Na ELIYA MBONEA-ARUSHA
SHIRIKA la Mfuko wa Msamaria la Marekani linaloendeshwa na Frankline Graham, mtoto wa Muhubiri maarufu duniani, Bill Graham, limetoa ndege kubwa kwa ajili ya kubeba wanafunzi majeruhi watatu wa ajali ya basi la Lucky Vincent iliyoua watu 35.
Ndege hiyo DC 10, inatarajiwa kuruka usiku wa leo (jana) Alhamisi kutoka Uwanja wa ndege wa Charllote katika Jimbo la North Carolina, Marekani na inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) leo.
Akizungumzia kukamilika kwa baadhi ya hatua za safari hiyo mjini hapa jana, mratibu wa safari hiyo, Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, alithibitisha kukamilika maandalizi ya safari hiyo.
“Kuna mambo nimeamua kuyasimamia, nimewasiliana na Shirika la Mfuko wa Msamaria linasimamiwa na Frankilin Graham mtoto wa Bill Graham nimewaeleza kilichotokea kwa watoto wakakubali kutoa ndege,” alisema Nyalandu na kuongeza:
“Tunashukuru Mungu Hati za kusafiria zimekamilika kwa wazazi, madaktari na watoto maandalizi ya VISA yanaendelea kushughulikiwa safari hii tunatarajia itakuwa Jumamosi (kesho) endapo tu VISA itakuwa imekamilika”.
Alisema ndege hiyo DC 10 baada ya kutoka KIA itakwenda moja kwa moja hadi Uwanja wa ndege wa Charllotte, North Calorina.
Alisema baada ya kuwasili uwanjani hapo Shirika hilo la Msamaria limeandaa ndege nyingine maalumu (Air Ambulance) itakayoondoka uwanjani hapo hadi Hospitali ya Mercy iliyopo Jiji la Sioux katika Jimbo la IOWA.