Na Shermarx Ngahemera,
BARA la Afrika kwa ujumla wake limekosa la kufanya kutokana na tatizo linalokua kila siku la ajira kwa vijana, hivyo kusababisha kukosa utulivu na amani.
Wafadhili nao wakiwa wanafiki kwa kukosa maneno ya kusema zaidi ya kutoa hadahari suala hilo lishughulikiwe kiamilifu mapema kabla ya mambo hayajaenda kombo.
Tatizo kubwa Afrika ni namna ya kuzalisha ajira zaidi ya milioni moja kila mwaka kutuliza vijana wenye mihemuko ya maendeleo na mahitaji ili kuendeleza nchi zao.
Ajira katika nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA) ni muhali wakati idadi kubwa ya watu katika nchi hizo ni vijana chini ya mika 15; ni zaidi ya asilimia 47 na hivyo kuweka mahitaji maalumu kwa Afrika ikilinganishwa na mabara mengine. Kiumri bara la Afrika ni changa likiwa na wakazi wake wengi vijana wadogo wasio na elimu na wastani wa miaka 15 kuwa ndio wengi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), tatizo la ukosefu wa ajira mwaka huu litazidi kushuka na kufikia asilimia 10.8, kupungua huko kulianza mwaka 2012. Hata hivyo, hali hiyo si endelevu kwa miaka inayofuata kwa ajili ya kukosa msukumo wa mitaji na ukosefu wa viwanda ambavyo vingeweza kuajiri watu wake na mipango duni ya nchi 54 zinazofanya Afrika.
Takwimu zinaonesha kuwa wafanyakazi tisa katika ya kumi mashambani na mijini wana ajira zisizo rasmi na asilimia 38 ya watu hao wako tayari kuhama kufuata ajira za uhakika kokote zinakopatikana.
Kuzidi huko kwa makundi ya waliokosa ajira huvuka mipaka na kuleta athari kubwa mashambani na mijini na hata kwenye mipaka ya nchi za jirani zenye kuonesha unafuu fulani wa matatizo. Hivyo kufanya mwendelezo wa mataifa yaliyoshindikana (failed states) kuendelea kukosa amani na kuwa hazina ya wavunja amani kwingineko kwa kujiunga na makundi ya wavunja amani, majangili na wahafidhina wenye msimamo mkali dhidi ya Serikali zao na vibaka mijini.
Ingawa tatizo linaonekana kuwa ni kubwa kawa wakati huu ukweli ni kuwa hiyo ni sehemu ndogo tu ya tatizo ya lile linalokuja na hivyo matayarisho mahiri yanahitajika kupambana nayo siku za usoni.
Wingi wa watu Afrika unategemea kuongezeka na kuwa mara mbili ifikapo mwaka 2050, ambapo mamilioni ya watafuta kazi wataendelea kumwagikia kwenye ofisi za ajira ambazo hawana cha kuwapa na hali tete itaendelea kutesa na kuwa chungu zaidi kwa ushindani kupata kazi, mishahara duni na ubaguzi kujali zaidi watu wa kwenu au vigezo vingine zaidi ya elimu na ujuzi wa kazi.
Albert Zeufack yeye ni Mchumi Nguli wa Benki ya Dunia Afrika, anasema: “Nusu ya Waafrika ni vijana chini ya miaka 18 na kwa miongo mingine mingi hali itaendelea kuwa hivyo na kufanya kuwa kila mwaka kiasi cha watu milioni 190 wa umri wa miaka 15 na 24 wanaingia katika soko la ajira na hivyo kutaka Serikali za Afrika kufanya juhudi ya kushughulikia tatizo hilo kabla mambo hayajawa kombo kabisa.
Inatakiwa kufanya tathmini kwa viongozi wa Afrika kujua ni kwanini walipokea kwa shangwe ukuaji wa uchumi wa Afrika hadi mwaka 2014 katika kile kinachoitwa ‘Afrika Rising’ lakini hawakuweza kuweka misingi ya uchumi endelevu.
Matendo anayofanya Rais Dk. John Magufuli ya kufanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ni sahihi kwani itafanya nchi itoe fursa nyingi za kazi za moja kwa moja na zile za kupita na hivyo kulegeza makali ya kukosa ajira, vilevile umiliki wa ardhi ulio nafuu huwezesha wale wenye nia ya kilimo kuweza kufanya hivyo bila matatizo sana. Hivyo sekta ya kilimo kuweza kuajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania.
Mshauri wa Mataifa, McKinsey, anasema Afrika kwa kipindi kirefu watategemea hazina za malighafi kwa maendeleo yake.
Kuanzia mwaka jana, bei ya mazao ambayo nayo ilipanda kwa maana ya bidhaa za madini na malighafi nyingi kwa ajili ya viwanda ikiwamo dhahabu, shaba na mengineyo na hivyo kutoa fursa kwa chumi za Afrika kuinuka tena. Hivyo hii ni nafasi mwafaka kwa Afrika kuwa na mipango ya jumla ambayo itatoa nafasi kubwa ya uzalishaji ajira.
“Ni kwa kuwa na viwanda, mapinduzi ya kilimo na uongezekaji wa tija kwa shughuli mbalimbali ndio itawezesha kuepusha zahama itakayotokana na kukosa ajira kwani itaendelezwa na hatua hizo,” anasema Aeneas Chuma.
Migodi ya shaba ya Zambia, makaa ya mawe ya Msumbiji jimbo la Tete na chrome ya Zimbabwe na Afrika Kusini wafanyakazi wamerudi kutokana na mahitaji yaliyokuwa ya China na hivyo kufanya mwanzo kama watu watazingatia ongezeko la thamani na mipango thabiti ya ajira kwa watu wa nchi hizo.