32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

SIRI KUU NI UBUNIFU ZAIDI YA WENGINE

Na ATHUMANI MOHAMED

WAPO mabingwa wa kulaumu, kuonea wengine vijicho na wale wasema hovyo kuhusu mafanikio ya wengine. Watu wa aina hiyo ni vigumu kusonga mbele, maana mafanikio ya wenzao kwao ni kero.

Wapo wengi sana kwenye jamii yetu. Mtu akifanikiwa, badala ya kumpa moyo, kazi yao ni kuwasema vibaya.

Utasikia: “Aaaah! Wapi, jamaa yule anatembea sana kwa waganga. Hana lolote. Dukani kwake anauza zaidi kwa sababu ya ushirikina!”

Yaani mwingine kuuza zaidi anawaza ni ushirikina tu. Hana fikra nyingine zaidi. Hajiulizi, kwanini yule anauza zaidi yake.

Ndugu zangu, kwenye maisha kulalamika pekee hakuna maana. Unaweza kuwa na wivu sana, unaweza kuwa na chuki sana au ukachagua kuwa bingwa wa kulalamika na kuhamasisha migomo lakini kamwe haitakusaidia hata siku moja.

Lipo jambo moja kubwa ambalo wengine hawalijui ndiyo maana wanapoteza muda wao kulalama; ubunifu. Hii ndiyo siri kubwa ya mafanikio.

 

UNAYO BIASHARA?

Kama wewe ni mfanyabiashara, siri kubwa zaidi ya kupata wateja wengi zaidi kuliko wengine ni kufanya vitu bora kuliko wengine.

Mfano una mgahawa wa chakula, wakati wengine wakiuza vyakula vya kawaida na mboga zake au vinywaji, wewe unaweza kuongeza na vitu vya nyongeza mfano mboga za asili nyingi kama mlenda, matembele, majani ya maboga, mlenda wa kusaga, kachumbari na vitu vingine.

Unaweza kushangaa watu wanakuja kwenye mgahawa wako na kuacha kwenda pengine kwa sababu tu ya kachumbari yako. Au unaweza kustaajabu wateja wanamiminika kwako kwa sababu tu una wahudumu wenye kauli nzuri kwa wateja.

Ukishakuwa mbunifu kwenye biashara yako, unakuwa wa tofauti na ni lazima upate wateja wengi zaidi kuliko wengine ambao hawana ubunifu.

 

WALIOKO MAOFISINI

Kwa walio maofisini wembe ni uleule tu, ubunifu. Mnaweza kuwa hata wafanyakazi sita au zaidi kwenye kitengo chenu, lakini utendaji wako ukawa wenye ubunifu kuliko wengine na ukaweza kujitofautisha kabisa na wengine.

Upe ubongo wako kazi ya ziada. Fanya kazi zako kwa ubunifu zaidi. Kazi ileile ikifanywa na wewe na akipewa mwingine kuonekane na utofauti.

Ni vizuri kutafuta kitu cha ziada ofisini. Ajira yako inakuwa salama zaidi ikiwa ikitokea siku unakuwa haupo kazini, basi watu wanahisi kukosekana kwa mtu muhimu. Usiishi bora siku zinakwenda.

Ukishakuwa wa tofauti, maana yake thamani yako lazima itapanda mahali pako pa kazi na utategemewa kwa mengi. Muhimu kuliko yote ni kwamba uhakika na usalama wa ajira yako unakuwa maradufu.

 

TAFUTA UBUNIFU KWA JUHUDI

Usiache muda wako upotee bure, muda wote fikiria kuwa bora zaidi. Ubora huo unapaswa kuutafuta kila kona na kwa juhudi zaidi. Tembelea mitandao mingi zaidi na kuangalia namna wengine wanavyofanya katika jambo ambalo unalifanya.

Siri ya kuwa mbunifu ni pamoja na kudadisi. Kuuliza si ujinga, unapojipanua zaidi mawazo kwa kujua mengi zaidi, inakusaidia kuongeza tija kwenye shughuli zako. Wanaoijua siri hii wanazidi kufanikiwa siku hadi siku.

Hakuna la zaidi. Wengine wanaweza kusema tofauti, lakini wewe tumia ubunifu kama silaha yako ya kwanza. Waliotumia silaha hiyo, wamefanikiwa maradufu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles