PATRICIA KIMELEMETA NA LEONARD MANG’OHA
-DAR ES SALAAM
TUKIO la umwagaji damu lililotekelezwa na wafuasi wa Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba wiki iliyopita, limezidi kuchafua hali ya hewa ndani ya chama hicho.
Wakati Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akishindwa kuhudhuria kikao cha suluhu kilichoitishwa na Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, Jeshi la Polisi kwa upande wake lilitangaza kuchukua hatua mbili tofauti.
Miongoni mwa hatua hizo ni kumkamata Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya na wenzake sita, wakihusishwa na tukio la kuvamia na kujeruhi watu mbalimbali, wakiwamo waandishi wa habari waliokuwa katika mkutano wa Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kinondoni anayemunga mkono Maalim Seif wiki iliyopita.
Hatua nyingine ni kupiga marufuku kufanya usafi katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, zilizoko Buguruni, Dar es Salaam.
Mambo hayo yote yametokea ikiwa ni siku moja tu baada ya wabunge na wanachama wanaomuunga mkono Maalim Seif kutangaza kwenda kufanya usafi katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, zilizoko Buguruni, kwa kuondoa wale waliowataja kuwa ni wahuni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alisema pamoja na Kambaya, pia wanamshikilia Twaha Abdallah (47).
“Hawa tunawashikilia na jalada lao tayari limepelekwa kwa wakili wa Serikali muda wowote watafikishwa makamani.
“Pia tunaangalia malalamiko ya wale waliokuja kulalamika kuwa wamejeruhiwa, akiwamo yule aliyekatwa na panga, huyu yupo Hospitali ya Muhimbili anaendelea na matibabu na tunamsaka aliyemkata na panga kwa sababu alifanikiwa kututoroka.
“Lakini niwahakikishie kuwa tutamkamata kwa sababu kama walivamiwa hawakupaswa kumkata mtu na panga, pia nimewaita viongozi wa pande zote mbili nimezungumza nao nimewaeleza kama wana ugomvi wahakikishe unaishia ndani usitoke nje na kusababisha uvunjifu wa amani,” alisema Kamishna Sirro.
Akitangaza kupiga marufuku zoezi la usafi kama lilivyoombwa na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea, Kamishna Sirro alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na sababu mbalimbali za kiusalama na mgogoro wa muda mrefu unaoendelea katika chama hicho.
Sirro aliwataka wanachama wa CUF kufanya usafi katika maeneo wanayoishi au ofisi wanayofanyia kazi na si kukusanyika katika eneo hilo.
Alisema kitendo cha wanachama hao kukusanyika kutoka maeneo mbalimbali kwa kigezo cha kufanya usafi kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuwataka wananchi kufuata maelekezo yaliyotolewa na Jeshi hilo.
KIKAO CHA MSAJILI
Kikao cha Msajili wa Vyama vya Siasa kilichoitishwa jana kwa lengo la kutibu yanayojitokeza ndani ya chama hicho, hakikuweza kuhudhuriwa na Maalim Seif, badala yake walioshiriki walikuwa ni Profesa Lipumba na Naibu Katibu Mkuu wake Bara, Magdalena Sakaya.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza, alisema lengo la kuwaita viongozi hao ni kuwataka wajiepushe na vurugu zinazohatarisha maisha zinazojitokeza ndani ya chama hicho.
Alisema migogoro inayojitokeza kwa sasa inaweza kuwaathiri wanachama na wananchi kwa ujumla, jambo ambalo linapaswa kukemewa kwa sababu likiachwa linaweza kuathiri wengine.
Alisema haoni sababu ya kuibuka kwa vurugu ndani ya chama hicho, kwa sababu suala la mgogoro wa uongozi lipo mahakamani.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kama wanachama wana malalamiko au shaka juu ya uongozi wao au wanachama, suala hilo linapaswa kupelekwa kwenye mamlaka husika ili liweze kutatuliwa au kufanyiwa kazi.
Katika hilo, alisema kila upande unapaswa kutii sheria na si kuchukua sheria mkononi.
"Kwa bahati mbaya Katibu Mkuu wa CUF hajafika kwenye hiki kikao, licha ya kumwandikia barua ya wito Aprili 24, mwaka huu pamoja na kuwasiliana nao mara kwa mara juu ya wito wetu, lakini ameshindwa kutokea kwenye hiki kikao, ila tunaamini taarifa ya mazungumzo yetu itamfikia pamoja na kumwandikia barua ya kumwelezea," alisema.
Alisisitiza kuwa, vyama vya siasa havina jeshi la kujilinda zaidi ya vyombo vya ulinzi na usalama vinavyosimamiwa na Serikali.
Kutokana na hilo, alisema wafuasi wa CUF wanapaswa kujipima wenyewe na kuangalia kama wanachokifanya kipo kisheria.
Akizungumza kuhusu tangazo la wanachama na wabunge wanaomuunga mkono Maalim Seif kwenda kufanya usafi kesho ofisi za chama hicho Buguruni, Nyahoza alisema, kama wanaamini hakutakuwa na vurugu zozote wanaweza kwenda, lakini kama wamepanga kwenda kufanyiana vurugu wanapaswa kujiepusha kwa sababu watakaoathirika ni wananchi na si viongozi.
MAALIM SEIF ADAI HAKUITWA
Wakati Ofisi ya Msajili ikisisitiza kumtumia mwaliko Maalim Seif, hata hivyo, taarifa iliyotolewa baadaye jana jioni na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Nassor Mazrui, ilieleza kuwa kiongozi huyo hajapokea barua yoyote ya wito kuhusu kikao hicho.
Mazrui, hata hivyo, alikumbusha kuwa Jaji Francis Mutungi ni miongoni mwa washtakiwa katika kesi ya wizi wa Sh milioni 369 za ruzuku ya CUF na mashauri mengine yaliyopo mahakamani na kuhoji kukutana kwao bila uwepo wao.
"Ofisi ya Katibu Mkuu, Mtendani, Zanzibar na wala Katibu Mkuu Maalim Seif hajapokea taarifa yoyote ya barua, simu au barua pepe na au kwa njia nyingine yoyote ile wito wa kuhudhuria kikao chochote kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama ya Siasa Nchini," alisema Mazrui.
Aliongeza CUF wanaamini kikao hicho pengine ni mwendelezo wa vikao vyao vya kujadiliana namna ya kujinasua na kesi zinazowakabili mahakamani na kupanga njama za kuhujumu CUF na viongozi wake ambavyo mara zote wao wamekuwa wakijulishwa na intelijensia yao.
Akizungumzia hatua ya Jeshi la Polisi kupiga marufuku zoezi la usafi, Mazrui alionekana kushangazwa na hatua hiyo, akisema ofisi hiyo ni mali ya CUF, hivyo kama chombo hicho cha ulinzi kilivyotumika kumsindikiza Lipumba na genge lake kufanya uvamizi katika Ofisi hiyo Septemba 24, 2016, lilipaswa kufanya hivyo kwa wabunge na wanachama hao.
Alilitaka Jeshi la Polisi kuacha tabia ya kuzuia kufanyika kwa shughuli zote za chama kwa kusingizia uvunjifu wa amani, huku wakimlinda Lipumba na wenzake.
Zaidi alisema wanaamini kuwa, wahusika wa tukio la uhalifu la Mabibo watachukuliwa hatua za kisheria.