29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MZAZI ASHUHUDIA MAUTI YALIYOMKUTA MWANAE

Wananchi wakiwa nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mount Meru, Arusha kwa ajili kutambua miili ya wanafunzi

 

 

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

MMOJA wa wazazi ambao watoto wao wamefariki katika ajali ya gari iliyosababisha vifo vya wanafunzi 33 wa Shule ya Msingi Lucky Vincent, alikuwa miongoni mwa mashuhuda wa ajali hiyo pasipo kujua kama mtoto wake, Justine Alex, alikuwamo katika msafara wa gari hilo.

Mzazi huyo, aliyetambulika kwa jina la Lemburis Saruni, inadaiwa kuwa  alishuhudia ajali hiyo akiwa kwenye gari la  nyuma, huku lile lililobeba wanafunzi  hao likiwa mbele.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, ndugu wa karibu na Lemburis ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema baada ya kuona gari hilo limeanguka kwenye korongo alilazimika kushuka ili kwenda kuangalia bila kujua kama mtoto wake ni miongoni mwa waathirika wa ajali.

“Hiyo ajali imeua ndugu zangu, akiwamo mtoto wa baba yangu mdogo, na yeye leo alikuwa anakwenda Ngorongoro, alifuatana na hilo basi la wanafunzi bila kujua na  kaliona likidondoka, akashuka akalifuata akakuta mwanawe ndio yupo ananing'inia mlangoni,” alisema ndugu huyo.

Alisema baada ya kumuona akiwa katika hali hiyo, alilazimika kumwondoa na kumuweka pembeni, lakini kwa bahati mbaya alikufa akiwa amemshika mkononi.

Alisema Justine alikuwa mtoto pekee wa Lemburis. Alisema mama wa Justine alifariki dunia mwaka juzi.

Gazeti hili lilijaribu kumtafuta mzazi huyo kwa njia ya simu ya kiganjani ili aweze kuelezea tukio hilo, lakini hakupatikana hewani.

Mbali na mtoto huyo, mtoa taarifa alibainisha kuwa ajali hiyo huenda ikawa imesababisha vifo vya ndugu zao wengine watano ambao walikuwapo katika msafara huo, ambao ni wanafunzi na walimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles