28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

PASAKA ITUONDOLEE HOFU YA UTEKAJI NYARA

NA EVANS MAGEGE,

WAUMINI wa madhehebu ya Kikristo duniani kote, leo wanaadhimisha Sikukuu ya Pasaka ambayo ni ukumbusho wa kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo.

Kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo kunatimiza azimio takatifu la mapatano mapya ya mwanadamu na Mungu kupitia msamaha wa dhambi.

Historia inaonyesha kuwa, kabla ya kuja kwa Yesu Kristo duniani zaidi ya miaka 2000 iliyopita, Pasaka ilikuwa inaadhimishwa kama kumbukumbu ya Wanaisraeli walipoachiwa na Pharao wa Misri na kuruhusiwa kurudi kwenye nchi yao ya ahadi Kanani.

Pasaka ni neno linalotokana na maneno ya Kiingereza Pass Over. Wakati ule Wayahudi (wana wa Israeli) walipokuwa utumwani, Mungu alisikia kilio chao, akamtuma Mussa kuwaongoza Waisraeli kutoka Misri. Lakini Pharao (Mfalme) akawa anawakatalia.

Mungu alimpiga Pharao kwa mapigo 10. Pigo la mwisho, Mungu akamwambia Mussa, kila nyumba ya Myahudi ichinje mnyama asiye na mawaa na damu yake apake mlangoni ili malaika watakapokuja waipite (pass over) nyumba hiyo. Usiku malaika walipita na kuua kila kizaliwa cha kwanzo pamoja na mtoto wa kwanza wa Pharao. Pigo hilo halikuwagusa Wayahudi. Ndipo Pharao akamwaru Mussa na watu wake waondoke Misri.

Pasaka ilikumbukwa na Wayahudi kama siku ya ukombozi. Wakristo huadhimisha Pasaka kama siku ya ukombozi. Kama Mussa alivyowakomboa Wayahudi kutoka utumwani, Pasaka ni siku ya ukombozi kutoka dhambini Misri kwa kusulubiwa, kufa, kuzikwa na kufufuka kwa Yesu Kristo.

Pasaka ni siku ya maadhimisho ya kukumbuka siku ya ukombozi na Wakristo hufanya ibada ya toba kutubu na kujiweka safi kwa ajili ya kuingia kwenye mapatano mapya na Mwenyezi Mungu.

Hisia za uchungu au mateso makali kwa mfano wa jinsi wana wa Israeli (Wayahudi) walivyoteswa utumwani au jinsi Yesu alivyoteswa msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, ndiyo zinavuta picha halisi ya kwamba maadhimisho ya Pasaka ni sawa na kuvuka daraja la kutoka kwenye maovu na kuingia kwenye mambo mema yampendezayo Mungu.

Mapito ya kuelekea Pasaka mwaka huu, yalizongwa kwa uchungu wa fikra na hisia ya hofu kutokana na vitendo vya utekaji  vitendo ambavyo vimewajengea hofu Watanzania.

Hali hiyo imechochewa na tukio la hivi karibuni la kutekwa nyara kwa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Ibrahim Mussa (Roma Mkatoliki) na wenzake wawili.

Vijana hao walitekwa nyara na kupelekwa kusikojulikana kwa siku mbili, kisha wakatelekezwa usiku wa manane katika eneo la wazi.

Kwa mujibu wa maelezo ya Roma mwenyewe, ambaye alitoa sehemu ya simulizi ya tukio hilo, anasema baada ya kutekwa walikumbana na matezo makali kabla ya kutelekezwa katika eneo la Ununio, jijini Dar es Salaam.

Tukio la Roma na wenzake kutekwa limeibua hofu kubwa ndani ya jamii ya Watanzania, hofu hiyo imekuwa na nguvu kiasi cha kuzua mjadala mzito kwenye Bunge, ambapo baadhi ya wabunge wameeleza bayana kwamba wametishwa na  mwingine akitanabahisha kuwapo mkakati wa kuuawa yeye na wenzake 10.

Mapema wiki iliyopita Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alieleza kuwa  amepata taarifa zinazodai yeye na wabunge wenzake 10 wako katika hatari ya kuuawa na genge la watu wanaojihusisha na utekaji nyara.

Maelezo hayo ya Bashe yaliongeza hali ya hofu miongoni mwa wabunge na mjadala ukahamia kwenye tukio la madai ya kutekwa nyara kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ben Saanane, ambaye bado hajulikani alipo tangu Novemba, mwaka jana.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ameelezea hofu ya utekaji nyara kwa kupendekeza kuundwa kwa Kamati Teule ya kuchunguza vitendo hivyo.

 “Mtanzania aliyepotea Ben Saanane ni suala ambalo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa juu, si suala linalopaswa kuchukuliwa kisiasa.

“Si suala linalopaswa wabunge wabebe uthibitisho walete mezani kwa sababu taarifa zilizopo sasa na ziko Jeshi la Polisi zinaonesha kwamba Novemba 15 Ben Saanane, kwenye mawasiliano yake ya simu kuanzia asubuhi alikuwa maeneo ya Tabata.

“Akaenda maeneo ya Mikocheni, akatumia muda mwingi sana maeneo ya Mwenge, akapelekwa ama akaenda Mburahati saa nne usiku ya mwezi Novemba, simu yake ikapoteza mawasiliano tangu hapo, hajawahi kuwa traced (kuonekana) tena.

“Na haya maelezo yako polisi na ukifuatilia Jeshi la Polisi wanakwambia tumefikia mwisho. Lakini mwelekeo wetu unaonyesha kuwa waliomchukua Ben Saanane ni (anataja moja ya taasisi nyeti ya mambo ya usalama), na mwenyekiti wewe ume-save (umefanya kazi) katika Kamati ya Usalama na Mambo ya Nje, unafahamu Sheria ya Usalama wa Taifa kifungu namba tano, kifungu kidogo cha pili, kinapiga marufuku Usalama wa Taifa ku-enforce laws (kusimamia sheria).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema kuwa Serikali inalifanyia kazi suala hilo na kwamba itatoa taarifa baada ya kufanyika uchunguzi juu ya matukio hayo.

 “Wabunge wamezungumzia suala la usalama. Ninaomba niwahakikishieni kwamba Serikali inalifanyia kazi na baadaye tutatoa taarifa kwenu… tuache vyombo vyetu vifanye kazi ya uchunguzi, kwamba ni nani anayefanya haya na je, matukio haya yanakubalika? Tunajua ni matukio yasiyokubalika,” alisema Majaliwa.

Tukirudi kwenye maandiko ya Biblia takatifu, yanaonyesha kuwa Sikukuu ya Pasaka imekuwa ndani ya utamaduni wa Wayahudi tangu enzi za Nabii Musa, ambapo msingi wake ulitokana na ukombozi wa Mwenyezi Mungu wa kuwatoa wana wa Israeli utumwani nchini Misri.

Kwa mantiki hiyo, Pasaka inayoadhimishwa leo ituweke kwenye mwelekeo mpya wa kuwaondoa Watanzania kwenye uchungu wa mawazo juu ya nini kitatokea kwenye maisha yao baada ya kuwapo matukio haya ya utekaji nyara au kupotea kusikojulikana. 

Ukisoma msingi wa Pasaka katika Agano la Kale (Kutoka 12:1); imeandikwa kwamba, Bwana  akanena na Musa, na Haruni katika nchi ya Misri akawaambia, “Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu na utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu” .

Kimantiki msingi wa matukio ya uonevu, utesaji wa wanadamu ni sehemu ya machukizo mbele za Mungu na kwa sababu hiyo, hata Pharao na ukaidi wake wa kuwatesa wana wa Israeli, Mungu alilazimika kuwakomboa watoto wake kwa kuwatoa utumwani.

Ukombozi wa wana wa Israeli unaakisi kifo cha Yesu Kristo, ambaye alijitolea kufa kwa ajili ya kuondoa ghadhabu ya Mungu dhidi ya maasi ya binamu.

Biblia inasema Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikiwa, ‘Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti’—Wagalatia 3:13.

Na Warumi 3:25 inasema: “Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa”.

Pia ukisoma Yohana 1, 4:10 inasema: “Huu ndio upendo, si kwamba tulimpenda Mungu, bali yeye alitupenda, akamtuma mwanawe, ili yeye awe dhabihu ya

kipatanisho kwa ajili ya dhambi zetu”.

Kwa muktadha wa machungu au hofu  ya utekaji nyara ambayo Watanzania wengi wamekuwa nayo, hasa katika kipindi cha hivi karibuni, leo watakuwa na nafasi kubwa ya kuomba nguvu ya Mungu iyayeyushe matendo ya utekaji na utesi wa watu, hivyo ufufuo wa Yesu ujenge faraja mpya kwa kila Mtanzania kuishi katika imani yenye amani tele na ujenzi wa Taifa.

Tukumbuke kwamba, taji la miiba na misumari iliyopigiliwa mikononi mwa Yesu Kristo ilimchoma mwili wake na alikufa msalabani. Damu ilipakwa kwenye miimo ya milango kwenye hali sawa na ile damu iliyomwagika msalabani.

Hiyo ni ishara ya uchungu sasa na hofu ya utekaji nyara inavyosumbua fikra za wananchi kimantiki, hali hiyo ni dalili ya mateso kwa maana ya kutendewa ukatili.

Kutoka 1:14, Warumi 1:20 na Yeremia 9:15. Pasaka iliambatana na kula "mboga za uchungu".

Mboga hiyo iliwakilisha taswira ya uchungu wa utumwa ambapo  watu walitaabishwa na inachukuliwa pia kuwa ni taswira ya mateso ya Kristo, lakini baada ya kutimia kwa Pasaka maisha yalibalika kutoka kwenye uchungu na kuingia kwenye furaha.

Vivyo hivyo siku ya leo ni siku ambayo inatuweka Watanzania katika furaha ya kuvuka mateso ya fikra juu ya hofu ya utekaji nyara na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu anaweza kutusaidia kuyaishi maisha mapya kutoka huko kwenye lindi la utekaji nyara.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles