Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
CHANGAMOTO zilizopo katika sekta ya afya zimeonekana kuwa fursa kwa baadhi ya watu ambao wamefanikiwa kuendesha maisha yao kutokana na kuanzisha huduma mbalimbali.
Zahanati na vituo vya afya vya umma vilivyopo bado havikidhi mahitaji ndio maana kwingineko hasa katika maeneo ya vijijini wananchi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma.
Ziko jitihada kadhaa zinazofanywa na serikali kukabili upungufu huo kama vile kubuni Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) unaotekelezwa katika awamu mbili za miaka mitano mitano (2007/08 – 2011/12 na 2012/13 – 2017/18).
Mpango huu unalenga kusogeza huduma za afya hususan tiba, kinga, uboreshaji na utengamao karibu na wananchi.
Serikali pia ilianzisha mfumo wa kushirikisha watu binafsi katika kutoa huduma za afya nchini (PPP) ili kutatua changamoto zilizopo katika sekta hiyo.
Watu tofauti, taasisi na madhehebu ya dini yaliitikia wito huo na kuanzisha zahanati, vituo na hospitali lakini wapo wengine ambao wanatumia fursa hiyo vibaya kutaka kuangamiza afya za Watanzania.
Hapa nawazungumzia watoa huduma binafsi ambao wamekuwa wakiendesha shughuli zao bila kufuata taratibu na miongozo ya afya.
Katika Manispaa ya Ilala vituo vya umma vilivyopo ni 27 huku vya binafsi vikiwa zaidi ya 200 ambavyo vimekidhi matakwa ya kisheria, lakini vipo vingine vinavyoendesha shughuli zake isivyo halali.
Hivi karibuni manispaa hiyo ilifanya ukaguzi kubaini vituo vinavyotoa huduma kinyume cha sheria na kuhatarisha maisha ya watu.
Yaliyobainika katika ukaguzi huo yanasikitisha kwani baadhi ya watoa huduma waliokutwa katika zahanati na vituo hawakuwa na taaluma za fani husika, vifaa duni vya tiba, mazingira machafu na wengine kuuza dawa zilizokwisha muda wake.
UKAGUZI ULIVYOFANYIKA
Kaimu Mratibu wa Vituo Binafsi vya Afya wa Manispaa hiyo, Dk. Yusuph Ally anasema walifanya ukaguzi katika Kata za Kiwalani, Kitunda, Kivule, Mzinga na Kipunguni na kubaini vituo vingi havijasajiliwa na vinatoa huduma kinyume cha sheria.
Anasema kutokana na ukaguzi huo walivifungia vituo 21 ambapo kati yake ziko zahanati nne, maabara nane, nyumba za kawaida mbili na maduka saba ya dawa ambayo yalikutwa yakitoa huduma za zahanati.
“Wengi wanatoa huduma kwa kujificha, unakuta kituo hakina jina na wala hakina wataalamu wanaokidhi vigezo. Hali hii ni hatari sana kwa sababu uwezekano wa kupata maambukizi ni mkubwa,” anasema Dk. Ally.
Mbali ya kuvifungia vituo hivyo, pia vifaa tiba na dawa zilizokutwa vilichukuliwa kama ushahidi na wahusika walitozwa faini na wengine walipelekwa mahakamani.
Naye Mratibu wa Huduma za Maabara katika manispaa hiyo, Petrobash Hassan alivitaja vifaa vilivyokamatwa katika vituo hivyo kuwa ni hadubini, vifaa vya kutolea mimba, vifaa vya kupima mapigo ya moyo, wingi wa damu na sukari.
“Vifaa tumevichukua kama ushahidi wa mahakama na dawa tunakwenda kuzihakiki kwa kutumia wafamasia wetu kwa sababu kwenye maduka mengine tumekuta dawa zinazouzwa zimekwisha muda wake.
“Kwingine tumekuta wagonjwa wana vyeti vinavyoonyesha wamepimwa na kugundulika kuwa na maradhi kadhaa lakini cha kushangaza tulipotaka tuonyeshwe chumba cha maabara hakikuwepo,” anasema Hassan.
VIPIMO VYA HIV
Kulingana na mtaalamu huyo, kabla mtu hajapimwa HIV ni lazima kwanza apewa ushauri nasaha kutoka kwa wahudumu wa afya waliopatiwa mafunzo ya ushauri nasaha.
Anasema kutokana na unyeti wa suala hilo ndio maana wamekuwa hawaruhusu maduka ya dawa kuuza vipimo hivyo.
“Lakini cha kushangaza yako maduka ya dawa tulikuta mbali ya kuuza vipimo pia yalikuwa yakipima watu. Hali hii ni hatari kwa sababu mtu anaweza kuchukua uamuzi mgumu kama wa kujiua au kufanya lolote lile lakini kama akiandaliwa kwa kupewa ‘counseling’ atapokea majibu na kukubali hali halisi,” anasema Hassan.
Anasema licha ya kukuta vipimo vikiuzwa katika maduka ya dawa, pia baadhi ya zahanati zilikutwa zikiwa na vipimo vya HIV ambavyo kwa sasa havitumiki hapa nchini.
Naye Mratibu Uhakiki Ubora Huduma za Afya katika manispaa hiyo, Semeni Segela anasema athari za kutibiwa katika vituo ambavyo havijasajiliwa ni kubwa kwani uwezekano wa kupata maambukizi ni mkubwa.
“Hatuwagandamizi walio kwenye sekta binafsi bali tunapambana na wale wanaotoa huduma bila kuwa na sifa za kitabibu, kuna wengine wanazo lakini hawafanyi shughuli zao kihalali,” anasema Segela.
WATOA HUDUMA BINAFSI
Baadhi ya watoa huduma wanakiri kutoa huduma kinyume cha sheria kwa kisingizio cha ugumu wa maisha huku wengine wakisema wanafanya shughuli hizo kwa uzoefu.
“Mimi niliwahi kuwa muhudumu wa maabara Sumbawanga mkoani Rukwa hivyo, nina uzoefu wa shughuli hizi,” anasema ambaye alikutwa akiendesha zahanati bubu katika Kata ya Mzinga.
Ofisa Afya wa Kata ya Mzinga, Hamisa Mtendamema anasema uelewa wa wananchi bado ni changamoto na kwamba wakati mwingine wamekuwa wakichangia kuendelea kuwapo kwa vituo hivyo.
“Wananchi wengi wanapenda kwenda kwenye vituo vya watu binafsi kuliko hospitali za umma hata kama ziko karibu na maeneo yao, sawa hatukatai lakini wanapaswa kujiridhisha kama kweli pale wanapokwenda ni mahala salama.
“Wengine wanajulikana ni maarufu kama madaktari wa watoto lakini ukichunguza unagundua hata taaluma hizo hawana, ukimweleza mwananchi anaona kama unamuonea yule mtu,” anasema Mtendamema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma Binafsi za Afya (APHTA) katika Kanda ya Dar es Salaam, Dk. Lazaro Wambura, anasema kutokana na ongezeko la magonjwa na ufinyu wa rasilimali, serikali ilianzisha mfumo wa kushirikisha watu binafsi katika kutoa huduma za afya nchini (PPP).
Hata hivyo, anasema baadhi ya watoa huduma binafsi wamekuwa wakienda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa mfumo huo na kuwaharibia wengine ambao wanafuata taratibu.
“Sekta hii imevamiwa kama zilivyo sekta zingine, nami nikikuta mtu anatoa huduma kinyume cha sheria huwa naumia kwa sababu wako watoa huduma wanaotoa kihalali ambao walipaswa kuwaibua hawa lakini wanakaa kimya.
“Tunahimiza watu wapate huduma katika maeneo ya karibu lakini watoa huduma wahakikishe wanasimamia maadili na miongozo yote inayohusiana na taaluma za afya,” anasema Dk. Wambura.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Victorina Ludovick anasema wamekuwa wakipokea wagonjwa wengi hasa katika Hospitali ya Rufaa Amana ambao hufika wakiwa katika hali mbaya.
“Tunashirikiana na sekta binafsi lakini tunahimiza wananchi waende katika vituo vinavyotambuliwa na serikali, kwa sababu tumekuwa tukipokea wagonjwa wengi ambao ukiwachunguza unakuta walizembea katika matibabu.
“Na ukichunguza kwa makini unakuta alianza kupata tiba kwenye vituo ambavyo sisi hatuvitambui, hivyo tunahimiza wananchi kwenda katika vituo vya umma vilivyo karibu au kama anaamua kwenda ‘private’ basi aangalie vituo vinavyotambulika,” anasema Dk. Ludovick.
Anasema sekta binafsi inapaswa kutoa huduma za afya kwa jamii kwa kuzingatia sera na miongozo ya utoaji wa huduma hiyo nchini.
“Tutaendelea kufuatilia huduma za afya ambazo zinatolewa na watu binafsi ili zilingane na zile zinazotolewa katika vituo vya umma,” anasema Dk. Ludovick.