25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI WASOMEA JIKONI KWA KUKOSA MADARASA

Na ASHURA KAZINJA, MOROGORO

WANAFUNZI wa shule ya awali katika Shule ya Msingi Mkambarani wanasomea jikoni kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.

Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkambarani, Bill Numbi wakati akizungumza na MTANZANIA kijijini hapo ambapo alisema wanafunzi hao wanasomea kwenye jengo lililotengwa maalum kwa ajili ya jiko kutokana na uhaba wa madarasa.

Bill alisema jengo hilo linatumika kwa muda na kwamba fedha zitakapopatikana litarekebishwa au kujengwa jipya litakalokidhi sifa za kuwa darasa la watoto wa awali.

“Hili jengo lilijengwa maalum kwa ajili ya jiko, lakini baada ya kuwapo na uhaba wa madarasa hasa la awali likiwa halipo kabisa na kijijini kuna watoto waliofikia umri wa kwenda chekechea ikabidi jengo hilo ndio litumike kama darasa ili watoto hao waweze kupata elimu ya awali ambayo kwa sasa ni ya lazima” alisema Bill.

Alisema kutokana na shule kujengwa na nguvu za wananchi bila msaada kutoka serikalini ujenzi wa shule hiyo kikiwamo choo kusuasua.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Benadeta Malisa alisema wanakabiliwa na uhaba wa madarasa, madawati, choo na ukosefu wa maabara.

Alisema hali hiyo inasababisha msongamano wa wanafunzi darasani hivyo kukosa mazingira mazuri ya kusomea na kusababisha kushuka kwa elimu, kuwa na ari duni ya kujifunza.
Pia alisema kuwa Shule ya Msingi Mkambarani yenye madarasa la awali mpaka la saba inakabiliwa na upungufu wa vitendea kazi kama vitabu vya kiada kwa walimu na wanafunzi.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles