Na TIGANYA VINCENT,
MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amesimamisha kwa muda uchimbaji wa dhahabu katika machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge kuepusha maafa zaidi.
Hatua hiyo inatokana na maafa yaliyokea hivi karibuni ambako wachimbaji wadogo sita walifariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi na mmoja kwa kukosa hewa, wakati wakichimba dhahabu katika eneo hilo.
Uamuzi huo ulitolewa jana wilayani Sikonge na RC Mwanri kwa kushirikiana na Kamati na Ulinzi na Usalama mkoani humo baada ya kutembelea machimbo yaliyosababisha maafa hayo kujionea na kuwapa pole wafiwa.
Alisema yeye na kamati yake waliona ni vema wasimamishe kwa muda ili taratibu zote za kuhakikisha usalama na zile Baraza la Taifa la Mazingira za mpango wa ulinzi wa mazingira zinafuatwa kabla ya kendelea na shughuli za uchimbaji.
Mwamri alisema lengo ni kutaka wachimbaji hao waendelee kuchimba katika hali ya usalama bila kuhatarisha maisha yao na nguvu kazi ya taifa.
Aliwaagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati na Magharibi, Salim Salim na Ofisa Madini Mkazi wa Tabora, Laurent Mayala kuhakisha umbali kutoka shimo moja la uchimbaji hadi jingine unazingatia matakwa ya sheria na kanuni kuliko ilivyo sasa ambako kutoka shimo hadi shimo ni mita tatu hali ambayo ni hatari.
Rc alisema ni vema ofisi hizo zikahakikisha zinawapanga wachimbaji wadogo hao kulingana na matakwa ya sheria na siyo kuwaacha ovyo ovyo.
“Mimi siko tayari kuona watu wengine zaidi wanakufa kwa sababu ya uchimbaji usiozingatia matakwa ya sheria na ambao hauna baraka za NEMC.
“Hivyo kaeni chini na wamiliki wa mgodi muwapange vizuri kwa kuzingatia sheria na bila upendeleo.
“Serikali ya Awamu ya Tano ilishaahidi kuwa itawashika mkono wachimbaji wadogo lakini ni vema tukahakikisha mpango wa ulinzi wa mazingira umezingatiwa.
“Pia wawepo wakaguzi watakaohakikisha taratibu za umbali kutoka shimo hadi shimo umezingatiwa kulinda usalama wao kwanza,” alisema.
Aliwaagiza maofisa madini kuharakisha kufuatilia kibali cha NEMC na kuandaa mpango kazi wa uchimbaji mzuri na salama vijana wanaojihusisha na uchimbaji wa madini Kitunda wasikae muda mrefu bila kuendelea na kazi yao ya uchimbaji madini.
Eneo la machimbo ya Kitunda lina wachimbaji zaidi ya 10,000.