia na kiwanja ili tujue tunaondokaje kwenda kuanza maisha pengine,” alisema.
Naye Hassan Mussa alisema agizo hilo limewaacha wananchi njia panda huku wakijifananisha na wakimbizi katika nchi yao.
“Hatujui sisi ni wananchi au wakimbizi katika nchi yetu. Tunaona uchungu kweli kweli, tunataka kujua nini hatma ya maisha yetu ya sasa na ya baadaye.
“Tuna masikitiko mengi, tumeishi katika maeneo haya kwa zaidi ya miaka 30 leo hii tunaambiwa tuondoke ndani ya siku 30 na hakuna malipo yoyote, tutaishi namna gani?,” alihoji.
Akijibu hoja hizo, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, alisema upana uliotajwa na TANROAD katika notisi hiyo una utata na kwamba atasimama na wananchi hao kutetea wapate haki yao.
“Suala hili halijaanza leo, lilianza tangu wakati wa Serikali ya Awamu ya nne iliyokuwa inaongozwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete wakati huo Rais John Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi.
“Nilitaka kulisema bungeni wakati huo, bahati mbaya mbunge unapokuwa na hoja binafsi Serikali inalifahamu kabla hujalisema, siri hii sikuwahi kuisema hata siku moja, lakini leo (jana) naisema.
“…nilipotaka kulisema, Magufuli (wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi alinifuata na kuniambia ikiwa nitasema atatumia Sheria ya Barabara ya mwaka 1932, 1967, 2007 na kanuni za mwaka 2009 na bila kujali rufaa waliyokuwa wamekata wananchi ataiagiza TANROADS kutekeleza bomoabomoa hiyo,” alisema Mnyika katika mkutano huo.
Mnyika alisema hata hivyo suala hilo halikutekelezwa kwa wakati huo na sasa limerudi tena.
“Sikujua kama alikuwa anafikiria kuja kuwa Rais. Baada ya kushinda urais haoni tena thamani, anatumia mamlaka aliyopewa, na ndiyo maana siku ile alimpigia simu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalaam na kuagiza wafanye bomoa bomoa,” alidai Mnyika.
Kutokana na hali hiyo Mnyika aliagiza Baraza la Madiwani kwa kushirikiana na kamati ya wananchi iliyoundwa kuandika barua ya kuomba kuonana na Rais Dk. John Magufuli kwa dharura.
“Iandikwe barua ya kuomba kuonana na Rais (Dk. John Magufuli) na mimi nitakuwepo, jambo hili ni la dharura na limetugusa kweli. Kwanza upana una utata hakuna barabara iliyowahi kujengwa popote yenye upana wa mita 243 sawa na viwanja viwili na nusu vya mpira,” alisema.
Alisema kulingana na hotuba iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano bado Serikali haina fedha za kuanza ujenzi wa barabara sita inayotaka kujenga katika eneo hilo.
“Katika aya ya 69 ya hotuba ya waziri ameeleza wazi kibali cha ujenzi huo kimesitishwa kwanini wananchi wabomolewe nyumba zao, mradi huu una utata mkubwa,” alisema.
Alisema mwaka 2013 mahakama ilieleza kwa kuwa wananchi walioko kwenye maeneo hayo walipelekwa na serikali yenyewe kuanzisha vijiji na mwaka 1974 hadi 1978 walipewa hati za vijiji wana haki ya kulipwa fidia.
“Nilihoji suala hili bungeni Mei 6, mwaka huu Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano hakunijibu, nikamuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa naye hakunijibu badala yake alinitaka nimsubiri waziri mwenye dhamana aje anijibu.
“Niliuliza pia Tanroad wao wakanieleza suala hilo hawawezi kuliongelea kwani maamuzi hayo yametoka katika ngazi ya juu,” alisema.
Mnyika alisema kesho (leo) ataandamana na wananchi 546 kwenda kufungua kesi katika mahakama ya ardhi kuweka zuio dhidi ya notisi hiyo.
“Tumekubaliana pia na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea tutakwenda kulisemea tena bungeni, nipo tayari hata kuondolewa katika ukumbi wa bunge lakini lazima niseme, tuombeeni naamini tutashinda vita hii,” alisema.