Na JOSEPH LINO,
NDOA ya kwanza ni ya Adam na Hawa. Haikuwa na sherehe wala mbwembwe nyingi lakini ilifana sana, kwani ilidumu miaka si chini ya 900. Msingi wa ndoa hiyo ni upendo na si mali wala tamaa ya sifa. Haikuwa na shuhuda ila Mungu Mwenyezi. Harusi ni matokeo ya ndoa ambayo ni takatifu bila hiyo hakuna harusi au sherehe.
Sherehe za harusi ndizo zimekuwa kikwazo kwa vijana wengi kuoa na kuolewa kwani mahitaji yake yamekua kuliko uwezo wa wengi kama tutakavyobainisha katika habari hii ambayo imetayarishwa kwa mazingira ya jiji la Dar es Salaam; jiji lenye idadi ya wakazi inayokaribia milioni tano kwa mujibu wa Sensa na Makazi ya mwaka 2012.
Wafanyabiashara wamezikomalia harusi kwani zina kipato kikubwa na hupatikana kwa saa chache. Uwekezaji mwingi umefanyika katika kumbi, muziki, mavazi, chakula, mapambo, usafiri na sherehe. Watu wengi wametajirika kwa shughuli za harusi. Huwaambii kitu!
Lakini kuna kasoro moja kwamba Serikali haipati chochote kutokana na makusanyo hayo ya pesa au haijatambua kuwa ni chanzo kimojawapo kikubwa tu cha mapato kama itakuwa makini.
Harusi imekuwa biashara kubwa ambayo kwa namna nyingine tunaweza kusema sekta ndogo ya harusi ambayo inajumuisha huduma zote zinazotolewa ikiwemo, kumbi, washereheshaji (Mc’s), chakula na vinywaji, picha na video, nguo, usafiri, mapambo na saluni. Vyote hivyo huchukua muda na gharama kubwa kufanya matayarisho ili watu wafurahie na kukumbuka siku hiyo kuwa ilifana sana. Kamati ya harusi ndio msingi wa sherehe yote na wengine ndio wamebobea na kufanya kuwa taaluma. Wanakodishwa.
Si kitu cha kushangaza kuona watu wanatumia mamilioni ya pesa kwa ajili ya harusi ambayo ni biashara kubwa maeneo ya mijini kama Dar es Salaam ambako kuna mkusanyiko mkubwa wa watu wa tamaduni mbalimbali na hivyo harusi hukusanya waliomo na wasiwamo ila wote wanafanikisha shughuli.
Watu hususani vijana huwa na ndoto ya kufanya harusi ya kifahari au gharama kubwa ili ionekane kuwa ni kitu muhimu pekee kwao.
Kwa mtazamo huo finyu, upendo kwa wanaooana unapimwa kwa kiwango cha fedha wanazotumia kwenye harusi yao.
Kufanya harusi ni gharama kubwa na kiwango cha chini ni Sh milioni tano kufanikisha starehe ya saa chache kwa siku moja ambayo haina umuhimu sana katika taratibu za kidini.
Kwa mtazamo wa Mchungaji, Yared Dondo wa Kanisa la TAG City Harvest, anasema sherehe ya harusi si muhimu sana, muhimu ni ndoa na mawazo yanatakiwa yawe kwenye ndoa na si harusi.
“Hata kama nikifungisha ndoa na baadaye tukanywa soda tu, haina shida kanisa linaangalia ndoa si harusi. Lakini sherehe za harusi hazikatazwi kama mtu ana uwezo nazo tunasherekea kama kawaida, lakini si kikwazo cha kutokufunga ndoa. Ndoa ndio takatifu na si harusi,” alisema.
Kutokana na uhitaji mkubwa kwa watu kufanya harusi, kumekuwapo na ongezeko kubwa la gharama za huduma mbalimbali za harusi ambazo hufanywa siku maalumu za juma ikiwamo Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili; zimefanya sekta hiyo kuwa biashara kubwa.
Gharama za harusi
Kumbi za harusi zimevutia watu wengi kuwekeza katika biashara hii ambayo miaka ya hivi karibuni kukodi ukumbi wa harusi ni gharama ya juu kutokana na uhitaji mkubwa.
Kama ilivyodokezwa awali, harusi za Kikristo ni ghali kwani kuna mahitaji mengi katika shughuli tatu za Ndoa, Send off (Kikeni)Kitchen Party na Reception (harusi) kwenye kumbi. Watu hula chakula kizuri na kunywa kilevi na muziki wa dansi.
Wakati huo, Waislamu wana ndoa, ‘Kitchen Mada’ inayoshabihiana na Kitchen Party; hii ikiwa ni zaidi kwenye mafunzo ya dini ya Kiislamu na sherehe holini kwa wale wenye uwezo ili kupata zawadi na pongezi za tafrija hasa chakula kingi kizuri. Haya ni ya kileo kwani Taifa limechangamana na hivyo kufanya matendo hayo kufanana kwa mengi na yale ya Kikristo isipokuwa hakuna kilevi katika sherehe za Waislamu na hivyo kufanya gharama kupungua sana. Vile vile kwa Waislamu wanafanyia shughuli ya harusi nyumbani kwa bibi harusi kusiko na gharama na kwenye kumbi ni kwa fahari tu na si lazima.
Kumbi za harusi nyingi zilizopo jijini Dar es Salaam hutoza gharama kubwa. Zilizopo maeneo ya kuzunguka jiji kama Sinza, ni kuanzia Sh milioni 1.5 mpaka Sh milioni 3 kwa ukumbi kufuatana na uwezo wake wa kuingiza watu kwa mfano kuna ukumbi ambao huingiza watu zaidi ya 500, 1000 au zaidi.
Kwa mfano ukumbi wa Mlimani City hutoza kuanzia Dola za Marekani 3,500 sawa na Sh milioni 7.8 kwa watu 250, ukumbi watu 500 unalipia Dola za Marekani 6,000 sawa na Sh milioni 13.5 na watu 750 ni Sh milioni 21.4. sawa na Dola 9,500 kwa nafasi tu, meza na viti bila mapambo. Chakula unaweza kuleta mwenyewe au kuagiza hapo hapo.
Kwa upande wa gharama za chakula bila kujumuisha vinywaji, sahani moja ya chakula ni Sh10,000 mpaka Sh35,000.
Kumbi za Harusi
Ukumbi wa Diamond Jubilee uliopo Upanga, Dar es Salaam ambako watu wengi hufanyia harusi zao hasa Wahindi, unakodishwa kwa Sh milioni 6 kwa watu 2,800, hata hivyo kwa ukumbi wa VIP ni Sh milioni 8.5 kwa watu 550.
Gharama hizo ni za ukumbi tu, vitu vingine vyote inakuwa juu ya mteja mwenyewe.
Kwa upande wa Ukumbi wa Blue Pearl unaanzia Sh milioni 2.5, huku chakula kwa kila sahani ni Sh 25,000 na vinywaji vyote vya kawaida huuzwa kwa bei ya Sh 2,000.
Ukumbi wa Cutch uliopo Mnazi Mmoja, Posta, unalipia Sh laki nane kwa kumbi mbili ikijumuisha sherehe ya wanawake na wanaume, hii ni hususan kwa sherehe za Kiislamu ambapo mapambo, chakula na vitu vyingine ni gharama za mteja mwenyewe.
Katika usafiri, gari la kubeba bwana na bibi harusi si chini ya Sh. 250,000 mpaka Sh.500,000 kutegemea aina ya gari, hapo pia kuna gharama za usafiri wa kubeba wazazi wa pande zote mbili kwenda ukumbini kwa ujumla inaweza ikatumika zaidi ya Sh milioni mbili.
Pia kila harusi huenda na mapambo katika ukumbi; kiwango cha chini ni kuanzia Sh milioni 1.5 hadi Sh milioni 5 au zaidi kulingana na mahitaji na ukubwa wa ukumbi.
Gharama za kupamba bibi harusi saluni ya kawaida ni kuanzia Sh.250,000 hadi Sh.500,000 huku picha na video kugharimu Sh milioni moja hadi Sh milioni tatu.
Kwa upande mwingine gharama kubwa ni mavazi ya harusi ikiwa nguo ya bibi harusi inaanzia Sh.500,000 hadi Sh milioni moja ya kukodi na ya kununua ni zaidi ya shilingi milioni moja na kuendelea pale Kariakoo, suti ya bwana harusi huuzwa Sh.500,000 hadi Sh milioni moja. Hapa pia kuna gharama zaidi ya viatu na tai na vitu vingine vidogo vidogo ambazo pia ni gharama kubwa.
Harusi ili ikamilike pia kunahitajika pete za maharusi ambazo pete za kiwango cha kawaida ni kuanzia Sh.200,000 kuendelea ambapo inafikia hadi Sh milioni 2 kutegemea na kiwango cha madini ya dhahabu yaliyopo ndani ambayo gharama inaweza kupanda zaidi kwa uzito wake mkubwa au nakshi iliyotoneshwa kwenye pete hiyo ya dhahabu.
Mary Mallya hufanya biashara ya kupamba kumbi za harusi, sherehe za kuaga biharusi (sendoff) na kupeana vyombo (kitchen party), anasema gharama za upambaji zinategemea mahitaji ya wenyewe lakini haiwezi kupungua chini ya Sh milioni moja.
Peace Yared wa MaryGold Wedding Planner, anaelezea namna ya gharama zinazotumika katika maharusi na sendoff, kuwa kila mteja anakuwa na mtazamo wake namna harusi yake anataka ionekane.
“Ni gharama kubwa sana kwa siku hizi kuandaa sherehe za harusi, ila kila mtu na uwezo wake wa bajeti ambayo inatoa mwongozo mzima wa harusi itakavyokuwa,” anafafanua.
Kero za michango
Watu wanakutana kila wiki kwenye Bar katika vikao vya maandalizi ya harusi au send off ambavyo huchukua zaidi ya miezi miwili na wanapokutana hugharamia vikao vyao kwa kile kinachoitwa ‘uchakavu’.
Jambo kubwa linalozungumzwa ni masuala ya michango hasa namna watu watahamasishwa kukusanya michango hiyo na kupata taarifa mbalimbali za huduma.
Katika hali isiyo ya kawaida, siku hizi kero ya kufuatilia michango imekuwa ni kubwa kutokana na hali ya uchumi inavyokwenda.
Heri Mpashe, mkazi wa Manzese anasema uchangiaji huu umekuwa kiholela kwani bwana na bibi harusi watarajiwa wanatakiwa wawe na utaratibu wa kugawa kadi na si tu kuwasumbua watu kila siku.
“Kadi za michango zimekuwa kero kiasi kwamba ndani ya mwezi mmoja ukiwa maarufu unaweza kugawiwa kadi zisizopungua 10 na wote wanataka mchango usiopungua Sh 50,000, kwa namna hii hatuwezi kwenda kabisa,” anasema Mpashe.
Anasema Watanzaia tunahitaji kubadili mitazamo isilenge zaidi katika uchangiaji wa harusi, tunahitaji kuchangia zaidi katika elimu kwani kuna vijana wetu hawana hata dawati la kukalia, yatima, wajane na wengine wengi wenye mahitaji mbadala ya kuchangia harusi. Tusichangie kwenda kuzila wenyewe hizo fedha bali ziwe kupunguza madhila ya jamii.
“Raia masikini hulazimika kuchanga pesa nyingi na wengi hulazimika kuingia kwenye mikopo ambayo huwatesa mno, mtu hulazimika kuchangia hata kama hana pesa kwa kuogopa kutengwa na jamii,” anasema.
“Mimi nimeshafanya uamuzi wa kutochangia harusi ovyo na viwango vya kuchangia wanavyoviweka havinipi shida kwa sababu harusi za watu nisiowajua siendi hata nikipewa kadi,” anaongeza.