24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE CCM WAFICHUA ‘MCHAWI’ WA TATIZO LA MAJI

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

BAADHI ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamesema Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo chanzo cha kukwama kwa miradi mingi ya maji nchini.

Kutokana na hali hiyo, wamemtaka Waziri wa Fedha, Dk. Phillip Mpango, kulithibitishia Bunge kuwa atatoa fedha zote zitakapopitishwa na mhimili huo katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Wabunge hao walitoa shutuma hizo jana, wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18, iliyowasilishwa juzi na Waziri wa Wizara hiyo, Gerson Lwenge.

Katika mchango wake, Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe, alisema hawezi kuunga mkono bajeti ya wizara hiyo, kwa kuwa hakuna sababu ya wananchi kukosa maji wakati fedha zinapitishwa na Bunge.

“Kwanza kabisa, nampongeza Rais Magufuli kwa kusaidia kuondoa tatizo la maji Nzega wakati tukisubiri mradi wa miezi 36 (mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Tabora unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36), kwa sasa Nzega tunapata maji angalau mara mbili kwa mwezi.

“Nataka niseme jambo moja la kusikitisha pamoja na shukrani zote hizo nilizotoa. Leo Nzega tuna siku tano hatuna maji, sababu ni moja tu, kwamba Mamlaka ya Maji ya Nzega, ambayo imeanzishwa mwaka mmoja uliopita, imekatiwa umeme na Tanesco.

“Umeme huo umekatwa kwa sababu ya deni la Sh milioni 206 ambalo chanzo chake ni Selikali Kuu kutopeleka fedha za OC (matumizi mengineyo) kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

“Kwa sasa, wananchi wa Nzega wanaadhibiwa kwa kukosa maji kutokana na fedha kutopelekwa. Lakini mheshimiwa mwenyekiti, Bunge hili naomba badala ya kuwa tunamnyooshea kidole Waziri wa Maji, tukumbuke mzizi wa matatizo yote haya ni Wizara ya Fedha.

“Hili ndilo tatizo kubwa kuliko yote kwa sababu kila sehemu ukiuliza, unakuta tatizo ni fedha za maendeleo hazijapelekwa. Mimi ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii ambapo tumeona kuna tatizo la X-Ray kutofanyiwa service (matengenezo) na Kampuni ya

Philips kwa sababu Wizara ya Fedha haijailipa kampuni hiyo.

“Leo mamlaka za maji za nchi nzima zinadaiwa shilingi bilioni 8 na Shirika la Umeme, lakini mamlaka hizi kwa ujumla wake zinazidai taasisi za Serikali Sh bilioni 39. Yaani Watanzania wanalipa bili zao, lakini wanakatiwa maji kwa sababu taasisi za Serikali hazilipi umeme.

“Mheshimiwa mwenyekiti, hapa ninayo Katiba ya chama changu ambayo inasema wajibu namba tatu wa mwanachama ni kujitolea nafsi yake, kuondosha umaskini, ujinga na dhuluma na kwa ujumla kushirikiana na wananchi wote katika kujenga nchi yetu.

“Kwa hiyo, mimi sitakuwa sehemu ya dhuluma ya wananchi wa Nzega kwa kukosa maji kutokana na uzembe unaotokana na maamuzi ya Serikali, I will not be a part of this (sitakuwa sehemu ya hili).

“Sitaunga mkono bajeti ya Serikali kwa sababu moja tu, Waziri wa Fedha aje hapa, atuambie anamalizaje deni la Tanesco ili mamlaka za maji ziache kukatiwa umeme kwa uzembe unaofanywa na Serikali Kuu.

“Mheshimiwa mwenyekiti, hapa wabunge tumejadili sana kuongeza fedha kwenye bajeti hii, kwa hiyo, naomba Waziri wa Fedha popote alipo, apigiwe simu au naibu wake aje, atuhakikishie kwenye fainance bill kama wataongeza tozo ya Sh 50,” alisema Bashe.

LUSINDE

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtera, Livingston Lusinde, alisisitiza umuhimu wa Waziri wa Fedha kutoa fedha zote za bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Pamoja na hayo, alilalamikia kutokuwapo bungeni kwa Dk. Mpango na Naibu wake, Dk. Ashatu Kijaji, wakati wabunge wakijadili bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Katika maelezo yake, Lusinde alisema Wizara ya Fedha ni wizara mtambuka kwa kuwa ndiyo inayotoa fedha katika miradi mingi nchini na kwamba kutokuwapo bungeni kwa waziri na naibu wake, ni jambo lisiloweza kukubalika.

AMINA MAKILAGI

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Amina Makilagi, alisisitiza umuhimu wa Serikali kutoa fedha zote zinazopitishwa na Bunge ili miradi ya maji iweze kutekelezwa.

Wengine wataka Bunge lijadili mvua

Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge wamelitaka Bunge lisitishe shughuli zake kwa muda ili lijadili madhara yaliyosababishwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Wabunge hao walitoa hoja hiyo jana, walipokuwa wakizungumza baada ya kuomba miongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge.

Aliyekuwa wa kwanza kuzungumzia hoja hiyo ni Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi (CCM), ambaye alisema Bunge linatakiwa kujadili mafuriko hayo kwa kuwa yamesababisha madhara makubwa mkoani Tanga na kwingineko nchini.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, Mkoa wa Tanga umegeuka kisiwa kwa sababu baadhi ya barabara zake zinazotoka katika mikoa mingine na kuingia mkoani humo, hazipitiki kutokana na kuharibika vibaya.

“Mkoa wa Tanga umekuwa kama kisiwa kwa sababu barabara zake nyingi zimeharibiwa na mvua. Kule Lushoto maporomoko ya mawe yameziba barabara na inavyoonekana Tanroads wamezidiwa na hawana tena uwezo wa kukabiliana na uharibifu huo.

“Kwa hiyo, naomba Bunge lisitishe shughuli zake kwa muda ili tujadili tatizo hili angalau kwa dakika ishirini,” alisema Shangazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema kuna haja Bunge kusitisha shughuli zake ili lijadili madhara ya mafuriko hayo kwa kuwa uhai wa binadamu ni muhimu kuliko kitu kingine.

“Moja ya wajibu wa Bunge ni kusimamia na kulishauri Bunge. Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, baadhi ya watu wamepata madhara makubwa, kwani wengine hawana makazi na wanahitaji msaada.

“Kwa mfano, kule Pemba kuna kaya 600 hazina makazi, Unguja kuna kaya 200 hazina makazi na shule nyingi zimefungwa pia. Hata Tanga, Dar es Salaam, Morogoro na kwingineko nchini, hali ni mbaya.

“Kwa hiyo, mheshimiwa mwenyekiti, naomba Bunge liahirishe shughuli zake kwa muda ili tujadili mafuriko hayo,” alisema Mbatia.

Hata hivyo, Chenge alipokuwa akijibu miongozo hiyo, alisema Bunge haliwezi kuahirisha shughuli zake kwa kuwa Serikali inajua uwepo wa mafuriko hayo na inayafanyia kazi.

“Serikali imewasikia na iko humu bungeni. Kwa kuwa ina mkono mrefu, najua itachukua hatua kwa kutoa taarifa hapa bungeni kama ikiwezekana. Kwa hiyo, Bunge haliwezi kuahirishwa kwa sababu hiyo,” alisema Chenge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles