24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE :TUNAGEUZWA ATM

MAREGESI PAUL Na

RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

MBUNGE wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), amesema wananchi wamewageuza wabunge wa Tanzania na kuwa kama mashine za kutolea fedha (ATM) na Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS).

Kutokana na hali hiyo, amesema kuna haja Serikali kuboresha mafao yao ili yaendane na majukumu wanayokabiliana nayo.

Waitara aliyasema hayo jana mjini hapa wakati wa semina ya wabunge walioko katika mabunge ya nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CPA).

“Mshahara wa mbunge kila mwezi unakatwa shilingi milioni 1.2, lakini baada ya kumaliza miaka mitano ya ubunge, mafao yake yanakatwa tena.

“Hivi huo utaratibu mliutoa wapi wakati haupo nchi yoyote duniani? Sisi wabunge tumegeuzwa kama ATM au saccos kwa sababu tutatoa pesa kila mahali.

“Kule Kenya ofisi ya mbunge ni kama taasisi kwa sababu ina mbunge na ina mtafiti anayemsaidia mbunge kila anapotaka kufanya mambo yake.

"Hata kukiwa na harambee, mbunge unaitwa na kutakiwa uchangie fedha nyingi, sasa utachanga kwa fedha zipi wakati mnatulipa kidogo, yaani huu ni mzigo kwetu wabunge.

“Kwa hiyo, tuongezeeni mafao kwa sababu tunalipwa kidogo sana ikilinganishwa na nchi zingine,”alisema Waitara.

Kwa upande wake, Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo (CCM), pamoja na kulalamikia mafao madogo, alitaka kujua takwimu halisi za malipo wanayolipwa wabunge wa Kenya na nchi zingine ili wayalinganishe na wanayolipwa wabunge wa Tanzania.

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Shally Raymond (CCM), alisema kuna haja kwa wabunge hao kuboreshewa mafao yao ili waweze kufanya kazi kwa mafanikio zaidi.

Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema), pamoja na kulalamikia mafao, alilalamikia utaratibu wa vyama vya siasa kukutanisha wabunge wao ili wakubaliane kupitisha mambo yenye masilahi ya chama badala ya kuangalia utaifa.

Wakati hao wakisema hayo, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alitaka wabunge wawekewe bima ya afya ya maisha kama sheria inavyotaka.

“Kwanza kabisa nimeshangaa kusikia makao makuu ya CPA Barani Afrika yapo Tanzania na pia ofisi yao iko hapa bungeni.

“Kuhusu hilo suala la bima ya afya ya maisha ya wabunge, nashangaa kwanini Serikali haitaki kuliruhusu kwa wabunge kwani hata Tume ya Utumishi ya Bunge, imekuwa ikisisitiza juu ya jambo hilo.

“Yaani Tume ya Utumishi imelifuatilia kwa muda mrefu, lakini Serikali haitaki kukubali, jambo ambalo hakitendi haki kwa sababu baadhi ya wabunge wameshafariki na wengine wamepata ulemavu,” alisema Lugola.

Hata hivyo, wakati akijibu hoja hizo, Katibu wa Spika wa Bunge, Said Yakub, alisema chanzo cha wabunge kugeuzwa ATM ni wao wenyewe kwa sababu ndivyo walivyowazoesha wapiga kura wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles