24.1 C
Dar es Salaam
Thursday, October 21, 2021

RUFAA VYETI FEKI KUANIKWA JUMATATU

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Mitihani Nchini (NECTA), Dk. Charles Msonde, amesema orodha ya majina ya watumishi waliokata rufaa baada ya kutajwa kuwa na vyeti feki itatolewa hadharani keshokutwa.

Majina ya watumishi watakaotajwa  yatakuwa kati ya 9,932 yaliyokabidhiwa kwa Rais John Magufuli Aprili 28 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki.

Watumishi hao wanaodaiwa kuwa na vyeti feki walipewa takribani siku 12 kukata rufaa endapo wataona wameonewa.

Akizungumza na gazeti hili, Dk. Msonde alisema orodha hiyo itatolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi  hilo.

“Zoezi la kukata rufaa bado linaendelea, deadline (mwisho) Mei 15, sasa hatuwezi kutoa taarifa nusunusu, mtuvumilie nadhani mpaka Jumatatu nitatoa taarifa kamili,” alisema Dk. Msonde.

Alisema ni mapema sana kutoa taarifa hiyo, kwakuwa muda ambao watumishi wamepewa na Rais Magufuli haujakwisha.

Awali akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema hadi sasa idadi ya waliokata rufaa ni ndogo.

“Nipo njiani naelekea Dodoma, hapa sina taarifa kamili, lakini waliokata rufaa siyo wengi, jibu kamili watakuwa nalo NECTA kwa sababu wao ndio wanaopokea rufaa, sisi tunaletewa copy (nakala) za rufaa,” alisema Dk. Ndumbaro.

Akizungumzia awamu ya tatu ya kutangaza majina ya watumishi wenye vyeti feki waliopo katika wizara zilizobaki na taasisi, alisema yatatangazwa haraka hivi karibuni, baada ya mchakato huo kukamilika.

Majina hayo, ambayo awali yalipaswa kutangazwa Ijumaa iliyopita, Dk. Ndumbaro alisema wizara hiyo ilishindwa kufanya hivyo kwakuwa zoezi halijakamilika.

“Orodha ndio inakamilishwa, ipo kwenye hatua za mwisho, lakini very soon (hivi punde) itatoka,” alisema Dk. Ndumbaro.

Alisema endapo zoezi hilo litakamilika kama ilivyopangwa, huenda ikatolewa wiki ijayo.

Kitendo cha kuwaondoa watumishi wenye vyeti feki kazini kimeonekana kuathiri utendaji katika sekta mbalimbali, hasusan afya na hivyo kusababisha usumbufu kwa wagonjwa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,644FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles