22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

MSIBA WA TAIFA

Wananchi wakisaidia kutoa miili na majeruhi katika basi la wanafunzi wa Shule ya Lucky Vincent Nursery & Primary School ya Arusha baada ya kupata ajali katika Mlima Marera, Kijiji cha Rhotia wakati wakielekea wilayani Karatu mkoani Arusha kwa ziara ya masomo na mitihani.

 

 

Na WAANDISHI WETU-ARUSHA/ KARATU

NI msiba mzito si tu kwa wazazi na walezi, bali na Taifa kwa ujumla, baada ya ajali ya basi kupoteza maisha ya watoto 33, ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ya mjini Arusha.

Katika ajali hiyo, iliyotokea jana saa 3:00 asubuhi, mbali na wanafunzi hao 33, walimu wawili na dereva mmoja wa basi aina ya Mitsubishi Rossa lenye namba za usajili T. 871 BYS, nao walipoteza maisha baada ya gari hilo kutumbukia kwenye korongo lililopo Marera, eneo la Rotia, wilayani Karatu.

Ajali hiyo ilitokea wakati wanafunzi pamoja na walimu wao wakielekea wilayani Karatu kufanya mtihani wa ujirani mwema (joint examinations) na wanafunzi wenzao wa Shule ya Tumaini Junior School.

Katika matokeo ya mwaka jana ya darasa la Saba, shule hiyo ya Lucky Vincent ilishika nafasi ya pili kimkoa.

Kitaifa katika matokeo hayo ya mwaka jana ilishika nafasi ya 20 kati ya shule 8,109.

Inaelezwa kuwa, wakati gari hilo likipata ajali tayari magari mengine mawili yaliyokuwa yamebeba wanafunzi wa darasa la Saba na Nne wa shule hiyo yalikuwa mbele yakiendelea na safari na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wote waliokuwa wakielekea kwenye mtihani huo kuwa 96.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema chanzo chake bado kinaendelea kuchunguzwa kutokana na dereva mwenyewe kupoteza maisha.

 “Mahali palipotokea ajali kuna mteremko mkali sana, lakini wakati saa 3:30 asubuhi ajali ilipokuwa ikitokea mvua ilikuwa inaendelea kunyesha.

“Mpaka sasa taarifa za awali tulizo nazo waliopoteza maisha ni 33 na majeruhi ni watatu. Na Jeshi la Polisi tunaendelea na uchunguzi wa kitaalamu wa ajali hii,” alisema Kamanda Mkumbo.

MASHUHUDA

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika eneo la tukio, wananchi wanaoishi eneo hilo la Rotia walidai kuwa, gari hilo lilionekana kuendeshwa kwa mwendo kasi huku mvua ikiwa inanyesha.

Mkazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Andrew Burra, alilimbia MTANZANIA Jumapili kuwa, aliliona basi hilo likipita kwa mwendo kasi likiwa linatokea Arusha kuelekea Karatu.

 "Nikiwa kituo cha magari hapa Rotia nililiona basi hilo likipita kwa kasi, ilikuwa aaa 3:30 asubuhi. Na baada ya dakika tano hivi nikasikia kuwa basi hilo limepinduka kwenye mteremko mkali wa Mlima Marera likiwa na wanafunzi,” alisema Burra na kuongeza:

"Kwa mazingira ya mvua na kasi aliyokuwa nayo dereva, kwa kweli kulimudu gari lile ilikuwa vigumu sana, kwani ilikuwa ngumu kuona hata mita 10 mbele yako," alisema.

Shuhuda mwingine aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa, aliliona gari hilo linashuka kwa kasi kwenye mteremko huo mithili ya kwamba lilikuwa limekata breki.

Kwa mujibu wa shuhuda huyo, gari hilo lilionekana kumshinda dereva na hivyo kutumbukia kwenye korongo lenye kina cha urefu wa takribani futi 28 ambalo lipo  upande wa kushoto wa barabara hiyo.

Alisema baada ya ajali kutokea, alifika eneo la tukio mara moja kwa ajili ya kusaidia uokoaji  ambapo mtu wa kwanza kumwona ni dereva ambaye alikuwa tayari amekufa.

Alisema dereva huyo alikuwa amekatwa vibaya na vipande vya chuma na mwili wake ulikuwa umebanwa karibu na tairi la mbele upande wa kulia, huku utumbo ukiwa nje.

Alisema aliona hali mbaya zaidi kwa abiria waliokuwamo ndani ya gari hilo ambapo wengi wao walikuwa wamepoteza maisha. 

“Viti vyote vilikuwa vimeng’oka, kasoro viwili tu vya nyuma. Tumewakuta watoto kama 11 tu ndio wako hai, lakini wengine wote walikuwa wamepoteza maisha. Yani gari hii ni Toyota Coaster lakini imekuwa fupi kama Toyota Noah,” alisema shuhuda huyo.

Katibu wa Hospitali ya Lutheran Karatu, Bahati Meshack, alithibitisha kupokea miili 33, ambao wote walikufa pale pale katika eneo la tukio.

Miili hiyo ilihifadhiwa kwa muda katika Hospitali ya Lutheran Karatu, kabla ya baadaye jana mchana kuhamishiwa katika Hospitali ya Mount Meru.

Akizungumza nje ya Hospitali ya Lutheran, Karatu, mmoja wa walimu wa shule hiyo, Ephraim Jackson, alisema safari ya kuelekea Karatu wakitokea Arusha ilianza mapema alfajiri jana.

 “Tulikuja Karatu ili kufanya mtihani wa ujirani mwema na Tumaini Junior, lengo letu hakika limekatishwa na ajali. Tuliamka alfajiri kuwahi mtihani watoto wote wakiwa na afya njema na ari kubwa ya kufanya vizuri,” alisema Mwalimu Jackson, aliyekuwa gari la mbele na kuongeza:

“Bahati mbaya ndoto zao zimezimika katika ajali hii, ni masikitiko na simanzi kuu isiyoelezeka,” alisema.

ENEO LA SHULE/ HOSPITALI

Taarifa za ajali hiyo zilionekana kuwashtua na kuwachanganya baadhi ya wazazi na walezi ambao watoto wao wanasoma katika shule hiyo na hivyo kufurika shuleni hapo ili kujua hatima ya watoto wao.

Baadhi ya wazazi walionekana kutokuwa na taarifa sahihi, hali ambayo ilionekana kuzidi kuwavuruga.

SAA 12:18 JIONI MOUNT MERU

Kutokana na shauku ya kuona miili ili kuwatambua watoto wao, baadhi ya wazazi waliofurika katika uzio wa viwanja vya chumba cha kuhifadhia maiti walianza kufanya vurugu, ikiwamo kurusha mawe wakishinikiza kuingia ndani.

Vurugu hizo zilijitokeza baada ya kutangaziwa kuwa zoezi lote la kutambua miili litaendelea leo, hali iliyowafanya wazazi na ndugu wa marehemu kugoma kuondoka eneo hilo.

Mbali ya askari polisi wenye silaha kujitahidi kuwazuia, hali iliendelea kuwa tete kiasi cha kumlazimu Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daggaro, kutangaza utaratibu wa kusoma majina ya marehemu na kisha wazazi husika kuingia ndani kutambua miili.

Katika hali ya taharuki, wazazi ambao hawakusikia majina ya watoto wao walitakiwa kwenda Kituo Kikuu cha Polisi mjini kuonana nao, kwani walikuwa salama.

Kabla ya utaratibu huo kutangazwa, kuanzia saa tano asubuhi tayari mamia ya wananchi wa Jiji la Arusha na vitongoji vyake walikuwa wamefurika katika viwanja vya Hospitali hiyo, hususan katika eneo la viwanja vya chumba cha kuhifadhia maiti.

Wengine walionekana wakipita kwenye wodi za wagonjwa, wakitafuta watoto wao, hali iliyoonekana kuwapa wakati mgumu askari wanaosimamia usalama hospitalini hapo.

Majira ya Saa 11:07, wakati miili hiyo ilipoanza kuwasili kwa ajili ya taratibu nyingine za kidaktari, vilio katika eneo hilo la hospitali viliongezeka.

Awali Mkuu huyo wa Wilaya, Daqqaro akiwa hospitalini hapo alitangaza siku ya kesho kuwa maalumu kwa ajili ya Ibada na Dua ya kuaga miili ya marehemu hao katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, mjini Arusha.

“Miili mingine imeshawasili hospitalini, tunaendelea kusubiria magari mengine yanayoleta miili ya marehemu, huu ni msiba mzito sana, zaidi ya watu 32 wamefariki, ambapo majeruhi watatu, mmoja tayari yupo ICU,” alisema DC Daggaro jana jioni. 

Habari hii imeandaliwa na ELIYA MBONEA, ABRAHAM GWANDU NA JANETH MUSHI -ARUSHA 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles