33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

ULAJI MBOGA, MATUNDA JIONI UNAVYOCHOCHEA MATOKEO MAZURI DARASANI

Watafiti wamebaini kuwa watoto wanaokula chakula cha jioni kila siku kilichoambatana na mboga za majani hufanya vyema darasani

 

 

MATOKEO ya utafiti huu ni sababu tosha kwa wazazi kutokuwa na ‘msalie mtume’ kwa watoto wao wanaogomea ulaji wa mboga za majani na hata matunda.

Ni kwa sababu utafiti nchini Australia umeonesha kuwa kumalizia mboga za majani na matunda katika mlo wa jioni kila siku huwafanya watoto waamke siku inayofuata wakiwa vizuri kimasomo darasani.

Watoto ambao hula mboga za majani kwa mlo wao wa jioni kila usiku huchochea matokeo mazuri ya mitihani ya kuandika na uandikaji kwa usahihi, kwa mujibu wa utafiti huo mpya.

Hiyo inadhaniwa kuchangiwa na kile kinachofahamika kuwa mboga mboga zina utajiri wa antioxidants, ambayo huboresha chembe chembe za urithi (DNA) na kuzifanya ziwe na manufaa makubwa kwa ubongo.

Kwa taarifa antioxidants ni viini ambavyo vina uwezo wa kukinga seli za mwili zisiharibiwe na chembe chembe haribifu (free radicals) ambazo huweza kusababisha saratani.

Viini hivyo huungana na chembechembe hizo haribifu na kuzidhibiti ili zisisababishe madhara.

Mifano ya antioxidants ni pamoja na beta-carotene, lycopene, vitamin C, E, na A.

Tukirudi katika utafiti, watafiti kwa miaka mingi walikuwa wakiangalia zaidi athari za ulaji wa kifungua kinywa kwa watoto kwa ufanisi wa kitaaluma.

Kwa msingi huo, utafiti huu mpya ni wa kwanza kuangazia uhusiano wa kitaaluma na mlo wa jioni kwa watoto.

Utafiti ulibaini kuwa ulaji wa mboga mboga uliimarisha mafanikio ya watoto bila kujali kiwnago cha elimu ya wazazi wao.

Mwandishi kiongozi wa utafiti huo, Tracy Burrows, ambaye ni Profesa mwalikwa wa Chuo Kikuu cha Newcastle nchini Australia, anasema: “Matokeo hayo yametoa mtazamo wenye kufurahisha kuhusu mwenendo wa ulaji wa mlo wenye afya unavyoweza kuleta matokeo chanya ya mafanikio ya kitaaluma.”

Akieleza kuhusu utafiti huo, Louise Dye, profesa wa  nyendo na viinilishe katika Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza, anasema: “Kuna athari chanya ya mlo wenye afya kwa utendaji wa ubongo.

“viini vya polyphenols, ambavyo hupatikana kwa wingi katika mboga mboga na matunda, imeonesha kuwa na athari chanya katika ufanisi wa ubongo kwa watu wazima na watoto.”

Lakini pia anasema kuwa kunaweza kuwa na sababu nyingine kuelezea uhusiano baina ya mboga za majani na ufanisi shuleni.

“Kwa mfano, watoto walio katika makazi ambayo watu wazima huwapatia mlo wenye afya wana uwezekano mkubwa wa kupata msaada mwingine kama vile muda wa kujisomea na kufanya kazi za shule za nyumbani,” anasema.

Mafanikio ya mboga za majani kwa watu wenye umri mkubwa ziko wazi katika tafiti zinazoonesha kwamba mlo wa ki-mediterrania huzuia maradhi ya akili.

Kwa taarifa kile kiitwacho mlo wa kimediterania ni vyakula vinavyotokana na mimea kama vile matunda na mboga mboga, nafaka zisizokobolewa, jamii ya karanga.

Kadhalika kunahusisha utumiaji wa mafuta mazuri kama vile ya mizaituni badala yanayotokana na wanyama.

Hali kadhalika ni pamoja na kutumia viungo kutokana na miti na mbegu mbegu mahali pa chumvi kukolezea vyakula.

Mboga za majani na matunda zina utajiri wa ‘antioxidant’ zinazoboresha ubongo

Tukirudi faida ya mboga za majani na matunda, athari zake kwa watoto wenye umri wa miaka minane hadi 15 zilipimwa kwa kuwauliza wazazi namna wanavyokula vyakula katika mlo wao wa jioni.

Utafiti huo uliohusisha watoto zaidi ya 4,200 ulibaini kuwa watoto waliokula mboga za majani kila siku jioni kwa wiki walipata alama 86 katika majaribio ya kusoma, kuandika na kuhesabu.

Kuimarika kwa alama kulinganisha na watoto ambao hawakula mboga mboga katika mlo wowote wa jioni kulikuwa juu zaidi hasa katika uandikaji kwa usahihi na kuandika.

Utafiti huo uliochapishwa na jarida la Appetite, unaeleza kwamba mboga mboga za majani zina antioxidants, ambazo ni sawa na polyphenols na huimarisha DNA.

Timu ya utafiti uliona kwamba vinywaji vyenye carbohydrates kwa wingi vilisababisha watoto kufanya  vibaya shuleni.

Watoto walioripotiwa na wazazi wao kuwa angalau na unywaji wa glasi nne za vinywaji vitamu vyenye sukari, walipata alama 46 zikiwa chini ya wale waliokunywa kiwango cha chini cha glasi ya vinywaji hivyo.

‘Refined carbohydrates’ inayopatikana katika vinywaji hivyo ilionekana kupunguza kiwango cha ukubwa wa ubongo ikiwamo ‘kituo cha utengenezaji wa kumbukumbu’ kijulikanacho kitaalamu hippocampus.

Watoto ambao walikula vipande viwili vya matunda kwa siku walikuwa na kiwango kikubwa cha alama katika mitihani ya kuandika na kusoma, utafiti ulibaini.

Naveed Sattar, profesa wa utabibu wa metaboli katika Chuo Kikuu cha Glasgow, Scotland, alisema kuna sababu nyingine za kiafya na ustawi zinazoweza kusaidia utajiri wa mlo bora katika matunda na mboga mboga na vinywaji visivyo na sukari.

Anasema iwapo tutaweza kufanya iwe rahisi na nafuu kwa kila mtu kufuata mlo wa aina hiyo, tutegemee kila aina ya manufaa ya kiafya na ustawi wa binadamu ikiwamo ufanisi mzuri kimasomo darasani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles