Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Jimbo la Kibiti, Ally Ungando (CCM), amegoma kuzungumzia matukio ya kihalifu na mauaji yanayotokea katika eneo hilo, kwa kuhofia usalama wa maisha yake.
Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya kuuawa kwa aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Bungu wilayani Kibiti, Arife Mtulia, ambapo MTANZANIA lilimtafuta mbunge huyo ili kupata maoni yake.
“Sina comment yoyote juu ya mauaji hayo kwa sababu hata mimi ni binadamu nahofia usalama wangu pia vilevile,” alisema Ungando.
Kuuawa kwa kada huyo wa CCM ambaye alipigwa risasi na watu wasiojulikana juzi usiku akiwa nyumbani kwake, ni mwendelezo wa mauaji ya watu mbalimbali, wakiwamo askari wa Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali za vijiji mkoani Pwani.
Mauaji hayo yamekuwa yakifanyika mara kwa mara katika Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani, ambapo tukio hilo linafanya idadi ya watu waliouawa ndani ya muda mfupi kufikia 34.
Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, akisema Mtulia aliuawa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake juzi usiku.
“Ni kweli Mtulia ameuawa na watu wasiojulikana alikuwa ni kiongozi wa kata hiyo lakini kwa sasa hakuwa kiongozi,” alisema kwa ufupi huku akikata simu.
Kuuawa kwa kada huyo wa CCM kumekuja ikiwa imepita mwezi mmoja sasa tangu walipouawa askari nane na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi katika Kijiji cha Makengeni wilayani Kibiti.
Matukio ya mauaji katika Mkoa wa Pwani yanaelezwa kuonesha kila dalili kutekelezwa na watu wenye ujuzi na malengo mapana.
Tukio la sasa na lile ambalo lilichukua uhai wa askari wanane ni mwendelezo wa matukio mengine ya aina hiyo yaliyotokea katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja katika Mkoa huo wa Pwani.
Hadi sasa, si Jeshi la Polisi wala mamlaka nyingine ambazo zimekwishaeleza kwa uwazi kiini cha kuwako kwa mfululizo wa matukio ya aina hiyo katika maeneo yale yale.
Akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba aliliambia Bunge kuwa Serikali itaanzisha mkoa mpya wa kipolisi katika Wilaya za Kibiti, Rufiji, Mkuranga na Mafia ambapo utaitwa Mkoa wa Kipolisi Rufiji kwa leo kukabiliana na matukio hayo ya mauaji.
MFULULIZO WA MAUAJI
Kumekuwapo na mfululizo wa matukio ya mauaji katika wilaya za Kibiti na Mkuranga na kinachoshangaza ni kitendo cha wauaji kutochukua mali yoyote.
Aprili 14, mwaka huu askari nane waliuawa, ikiwa ni siku chache baada ya askari wa Jeshi la Polisi kuwaua kwa risasi wanaume watatu waliokuwa wamevalia baibui.
Wanaume hao, ambao walikuwa na pikipiki mbili walikuwa wakijaribu kukwepa vihunzi vya polisi vilivyokuwa vimewekwa katika Daraja la Mkapa.
Siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa askari, kada mwingine wa CCM naye aliuawa.
Februari mwaka huu, watu watatu, akiwamo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, waliuawa kwa risasi.
Wengine waliouawa ni Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji mapato ya ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni mlinzi, mgambo ambao walipigwa risasi kichwani na begani na walikufa papo hapo eneo la tukio.
Mei 5, mwaka huu kada wa CCM Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Amir Chanjale aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Januari, 2017, watu ambao Jeshi la Polisi hadi sasa halijawafahamu walimuua mfanyabiashara Oswald Mrope, kwa kumpiga risasi mbele ya familia yake.
Februari 3, 2017, watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto, huku yeye mwenyewe akifanikiwa kuwatoroka.
Oktoba, 2016, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho hicho, Aly Milandu aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wanne.
Novemba 2016, wenyeviti wawili wa vitongoji wa kijiji hicho, waliuawa kwa kupigwa risasi.
Mei, 2016 Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana aliuawa kwa risasi.