26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

MASHIRIKA MANNE YAFUJA BIL. 249/-

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mussa Assad

 

 

Na FREDY AZZAH-DODOMA

WAKATI ukata ukisababisha bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2016/17 kutotekelezwa kwa kiasi kikubwa, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonyesha mashirika manne ya umma yamefuja takribani Sh bilioni 249.95.

Ripoti hiyo ya mwaka 2015/16 iliyowasilishwa bungeni juma lililopita, inaainisha taasisi hizo kuwa ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

MUHIMBILI

Katika ripoti hiyo, mapitio ya ankara kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD), yameonyesha kuna ankara 48 za tangu mwaka 2010 zenye thamani ya Sh bilioni 2.29.

“Hospitali ya Muhimbili walilipa kiasi chote cha fedha. Hata hivyo, imebainika bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 1.84 ndizo zimefika na kupokewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili mpaka kufikia Juni 2016 na kuacha bidhaa zenye thamani ya Sh milioni 450.57, zikiwa hazijafikishwa Muhimbili.

“Kutokufika kwa muda kwa vifaa vya matibabu, kunasababisha usumbufu kwa hospitali katika utoaji wa huduma ya tiba. Menejimenti inashauriwa kuchunguza suala husika na kufanya usuluhishi wa taarifa na MSD na kufanya ufuatiliaji wa bidhaa ambazo hazijaletwa,” inasema taarifa hiyo.

TANESCO

CAG amesema kifungu kidogo Na. 1 cha kifungu Na. 83 cha sheria ya kodi ya mapato ya 2008 kinahitaji mlipaji kutoza kodi ya zuio inayotokana na ada zote za huduma na malipo ya mkataba.

Pamoja na sheria hiyo, CAG alibaini Tanesco haikuzuia kodi ya zuio yenye thamani ya Sh bilioni 1.36.

“Kwa kutotoza kodi ya zuio, si tu kunaipotezea Serikali mapato, bali kunaweza kusababisha adhabu na riba ambayo inaweza kwa kiasi kikubwa kuongeza gharama zisizo za lazima kwa kampuni.

“Menejimenti inakumbushwa kuzuia kodi ya zuio inayotokana na ada za huduma na malipo ya mkataba,” inaeleza ripoti hiyo.

NHIF

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, NHIF ilitoa mkopo wa Sh bilioni 44.29 kujenga kituo cha afya cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

“Hata hivyo, imebainika kuwa mkopo huo haukuwa na mkataba wala uthibitisho wa udhamini kutoka serikalini.

“Kuwapo kwa mkataba kungesaidia kuweka wazi haki na wajibu wa kila upande katika mkopo huu na utaratibu wa riba na urejeshaji wa mkopo.

 “Kukosekana kwa mkataba na uthibitisho wa udhamini wa Serikali, kunaweza kuusababishia mfuko kupoteza fedha za wanachama endapo mkopaji atashindwa kuwa mwaminifu, na itakuwa vigumu kupata haki mahakamani,” inaeleza ripoti hiyo.

Kutokana na hali hiyo, menejimenti ya NHIF imeshauriwa kuhakikisha mkataba wa mkopo unaingiwa kati yake na mkopaji. Pia uthibitisho wa udhamini unapatikana kutoka serikalini.

“Pia NHIF inashauriwa kuhakikisha inaingia katika mkataba kabla ya kutoa mkopo wowote mbeleni,” inaeleza ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, NHIF ilisaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ikiitaka Serikali kutoa fedha kuendesha malengo ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), ambayo ilihusisha gharama za kawaida za uendeshaji mfuko.

“Mpaka kufikia Juni30, 2015, NHIF ilipaswa kuwa imerejeshewa na Serikali Sh bilioni 1.20 kutokana na gharama ilizotumia kwenye miradi ya CHF kama ilivyoainishwa kwenye hati ya makubaliano.

“Hata hivyo, gharama hizo hazikuweza kurejeshwa na Serikali. Kushindwa kwa Serikali kuilipa NHIF kumeuongezea mfuko mzigo mkubwa wa kifedha, hivyo kusababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na kushindwa kupanua wigo wa shughuli zake.

“Menejimenti ya NHIF inashauriwa kuchukua hatua za ziada ili kuhakikisha Serikali inarejesha fedha husika,” inasema ripoti hiyo ya CAG.

 

BANDARI

Kwa upande wa TPA, ripoti hiyo inaonyesha hati ya makubaliano (MOU) inaitaka TRA baada ya kukusanya mapato ya kuhifadhi mizigo bandarini kuyawasilisha kwenye akaunti ya benki ya Mamlaka ya Bandari ndani ya siku 14.

“Hata hivyo, nilibaini kuwa kiasi cha Sh bilioni 98.7 kilichokusanywa na TRA kati ya Agosti hadi Desemba mwaka 2016 hakikuwasilishwa kwenye akaunti ya TPA kama makubaliano yanavyotaka,” inasema ripoti hiyo.

Inasema pia mapitio ya madeni ya watoa huduma ya kibiashara na mengineyo yamebaini kiasi kikubwa cha fedha kuliko kile ambacho kimeakisiwa kwenye vitabu vya hesabu (General Ledger).

“Kiasi kilichothibitishwa na watoa huduma ni Sh bilioni 105.50 wakati kiasi cha fedha kilichoakisiwa kwenye vitabu vikuu vya hesabu ni Sh milioni 687.23. Hii inafanya tofauti ya Sh bilioni 104.81 ikiwa ni kiasi chini ya kiasi halisi ambacho kimeripotiwa na TPA.

“Pamoja na hayo, menejimenti ya TPA haikuwa ikifanya mara kwa mara usuluhishi (reconciliation) kwa taarifa za watoa huduma. Hali hii imesababisha tofauti kubwa kati ya rekodi za watoa huduma na rekodi za TPA. Ni maoni yangu kuwa bakaa ya madeni ya kibiashara na madeni mengineyo imekosewa kwa kiasi kikubwa, hivyo haionyeshi thamani halisi ya deni.

“Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari inashauriwa kufanya usuluhishi wa mara kwa mara wa madeni yaliyoakisiwa katika vitabu dhidi ya rekodi za watoa huduma ili kuhakikisha usahihi,” inasema ripoti hiyo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,922FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles