28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

SERIKALI YAFANIKIWA KUPANGA MADARAJA YA HOTELI

Hoteli yenye hadhi ya nyota tano Serena, iliyopo jijini Dar es Salaam

 

 

Na ASHA BANI,

SERIKALI imefanikiwa kupanga madaraja ya hoteli zake baada ya mikwara mingi ya kutofanya zoezi hilo,  hatua ambayo imesifisiwa na wengi na kuleta tumaini la kuvutia watalii nchini.

Mahoteli hupanga madaraja yake katika ngazi tano na huzingatia kwa kiasi kikubwa huduma zitolewazo na hoteli hizo  kiushindani. Hii ni mara ya pili, mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana.

Tanzania kwa miaka mingi imeendesha biashara ya hoteli bila madaraja na kuleta matatizo mengi katika utozaji wa huduma zake na hivyo kwa kiasi fulani kuathiri mwenendo  wa biashara ya mahoteli.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema sekta ya utalii nchini inakua kwa kasi kutokana na vivutio vizuri  vilivyopo  nchini na mazingira ya mapokezi ambayo watalii wanayapata katika mahoteli mbalimbali  na amani iliyotamalaki nchini.

Maneno hayo aliyasema hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wakati wa kukabidhi vyeti vya kutambua hadhi za hoteli zilizopo kwa  kuzipa madaraja baada ya kuzikagua na nyingine  kufikia hadi nyota tano katika soko la utalii hapa nchini.

Alisema katika kipindi cha mwaka jana, watalii milioni 1.2 waliingia nchini Tanzania, huku Kenya ikiwa ni milioni 1.3  na nchi nyingine za Afrika Mashariki zikiwa na watalii wadogo zaidi, hivyo kuifanya Tanzania  kuendelea kujivunia na kuboresha mazingira zaidi.

Alisema biashara ya utalii  inachangia pato la Taifa kwa asilimia 25, hivyo ni muhimu katika kukuza uchumi kwani hutoa ajira kwa watu wengi  na huingiza fedha  nyingi za kigeni na  kuongeza pato la Taifa.

Katika  kupanga madaraja hayo, ni hoteli moja tu mwaka huu ya Serena imepita kuwa hoteli ya nyota tano zikifuatiwa na zile za nyota  nne za Double Tree na Ramada Hotel.

Kwa hoteli kuwa  ya daraja ya nyota tano inatakiwa kuwa  mahala pazuri (location) kuwepo  huduma  za bwawa la kuogelea,  sehemu ya kiwanja cha gofu au michezo  mingine zaidi ya gym, maduka ya huduma mbalimbali  ikiwemo ya kubadili fedha, vitabu na manukato, kituo cha biashara na huduma nyinginezo  kadha wa kadha.

Waziri alisema wametumia vigezo vya usafi wa mazingira kwa kutotiririsha maji machafu ovyo, huduma nzuri kama vigezo vya msingi kupata nyota yoyote ile.

Hoteli ya nyota tatu  ndio nyingi  na ni pamoja na Land Mark (Mbezi Beach)  Coral Beach, Ramada (ya Posta) Peninsula na Holiday Inn. Nyingine nyota tatu ni Saphire, Millenium Tower (Kijitonyama), Regency Park, Tiffany, SlipWay, Tanzanite na Hoteli ya Golden Tulip.

Baadhi ya hoteli za  nyota mbili ni pamoja na Shamool Hotel, City Style  na Mbezi Garden.

Akizungumza kwenye shughuli hiyo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Utalii Nchini (TCT), Abdulkadir Mohamed, alisema sifa  za hoteli hizo  zimezingatia viwango vya Afrika Mashariki, huku akiwataka wamiliki wa mahoteli kuendelea kutoa huduma bora zaidi ili kuvutia watalii.

Naye mmiliki wa Shamool Hotel iliyopo Sinza ambayo ilipata nyota mbili, Mariam Wadud, alisema licha ya kuwa biashara ni ngumu kwa sasa, wamejitahidi kuboresha huduma zao kwa kuzingatia matakwa ya wateja
ikiwa ni pamoja na malazi  mazuri, vyakula muda wote na kuwatembeza wageni katika maeneo mbalimbali wanayohitaji yakiwemo ya kitalii.

 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles