26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WASIRA ARUDI KORTINI KUMNG’ANG’ANIA BULAYA

Na KULWA MZEE, DAR ES SALAAM


MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania imepanga kusikiliza rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Bunda Alhamisi ya wiki hii.
Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo jana katika rufaa iliyokatwa na wapigakura wanne wa jimbo hilo.

Hiyo ni baada ya jopo la majaji watatu kukwama kuanza kuisikiliza kwa sababu  ya makosa yaliyofanyika na kusababisha Wakili wa Mbunge wa Bulaya, Tundu Lissu, kutopata notisi ya kuitwa mahakamani.

Jopo la majaji linaloongozwa na  Jaji Mbarouk Mbarouk liliahirisha usikilizwaji huo hadi keshokutwa na kuamuru makosa hayo yasirudiwe   kwa kuwa yamewapotezea muda.  

Warufani hao wanawakilishwa na  mawakili, Yassin Member na Constantine Mutalemwa huku Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiwakilishwa na Mawakili wa serikali, Obadia Kamea na Angela Msagala.

Lissu, wakili wa mjibu rufani wa kwanza ambaye ni Bulaya,   hakuwapo mahakamani hivyo  mawakili wa wakata rufaa waliomba kesi iahirishwe kwa muda mfupi kutokana na umuhimu wake.

Jopo hilo, Jaji Mbarouk,  Augustino Mwarija na Rehema Mkuye, lilikubaliana na ombi hilo, hivyo kuamua kuahirisha usikilizwaji huo hadi keshokutwa.

"Inasikitisha, haipendezi mnaopeleka notisi muwe makini kwa sababu mnatupotezea muda wakati tuna mambo mengi ya kufanya.

“Hili kosa lisijirudie, sisi tulikuwa tayari kusikiliza na tulipanga kesi moja tu,"alisema Jaji Mbarouk.

Wakata rufaa katika kesi hiyo ya uchaguzi Jimbo la Bunda ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagila ambao walikata rufani dhidi ya Bulaya, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Wakili Mutalemwa alitaja sababu za kukata rufani  hiyo kwamba uchaguzi haukuwa huru na haki kutokana na kuwapo   ukiukwaji wa wazi wa sheria za uchaguzi na kanuni.

Alidai tafsiri isiyo sahihi ya kanuni za uendeshaji kesi za uchaguzi kuhusiana na viapo na kutofuatwa   taratibu za uchaguzi kwa kutomuarifu mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mahali na tarehe ya kujumuisha kura na taarifa ya mwisho ya matokeo kuwa na idadi kubwa ya waliojiandikisha kupiga kura tofauti na Tume ya Uchaguzi ya Taifa.
Alidai sababu nyingine ni Mahakama Kuu kuifuta kesi kwa sababu wananchi wa Bunda ni masikini na utakuwa mzigo kwa Serikali kurudia uchaguzi.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles