WASHINGTON, MAREKANI
RAIS wa Marekani, Donald Trump, amemfukuza kazi Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) James Comey, hatua ambayo imezusha shutuma kutoka kwa pande zote za kisiasa.
Utawala wa Trump umesema hatua hiyo imetokana na makosa kadhaa inayodai Comey alifanya hasa namna alivyoshughulikia sakata la barua pepe za aliyekuwa mpinzani wake mkuu katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo mwaka jana, Hillary Clinton.
Hata hivyo, hatua hiyo inaonwa na wakosoaji kama uingiliaji wa kisiasa wa uchunguzi unaoendelea kuhusu ushiriki wa Urusi katika uchaguzi huo uliomwingiza Trump madarakani.
Pande zote za vyama vya Republican na Democrat zimeelezwa kusikitishwa na hatua hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani imesema taratibu za kumtafuta mrithi wa Comey zitaanza mara moja na kwamba aliachishwa kazi kwa kuzingatia mapendekezo ya wazi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu Jeff Sessions na Naibu wake Rod Rosenstein.
Rosenstein amekosoa namna Comey alivyoshughulikia kashfa ya barua pepe za Clinton, ikiwa ni pamoja na kukataa kumfungulia mashitaka Julai mwaka jana na pia matamshi yake kwa umma kuhusu uchunguzi huo.
Kwa mujibu wa gazeti la LA Times, taarifa hiyo ya kumfuta kazi Comey ilimkuta ghafla kwa vile alifahamu kuhusu kutimuliwa kwake kupitia habari za televisheni wakati akizungumza na maafisa wa FBI mjini Los Angeles.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujasusi ya Baraza la Seneti, ambaye anatokea chama cha Republican, Richard Burr, amesema amepata wasiwasi kuhusu muda na sababu ambazo zimetolewa kuhusu kutimuliwa Comey.
Naye Seneta John McCain pia wa chama hicho anachotoka Rais Trump amesema hatua hiyo imethibitisha ‘haja ya kamati maalum ya bunge kuchunguza kwa haraka uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi wa 2016.
Chama cha upinzani cha Democrat pia kilikosoa muda ambao hatua ya kumfuta kazi Comey imechukuliwa.
Kiongozi wa chama hicho katika Bunge la Seneti, Chuck Schumer, amesema huu ni wakati mwafaka kumteua kiongozi maalumu wa mashtaka kusimamia uchunguzi huo juu ya uhusiano na Urusi.
Alionya hatua hiyo isipochukuliwa raia wa Marekani wana haki ya kuwaza kuwa Comey amefutwa ili kukwamisha juhudi za kukamilisha uchunguzi huo.
Ikulu imekanusha kuwa kutimuliwa kwa Comey kuna uhusiano wowote na masuala ya kisiasa.