29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

DIAMOND, MPOTO WAWAFARIJI WAFIWA KWA WIMBO ARUSHA

 

 

Na MWANDISHI WETU, ARUSHA

MSANII wa Bongo Fleva, Nassib Abdul na msanii wa muziki wa asili, Mrisho Mpoto, wamewafariji wazazi, ndugu jamaa, marafiki na Watanzania wote walioguswa na vifo vya watoto 33 wa Shule ya Msingi, Lucky Vincent ya mjini Arusha, walimu wawili na dereva aliyekuwa akiendesha basi aina ya Mitsubishi Rossa lenye namba za usajili T. 871 BYS ambalo ndilo lililopoteza maisha yao kwa wimbo wa maombolezi ya tukio hilo.

Nyimbo za wasanii hao zilifikishwa kwa mwendesha tukio hilo la kuagwa miili ya watoto na walimu wa shule hiyo kwa namna tofauti kwenye Uwanja wa Kumbukumbu wa Shekhe Amri Abeid mjini Arusha.

Lakini licha ya kufikishwa kwa aina yake, nyimbo hizo mbili zilipata nafasi ya kuchezwa na kusikilizwa na waombolezaji waliokuwepo uwanjani hapo na wale walioshuhudia tukio hilo jana mubashara kupitia runinga zao.

Nyimbo hizo zote zina maneno ya kufariji na kutia moyo sana kwa wafiwa, pia zimeelezea uchungu na majonzi mazito ya Taifa kupitia msiba huo ambao ni sikitiko kubwa kwa Taifa zima, huku majirani zetu Wakenya wakitutumia salamu za pole kwa tukio hilo kubwa.

Awali msanii Mrisho Mpoto alidai kwamba alikuwa na mpango wa kutunga wimbo juu ya wanafunzi hao ikiwa kama sehemu ya kuwaenzi, lakini alikuwa akifuatilia tukio hilo ili awe na historia nzuri itakayomuongoza kuhusu ajali hiyo na idadi kamili ya waliofariki kwa ujumla.

“Tangu juzi nilikuwa na wazo la kutunga wimbo ila nilikuwa nikifuatilia baadhi ya mambo ili niwe na historia nzima ya tukio zima ili wimbo ninaoandika uwe na maelezo ya kutosha na ndicho nilichofanya na nipo pamoja na wafiwa wote kipindi hiki kigumu,” alisema Mpoto.

Licha ya wasanii hao maarufu kufanikiwa kuandika na kurekodi nyimbo hizo, wasanii wengine wengi wametuma salamu za pole kupitia akaunti za mitandao yao mbalimbali ya kijamii kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa familia hizo kwa lengo la kuwafariji na kuonyesha umoja wao katika kipindi hiki kigumu cha msiba mzito wa kitaifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles