30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE WAHOFIA NJAA

Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson

 

 

ELIZABETH HOMBO Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

BAADHI ya wabunge wametaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili wajadili kwa kina suala la tishio la njaa na kuadimika kwa sukari kwa dharura.

Hali hiyo ilijitokeza jana bungeni mjini hapa, baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu na wabunge hao kuomba mwongozo kwa Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Mbunge wa kwanza kusimamia kuomba mwongozo kwa Naibu Spika, alikuwa Mbunge wa Moshi Mjini, Jafary Michael (Chadema), ambaye alitumia kanuni ya 67 (1-7) na 47 (1).

Aliomba mwongozo huo kwa kumtaka Naibu Spika aahirishe shughuli za Bunge ili kuweza kujadili upungufu wa sukari nchini kama jambo la dharura.

“Mheshimiwa Naibu Spika, nasimama kwa kanuni ya 67 (1-7) sambamba na kanuni ya 47 (1), naomba nisisome kwa ajili ya kuokoa muda.

“Nikuombe ridhaa ya kiti chako kama kuna uwezekano Bunge lijadili kuhusu jambo la dharura. Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na upungufu mkubwa tena wa sukari katika nchi yetu.

“Kuna baadhi ya maeneo hivi sasa bei ya sukari ni Sh 2,900 mpaka 3,000 kwa kilo na huu upungufu unakoelekea utaendelea mpaka kipindi hiki cha mvua kiishe ili viwanda vyetu vifanye kazi, naona kama ni jambo la dharura kwa sababu hali ya wananchi inazidi kuwa mbaya, ukizingatia pia kuna shida ya hali ya chakula nchini na mfumuko wa bei.

“Naomba mwongozo wako katika hili ili ikikupendeza Bunge liahirishwe na lijadili jambo hili kama la dharura,” alisema Michael.

Kutokana na mwongozo huo, Dk. Tulia, alisema taarifa hizo za kupanda kwa sukari ndiyo anazisikia kutoka kwa mbunge huyo, hivyo haitajadiliwa kwa sababu hakuna taarifa rasmi.

“Kuhusu mwongozo wa Japhary; taarifa za kupanda kwa sukari kiti ndio kinasikia kwa mheshimiwa Japhary, kwa sababu hizo hakuna namna ya Bunge kuanza kujadili jambo hilo sasa, maana hizo taarifa hatuna. Hata tukijadili, tunajadili kwa taarifa ipi? Hivyo hatutaweza kujadili,” alisema Dk. Tulia.

Naye Mbunge wa Serengeti, Marwa Chacha (Chadema),  aliomba mwongozo kwa kutumia kanuni ya 69 (1), akiomba kiti kiahirishe shughuli za Bunge kujadili hali ya njaa nchini kama jambo la dharura.

“Mheshimiwa Naibu Spika, katika wilaya yangu ya Serengeti hali ya njaa inatisha, hivi sasa debe la mahindi ni Sh 25,000 hadi 30,000. Tangu nizaliwe haijawahi kutokea na hii imesababishwa na tembo ambaye anakula mazao pale yanapofikia kuvunwa.

 “Nimelipeleka jambo hili kwenye kamati na nimemwambia waziri mwenye dhamana. Juzi wamefariki watu watatu, mama na watoto wake wawili kwa sababu walikosa chakula wakala mihogo michanga,” alisema Chacha.

Alisema wananchi wake hawataki mahindi ya bure bali wanahitaji yale ya Serikali ambayo yatauzwa kwa bei rahisi.

“Tumeenda kwenye ghala la Serikali tukakuta mahindi yanaoza, sasa tunahitaji mahindi haya yaende Serengeti ili yaende kupunguza mfumuko wa bei na lini mahindi haya yatatumika kama si wakati huu wa njaa? Ninaomba kwa mujibu wa kanuni hii, kuahirisha Bunge ili tujadili suala la njaa katika nchi hii kwa sababu ni kubwa,” alisema.

Akijibu mwongozo huo, Dk. Tulia alisema kwa kuwa Waziri wa Kilimo yupo bungeni na aliwahi kuhakikishia mhimili huo kuwa chakula kipo cha kutosha, alifuatilie jambo hilo.

“Waziri wa Kilimo yupo hapa na huko nyuma alihakikishia Bunge kuwa chakula cha kutosha kipo… Waziri wa Kilimo umemsikia Mbunge wa Serengeti na kuna hao watu waliofariki kwa kula mihogo. Kwa kuwa uko hapa, tafadhali hili jambo lifuatiliwe na vyombo vinavyohusika,” alisema Dk. Tulia.

WASHINDIA UJI WA UBUYU

Katika hatua nyingine, wakazi wa vijiji vya Sepisa na Hombolo katika Kata ya Hombolo mkoani Dodoma, wamekuwa wakishindia uji wa ubuyu kutokana na ukosefu wa chakula, huku bei ya unga wa sembe ikiwa juu tofauti na siku zote.

Kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali iwapatie msaada wa chakula kutokana na njaa inayoikabili kata hiyo.

Pia wamesema ndege waharibifu wa mazao, kwelea kwelea,  wamevamia mtama katika baadhi ya vijiji vya kata hiyo na kusababisha hofu kubwa kwa wakulima wanaotegemea zao hilo kwa chakula.

Wakizungumza na waandishi wa habari juzi, wakazi hao walisema upatikanaji wa chakula katika kata hiyo si mzuri kwa vile kilo moja ya unga hivi sasa inauzwa kwa Sh 2,500 bei ambayo ni kubwa ikilinganishwa na uwezo wa wananchi wengi ambao ni masikini.

Nizar Wanjali alisema kutokana na tatizo la njaa familia nyingine zimekuwa zikishindia uji wa ubuyu baada ya bei ya mahindi kuwa juu.

“Hali ni mbaya, familia nyingine zinashindia uji uliotengenezwa kwa unga wa ubuyu,” alisema.

Alisema biashara iliyopo sasa ni ya ubuyu, ambao debe moja limekuwa likiuzwa kwa Sh 1,000.

“Watu wanauza ubuyu wakipata fedha ndiyo waweze kununua unga,” alisema.

Naye Raphael Masima alisema debe moja la mahindi limekuwa likiuzwa kwa Sh 25,000 hali ambayo inafanya wananchi wengi washindwe kumudu na kujikuta wakila mlo mmoja kwa siku.

  Neema Matonya alisema uhaba huo wa chakula umesababisha wafugaji wa nguruwe kuacha kufuga kutokana na kupanda bei ya pumba ambako debe moja kwa sasa linauzwa kwa Sh. 4,000.

Alisema hali hiyo imesababisha watu kuacha kufuga na hata nguruwe waliopo wamedhoofu kwa uhaba wa chakula.

Diwani wa Viti Maalum, Editha Luhamo (CCM) amekiri kuwapo tatizo la njaa huku akidai kuwa mtama ambao ulianza kuchanua umeanza kuliwa na kwelea kwelea.

“Sasa ninafanya juhudi za kuwasiliana na ofisi ya kilimo waweze kutusaidia katika tatizo hili,” alisema.

Pia alisema hali ya mazao katika kata hiyo ni mbaya kutokana na mazao kuanza kukauka kwa jua kali.

RIPOTI YA BoT

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi ya Februari mwaka huu, bei za jumla za mazao yote makuu ya chakula, isipokuwa mchele, ziliongezeka kipindi cha Januari 2017 kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana.

Aidha kati ya Desemba 2016 na Januari 2017, bei za mazao yote ya chakula ziliongezeka isipokuwa mtama.

Hata hivyo taarifa zinaeleza kwamba bei ya debe moja la mahindi imepanda mara dufu kutoka Sh 15,000 hadi 20,000 ya awali na kufikia Sh 26,000 hadi 30,000.

Kupanda huko kwa mahindi kwa zaidi ya asimilia 40, kumesababisha mateso kwa wananchi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Kilimo, Chakula, Mifugo na Uvuvi, ya Januari mwaka huu, gunia moja la mahindi limepanda hadi Sh 93,356.3  kutoka Sh 67,044.9 hadi 85,159.8 kwa Januari-Desemba 2016.

AKIBA YA CHAKULA

Ripoti hiyo ya BoT inaonyesha kuwa akiba ya chakula iliyopo katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ilikuwa tani 86,834 kufikia mwishoni mwa Januari 2017.  Kiwango hicho kilishuka kidogo ya kile cha tani 89,692 kilichokuwapo mwezi uliotangulia.

Anguko hilo la akiba ya chakula lilitokana na kuuzwa kwa tani 2,858 za mahindi. Tani 2,393.9 ziliuzwa kwa wafanyabiashara binafsi; tani 433.0 kwa Idara ya Magereza na tani 31.1 kwa Kitengo cha Uratibu wa Majanga kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu.

MFUMUKO WA BEI

Kwa mujibu wa ripoti ya BoT, mfumuko wa bei wa jumla wa miezi 12 ulibakia wastani wa lengo lililowekwa wa asilimia 5.0.

Mfumuko huo wa bei wa jumla ulikuwa asilimia 5.2 kulinganisha na asilimia 5.0 ya mwezi uliotangulia. Kupanda kwa mfumuko wa bei wa jumla kulichochewa na kupanda kwa bei za vyakula na vinywaji visivyo na kilevi, hasa nafaka za mahindi, unga, mchele, ndizi, mtama na maharage.

Mfumuko wa bei miongoni mwa vyakula na vinywaji visivyo na kilevi ulikuwa sababu kuu ya mfumuko wa bei wa jumla.

Kwa msingi wa mwezi kwa mwezi, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 0.8 kulinganisha na asilima 0.7 Januari 2016.

 Mfumuko wa bei wa mwaka kwa vyakula na vinywaji visivyo na kilevi ulipanda kufikia asilimia 7.6 Januari 2017 kulinganisha na asilimia 7.0 mwezi uliotangulia. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles