23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SOZIGWA, MWAMBUNGU WAFARIKI SIKU MOJA, HOSPITALI MOJA

AGATHA CHARLES NA VERONICA ROMWALD

– DAR ES SALAAM

VIONGOZI wawili, aliyekuwa Katibu wa Kwanza wa Rais (Ikulu- Habari ) wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Paul Sozigwa (84) na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, wamefariki dunia jana, nyakati tofauti wakiwa wanapatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa Taasisi hiyo, Anna Nkinda, alisema Sozigwa alifariki usiku wa kuamkia jana.

“Tulimpokea marehemu Aprili 25, mwaka huu akitokea wodi ya Mwaisela ambako alikuwa amelazwa, na kuanza kumpatia matibabu dhidi ya ugonjwa uliokuwa unamsumbua, Mei 9, mwaka huu afya yake ilianza kuimarika na akatolewa katika wodi ya uangalizi maalumu na kuhamishiwa katika wodi namba mbili,” alisema.

Nkinda alisema huko aliendelea kupatiwa matibabu na daktari wake hadi usiku wa kuamkia jana saa mbili na nusu ambapo alifariki dunia.

Naye, mtoto wa marehemu, Lucy Sozigwa, alisema msiba upo eneo la Mtoni, jirani na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) ambako ni nyumbani kwa mtoto wake mkubwa, Mchungaji Moses Sozigwa.

“Msiba uko hapa nyumbani kwa kaka Mchungaji Moses, Mungu akipenda tunatarajia kuzika siku ya Jumatatu huko Kisarawe, mkoani Pwani,” alisema Lucy.

Lucy alipotakiwa kueleza marehemu Sozigwa alikuwa akisumbuliwa na nini, alisema, kaka yake (mtoto wa marehemu pia) Moses ndiye angeweza kueleza kwa kina chanzo hicho.

Alipotafutwa Mchungaji Moses alisema baba yao alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu kwa muda mrefu.

“Mzee alikuwa mtu mzima, na katika umri huo tunaelewa kichwa kinakuwa kimechoka, na hali hiyo ilisababisha pia kupata tatizo lingine la moyo na uvimbe,” alisema.

Alisema jambo ambalo akilikumbuka linamuumiza kutokana na kifo cha baba yake, ni ule uzalendo aliokuwa nao kwa nchi yake.

“Alikuwa mzalendo wa kweli, sasa hivi tunaona uzalendo unapungua, baba aliipenda nchi, alifanya kazi kwa bidii siku zote, nikikumbuka jambo hilo naumia mno,” alisema.

Marehemu Sozigwa atakumbukwa kwa kushika nyadhifa mbalimbali nchini kabla ya kustaafu utumishi serikalini mwaka 1983.

Nyadhifa hizo ni pamoja na mwaka 1967 aliteuliwa kuwa Katibu wa Kwanza wa Rais (Ikulu-Habari ), Mkurugenzi Mkuu wa Kwanza wa Redio Tanzania (RTD), Ofisa Wilaya (DO), Wilaya ya Kisaraswe katika Serikali ya Kikoloni na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari na Utangazaji.

Mbali na hizo, pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwamo kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Kamati Kuu (CC) na Mwenyekiti wa Idara ya Udhibiti na Nidhamu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani.

Katika salamu za rambirambi, CCM kupitia Katibu wa NEC-Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, kilisema pamoja na kupokea taarifa hizo kwa mshituko, kitamkumbuka na kumuenzi marehemu Sozigwa kama mmoja wa waasisi wa Taifa na chama hicho.

Polepole katika taarifa yake alisema marehemu Sozigwa alihudumu katika uongozi wa kabla na baada ya Uhuru wa Tanzania Bara (Tanganyika) na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Jambo mojawapo ambalo ameshughulika nalo tangu awali ni uimarishaji wa misingi ya maadili na miiko ya uongozi CCM, kipekee sana ametumika kama Mtendaji Mkuu wa iliyojulikana kama Idara ya Udhibiti na Nidhamu ambayo sasa inajulikana kama Kamati ya CCM ya Usalama na Maadili, Uongozi chini ya Mwenyekiti John Magufuli,” alisema Polepole.

Polepole alisema, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, pia alitoa pole kwa familia, akisema utumishi na uongozi wa marehemu Sozigwa katika maadili na miiko ya uongozi unaendelea kuwa chachu ya kutenda siasa safi na uongozi bora ndani ya chama.

Katika mitandao ya kijamii kumekuwa na watu mbalimbali wanaomwelezea marehemu Sozigwa kuwa alikuwa na sifa kuu inayompambanua kuwa katika maisha yake yote ya siasa alihubiri kile alichokiamini.

Moja ya vipindi anavyodaiwa kuvianzisha akiwa Redio Tanzania ni ‘Mikingamo’ pamoja na kupinga ubepari huku akidaiwa aliishi kijamaa.

Akizungumzia kifo cha Mwambungu, Nkinda alisema naye alifariki dunia jana akiwa JKCI alikokuwa amelazwa kwa matibabu dhidi ya ugonjwa uliokuwa ukimsumbua.

“Mwambungu aliletwa JKCI Mei 10, mwaka huu akitokea Emergence (Idara ya Magonjwa ya Dharura), alipelekwa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu kwa matibabu, ambako alifariki dunia,” alisema Nkinda.

Itakumbukwa kuwa Mwambungu alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma tangu mwaka 2011, enzi za utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete na hata Rais Dk. John Magufuli alipoingia madarakani aliendelea naye.

Marehemu Mwambungu aliondolewa katika mabadiliko yaliyofanywa na Rais Magufuli Juni, 2016 na kurudishwa kuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Dar es Salaam, ili kupangiwa kazi nyingine.

Rais Dk. John Magufuli jana alizitumia salamu za rambirambi familia za marehemu Sozigwa na Mwambungu.

Kupitia taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Rais alisema Marehemu Sozigwa atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka, uchapakazi na uadilifu.

“Natambua kuwa marehemu Sozigwa ni miongoni mwa waasisi wa Taifa letu ambao walijitoa kwa dhati kupigania nchi yetu kabla na baada ya Uhuru. Alishirikiana na waasisi wengine, akiwamo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizolikabili Taifa baada ya uhuru, zikiwamo kupiga vita ujinga na maradhi ndani ya chama na serikali, hakika tutazienzi juhudi zake,” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu marehemu Mwambungu, Rais alisema alikuwa ni kiongozi wa aina yake, moyo wake na upendo ulimwezesha kufanikiwa katika kazi zake, na alipigania maendeleo ya wananchi pamoja na kutatua jambo kwa njia ya mazungumzo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles