Na BALINAGWE MWAMBUNGU,
MHARIRI wa habari, Reggie Mhango, wakati huo nikiwa Daily News, aliniambia niende nyumbani nikabadilishe nguo kwa kuwa jioni ile nilitakiwa kufuatana na Mhariri Mtendaji, Ulli Mwambulukutu, kwenda Ikulu kwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine.
Akaniambia kuwa, waziri mkuu alikuwa na sherehe ya kuukaribisha mwaka mpya 1984. Ilikuwa Februari.
Edward Moringe Sokoine kwangu atabaki kuwa kiongozi wa mfano mwenye uzalendo, upeo, msikivu, mpole, mwenye kupenda watu, mwaminifu, jasiri na asiyependa makuu.
Baada ya sherehe, Waziri Mkuu Sokoine alituaga. Nilijisikia vizuri sana niliposhikana naye mkono, kwani lilikuwa jambo la nadra maishani kupata bahati kama hiyo. Sokoine alimshika mkono kila mtu aliyekuwapo mahali pale.
Mawaziri wakuu waliofuata, hawakufuata nyayo za Sokoine. Tangu hapo, hakuna waziri mkuu aliyewahi kuwafanyia tafrija wanahabari au kuwaalika kwenye sherehe kama hiyo.
Hata marais waliofuata baada ya Mwalimu Julius Nyerere kung’atuka, huwa wanawaita wanahabari wanapoingia Ikulu, lakini wanapomaliza vipindi vyao, huondoka kimya kimya. Mwalimu Nyerere alituita Ikulu, tukala, tukanywa na kupiga naye picha ya kumbukumbu kwenye ngazi za Ikulu upande wa Mashariki.
Sherehe ile ya kuagana na Sokoine naichukulia kama ilikuwa ishara ya kutuaga. Miezi miwili baadaye, Aprili 12, 1984, Sokoine alifariki dunia katika ajali ya gari eneo la Dumila, Barabara ya Dodoma-Morogoro.
Wasomi na wanafilosofia wanasema kuwapo kwetu duniani hakutakuwa na maana kama hutataacha kumbukumbu yoyote ya kudhirisha uwepo wetu. Labda ndiyo filosofi iliyomwongoza Sokoine, kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yake na kuwatumikia Watanzania kwa moyo mkunjufu na kuwajali na kutaka wasonge mbele ili kutafuta maendeleo ya pamoja. Hii pekee ndiyo inatufanya tumkumbuke hadi leo. Na sisi ambao tulibahatika kumfahamu Sokoine kwa karibu, tunawajibika kukiambia kizazi cha sasa, Sokoine alizaliwa na kipaji cha uongozi.
Uongozi ni kipaji, unapoingia kusomea uongozi, unaongezewa mbinu tu za uongozi. Kule Unyakyusani, baba ndiye anamwandaa mtoto wake wa kiume kumrithi. Machifu hushauriwa na wazee ni mtoto gani wanataka awatawale baada ya chifu kufariki dunia na mtoto huyo huwa anaandaliwa.
Uongozi katika nchi yetu ni wa ‘nataka’ hata kama mtu anajijua kwamba hana uwezo wa kuongoza. Uongozi umewekewa sifa, na ukiwa na sifa zinazotakiwa, unaweza ukapata uongozi, lakini huna kipaji cha uongozi ndiyo maana tunatapatapa na mtu akiishapata uongozi kwa vile hakuzaliwa kiongozi, unatumia nguvu nyingi ili ukubalike na unaowaongoza kama hawakukubali, unawatishia kwa kutumia nguvu za madaraka uliyonayo.
Waliokuwa rika moja na Sokoine wanasimulia kwamba alichaguliwa kuongoza wenzake wa Kimaasai akiwa mdogo, ingawaje kulikuwa na vijana waliomzidi umri.
Sokoine hakuwa msomi mwenye madigrii, lakini alikuwa kiongozi mwenye busara, mpole na thabiti hakuwa mbabaishaji, au mwenye kigeugeu. Aliwaheshimu watu wote, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo. Sokoine alikuwa hapendi ‘longolongo’ alikuwa mkweli. Hakupenda hotuba ndefu za kuchosha wasikilizaji. Alikuwa mtu wa maneno machache ya kuelekeza nini kifanyike. Alikuwa mwenye kumbukumbu ndiyo maana maofisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu, walimbatiza jina la Bwana Siku Saba. Mtu akipewa kazi ya kumtafutia majibu kuhusu suala fulani, alitaka majibu yapatikane ndani ya siku saba. Siku ya saba ikifika, alikuwa anafuata majibu kwa ofisa husika, badala ya kumwita ofisini kwake. Sokoine hakuwa mwamrishaji. Watumishi wa Serikali walimheshimu, pia walimwogopa. Alikuwa mkimya.
Sokoine hakuwa mfujamali za umma, alitumia Land Rover katika safari zake mikoani. Aliurudisha utaratibu wa magari ya Serikali kukaa kwenye ‘pool’ yakiwa ofisini, ili ofisa yeyote aweze kutumia wakati wa kazi. Aliweka utaratibu wa kuwakopesha magari wakurugenzi na makatibu wakuu, ili kupunguza matumizi ya Serikali kwa upande wa usafiri. Mkurugenzi au katibu mkuu alikuwa na gari lake binafsi kumtoa nyumbani na kurudi nyumbani. Akiwa ofisini alitumia gari la ofisi.
Sokoine alianzisha utaratibu wa kununua gari aina moja ili kuondoa uagizaji wa vipuli vya aina tofauti. Magari yote ya Serikali yalikuwa hayatengenezwi kwenye gereji binafsi.
Sokoine alikuwa kiongozi mwenye maono alitaka Tanzania ijielekeze kwenye uzalishaji wa chakula. Kila halmashauri na kila wilaya, ilitakiwa kuwa na kituo cha trekta ili wakulima waweze kuyakodi wakati wa msimu wa kilimo. Nchi kama haiwezi kujilisha, inakuwa inauweka poni uhuru wake. Watu wenye njaa hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi, huwa legelege, ni rahisi kushambuliwa na magonjwa.
Njaa husababisha rushwa, uchoyo, hupoteza uaminifu na uzalendo. Sokoine alijielekeza kwenye utekelezaji wa sera ya Ujamaa na Kujitegemea kama ilivyokuwa imeainishwa katika Azimio la Arusha. Sokoine, kama Rais wake, Mwalimu Julius Nyerere, aliishi maisha ya kujihini. Sikuwahi kumwona Sokoine anakwenda vijijini akiwa amevaa suti na tai kama wafanyavyo viongozi wa sasa. Labda kwa kuwa alikuwa anatumia Land Rover ambazo hazikuwa na kiyoyozi!
Shirika la Usafiri Dar (UDA), liliposhindwa kazi ya kusafirisha abiria jijini, Sokoine alishauriana na viongozi na ikakubalika kuwa watu binafsi waruhusiwe kusafirisha abiria. Uamuzi ule wa mwaka 1984, ndio uliozaa daladala zilizoenea mijini nchi nzima. Kwa nini mabasi hayo yanaitwa dala dala ni kwa sababu wakati ule (gwala) shilingi tano ya Kitanzania, zilikuwa sawa na dola moja ya Marekani.
Edward Sokoine alikuwa mchapakazi. Msaidizi wake mahususi, Horace Kolimba (marehemu), aliwahi kuniambia kuwa alikuwa mtu wa mwisho kulala. Waziri mkuu alikuwa anamruhusu kwenda nyumbani baada ya saa saba. Alisema Sokoine alikuwa analala baada ya kusikiliza taarifa kutoka kwa wakuu wa mikoa yote Tanzania Bara.
Kolimba kama alivyokuwa waziri mkuu, pia alikuwa mtu mnyoofu, mchapakazi na hakuwa mtu wa kupindisha pindisha maneno.
Kifo cha Edward Sokoine kimeacha swali ambalo halijajibika. Kuna mambo ambayo yanatendeka nyuma ya pazia hatuyaoni. Lakini huenda siku moja swali hili litajibika kwa sababu Mungu atatuangazia nuru yake na itajulikana kwanini Sokoine alikufa kwa ajali.
Sokoine atakumbukwa milele kwa sababu jina lake limewekwa kwenye kumbukumbu ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, kilichopo mkoani Morogoro.