26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

KERO YA MAJI CHALINZE YAMTESA RIDHIWANI

NA PATRICIA KIMELEMETA – PWANI


MBUNGE wa Chalinze, mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete, ameahidi kushughulikia tatizo la maji linalowakabili wananchi wa jimbo hilo.

Ridhiwani alisema mkakati uliopo ni kuhakikisha anasimamia upatikanaji wa maji kutoka Mto Wami na kuongeza idadi ya visima ili wananchi wa jimbo hilo waweze kupata huduma hiyo.

Alisema mbali na uhaba mkubwa katika baadhi ya maeneo, kukatika kwa maji mara kwa mara, ni tatizo jingine linalokera wananchi wa Chalinze.

Ridhiwani alisema mkakati aliokuwa nao awali umewezesha kuchimba visima katika vijiji mbalimbali jimboni humo ili kupunguza ukubwa wa tatizo.

“Tangu niingie madarakani, nimeweza kuchimba visima katika vijiji mbalimbali ili kupunguza ukubwa wa tatizo, jambo ambalo limechangia wananchi walio pembezoni na makao makuu ya halmashauri kutokuwa na shida kubwa ya maji kama ilivyokuwa awali,” alisema Ridhiwani.

Baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Chalinze wameitaka Serikali kushughulikia kero ya maji ili waepukane na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

“Chalinze tuna tatizo sugu la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa miaka mingi, hali iliyosababisha kwenda umbali mrefu kutafuta maji katika marambo au mabwawa ili tuweze kutumia,” alisema Amina Semindu.

Alisema licha ya kuwapo Idara ya Maji ya Mto Wami, lakini mashine ya kusukuma maji imekuwa ikiharibika mara kwa mara, jambo ambalo limechangia wananchi kuendelea kutaabika na huduma hiyo muhimu.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Abdallah Omary, alisema kuwa Serikali inapaswa kuangalia sababu ya kuharibika mara kwa mara kwa mitambo ya kusukuma maji.

“Pale Idara ya Maji kuna tatizo… kwa sababu kila siku mashine zinaharibika jambo ambalo limesababisha wananchi kuendelea kutaabika na huduma hiyo… Tunaiomba Serikali kutumia jicho lake ili waweze kujua chanzo cha tatizo,” alisema Omary.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles