Na Mwandishi Wetu,
SERIKALI inatakiwa ijichunguze katika utekelezaji wa mipango yake ambayo inaonekana kuminya au kuvuruga masilahi ya uwekezaji kutoka sekta binafsi kabla mambo hayajaenda kombo kwao.
Kinacholalamikiwa na wengi ni kuwa kumeongezeka kuwapo kwa vitendo vya kushtukiza kwenye uchumi ambavyo huathiri mwenendo wa ustawi wa wafanyabiashara katika sekta mbalimbali na hivyo kuzua lawama, malalamiko na kufilisika kibiashara.
Nia ya Serikali kwa maendeleo ni nzuri lakini utekelezaji wa miradi umekuwa katika mtindo wa unyang’anyi na kutokujali athari zake kwa wafanyabiashara kama vile wao si kitu katika uchumi.
“Ni makosa kufikiri hivyo kwani wafanyabiashara ni injini ya kukua uchumi na wao ndio wenye uwezo wa kufanya mambo mengi na kwa wingi wao huleta tija katika uchumi husika,” anasema Godfrey Simbeye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Anasema hali imekuwa mbaya zaidi pale amabapo Serikali inatoa ushindani wa dhati kwa sekta hiyo kama vile haipo na hivyo kuashiria kukatika kwa mawasiliano kwa pande hizo mbili za uchumi yaani binafsi na sekta ya umma.
Mifano ni mingi lakini inatosha kusema ujenzi wa hosteli za UDSM, kazi za majengo ya Magomeni na ujenzi wa Chuo cha Muhimbili Mloganzila kuchukuliwa na Tanzania Buildings Agency (TBA), kuzuia zabuni kupewa watu binafsi kuendesha miradi TPA na ujenzi wa nyumba mbalimbali za wilaya nchini ni mifano halisi.
Wafanyabiashara wa majengo ya kukodisha eneo la Savei karibu na UDSM wanalamika kwa kusema wanasema kuwa hatua ya Serikali ya kujenga mabweni mapya ya Chuo Kikuu Cha Dares Salaam (UDSM) na nafuu ya pango iliyotoa kwa wanafunzi wa chuo kwa kupunguza kiwango cha pango kimevuruga uwekezaji na mwenendo wake katika sekta hiyo.
Vunja bei aliyoitoa Rais Magufuli kwa wanafunzi wa UDSM imegeuka kuwa mchunga kwa wamiliki wa nyumba za kupanga zilizo katika maeneo na taasisi hiyo kubwa ya elimu ya juu nchini.
Rais John Magufuli amezindua matumizi ya mabweni yenye uwezo wa kuwalaza wanafunzi 3,840 kutekelezwa na alienda mbali zaidi kwa kuamuru kupunguza kiwango cha pango kwa mwezi kwa kila mwanafunzi kutoka Sh 24,000 hadi Sh 15,000 na kuvunja ushindani kutoka mabweni ya watu binafsi katika eneo linalozunguka chuo hicho.
Rais alizindua hosteli hizo wiki mbili zilizopita na ujenzi wake umechukua chini ya mwaka mmoja na kugharimu Sh bilioni 10 na zilijengwa na TBA badala ya Sh bilioni 28 walizodai wajenzi binafsi.
“Choyo kwa kupata faida iliyopitiliza kutoka serikalini ndio ninachopinga na si kuwa adui wa wafanyabiashara ingawa inaonekana hivyo kwa watu wasio waaminifu,” alisema Rais Magufuli.
“Tunajenga nchi na watu lazima waweke uzalendo katika masuala haya ili nchi ipige hatua,” alisema.
Rais alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwekeza katika elimu hivyo itahakikisha wanafunzi nchini wananufaika kwa kupata elimu bora kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu. Elimu ni pamoja na makazi bora kwa wanafunzi husika.
Kwa miaka mingi wamiliki wa nyumba za kupanga walikuwa wakinufaika na ukosefu wa makazi ya kutosha chuoni hapo na hivyo wanafunzi kuwa wateja wao wakubwa na kuwapangisha kwa kiwango kikubwa cha kodi na masharti mengine yenye kero kwa walipakodi kukiwa na manyanyaso tele na kukosa utu wa kusubiri pale kodi ya pango inapochelewa kutolewa kwa wakati.
Kwa viwango vipya vinavyotakiwa kutozwa, kila mwanachuo atatakiwa kulipa sh 15,000 kwa mwezi na hivyo Sh 120,000 kwa miezi minane badala ya shilingi 200,000 zinazodaiwa na wapangishaji binafsi.
Kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na fedha ya kwenda na kurudi kutoka chuoni, ukijumlisha na nauli ya kila siku na muda mwanafunzi anapoteza akisubiri mabasi kituoni kwenda na kutoka chuoni.
Mambo si kuntu kwa Mariam Yohana anayesimamia hosteli zilizopo maeneo ya ‘Survey’ ambaye anaona mdororo wa ujaji wa wapangaji wake wanafunzi na kutishika kwa uhai wa biashara yake ya miaka mingi na kufichua kuwa kila mpangaji wake alikuwa anamlipa Sh 300,000 kwa miezi nane, ikiwa ni mara mbili ya kile watakacholipa kwa uongozi wa chuo kwa mabadiliko haya ya kodi.
John Massawe ni mmiliki, naye anasema hosteli yao kila mwanafunzi analipa Sh 300,000 kwa muhula mmoja na katika chumba kimoja wanakaa wanafunzi wanne. Anasema hosteli yake ina vyumba kumi na tano na hivyo kipato chake kiko hatarini na anaogopa anaweza kushindwa kulipa mkopo wake wa ujenzi na kuweka samani.
Lakini mmiliki mwingine mwenye hosteli iliyoko Sinza E, anayeitwa Godfrey Ulomi, anasema katika pango lake kila mwanafunzi analipa Sh 200,000 kwa miezi minane, hivyo ana wasiwasi wa kupata wateja wa kutosha baada ya mabweni ya Chuo Kikuu kufunguliwa. Yeye ana wanafunzi 20 kati yao wanawake ni wanne.
Ni furaha tele kwa Said Salum ambaye amepata nafasi katika ‘mabweni ya Magufuli’ na kuondokana na adha ya kuishi maeneo ya Sinza ambapo mwenye nyumba alikuwa na manyanyaso.
“Mimi hapa hulipa Sh 350,000 kwa mwaka yaani kila muhula nalipa Sh 175,000 ila sasa huyu baba mwenye nyumba ana mke mdogo ambaye ulimi wake ni mkali kama kisu kwa kutochagua neno la kusema kama atacheleweshewa kodi kwa madai kuwa maisha yake yanategemea kodi hiyo tu. Huwa hasikilizi mtu,” anasema Said. Anasema kunaokoa matumizi mengi kwa kuishi chuoni.
Manonga Josephat anadai kuwa si siri wanafunzi wengi walikuwa wanashinda na njaa kwa sababu fedha zote wanalazimika kumpa mwenye nyumba na hivyo kuwa kero kwa masomo yao.
Suala la Usafiri nalo linawaumiza zaidi kwani ulipaji wa nauli na chakula ulikuwa unafanya mikopo wanayoipata kutokidhi haja na ilibidi waishi kwa mbinu na mbinde, mwenendo usiolingana na hali ya kubobea kusoma.