24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE EALA KIZA KINENE

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma juzi, baada ya uchaguzi wa wabunge watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Na FREDY AZZAH, DODOMA

LICHA ya wabunge wa Bunge la Tanzania kukaa kwa zaidi ya saa tisa kufanya uchaguzi wa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), huenda waliochaguliwa wasiapishwe hadi pale mgogoro uliopo utakapotanzuliwa na mahakama.

Hii inatokana na uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupinga  wajumbe wake wawili, Lawrence Masha na  Ezekiel Wenje kupigiwa kura nyingi za hapana na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusababisha msimamizi wa uchaguzi huo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah kutangaza kuwa nafasi hizo hazijapata washindi.

Juzi Bunge lilichagua wajumbe saba wa kuiwakilisha nchi katika Bunge la EALA, sita kati yao wakitoka CCM na mmoja kutoka Chama cha Wananchi (CUF) – upande wa Profesa Ibrahim Lipumba.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema wanakwenda mahakamani kudai haki yao iliyopokwa kwa makusudi na CCM.

Akizungumza nje ya Ukumbi wa Bunge juzi usiku, Mbowe alisema CCM wasifikiri wameshinda, bali walichofanya ni kutia chumvi katika ugomvi ambao haukuwa wa msingi.

“Tulichokuwa tunakifanya hapa ni kutafuta wawakilishi wa nchi na si wa vyama, lakini  kutokana na uvunjwaji wa kanuni na sheria, Chadema na CUF tutakwenda kutafuta haki mahali pengine.

“Leo (juzi) tulitarajia kuwapata wawakilishi wa taifa na tuwe tumemaliza uchaguzi huu, lakini ndiyo kwanza kwa matokeo haya na kwa utaratibu huu wa upindishaji wa sheria za uchaguzi, tutakwenda mahakamani kuitafuta haki yetu.

 “Spika amevunja kanuni za Bunge, sheria hazikuheshimiwa, ubabe umetumika, kwetu sisi hii ni sehemu ya mchakato wa demokrasia, tutaendelea kuitafuta haki yetu, nafasi mbili za ubunge wa Afrika Mashariki wapende wasipende ni za Chadema.

“Hawawezi kueleza sababu za msingi za kuwakataa wagombea wetu, kwa sababu wagombea wetu wana sifa, lakini kwa sababu wenzetu wana mkakati wa ki-CCM na kiserikali, wanakataa wagombea wazuri kwa sababu ambazo hatuzielewi.

“Kama mtu ambaye unathamini utaifa, tumeleta wagombea wazuri sana wawili, ambao ni ‘very competent’ (wana uwezo), wamewapigia kura za hapana kwa sababu ni mkakati wa CCM, tunaona ni ujinga na tunasema tutaendelea kupambana, kama chama bado nafasi zetu mbili zipo, tutarejesha tena wagombea wawili, tutakaoleta ‘who knows’ (nani anajua), tunaweza kuamua kuwarejesha hawahawa wawakatae kwa mara nyingine.

“Tutawarejesha tena wagombea hawahawa wawakate tena, watuambie wanatumia sheria gani kuwakataa wagombea wa upinzani.

“Wanajipaje uhalali wakutuchagulia sisi wapinzani ni nani wawe wawakilishi wetu, huo ni ujinga, hakuna demokrasia kama hii duniani,” alisema Mbowe.

HATIHATI KUTOAPISHWA WALIOCHAGULIWA

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, alisema kwa kilichofanyika katika uchaguzi huo na msimamo wa Chadema kwenda mahakamani, ni dhairi wabunge hao hawataapishwa hadi nafasi mbili zilizo wazi zizibwe.

 “Muhula uliopita Uganda walikuwa na mgogoro watu wakaenda mahakamani, wenzao walikaa kwa miezi sita bila kuapishwa, kwa hiyo hata hawa watakaa hadi nafasi mbili zikamilike kwa sababu sasa uchaguzi kwetu bado haujakamilika,” alisema.

 Alisema ni jambo la kusikitisha kwa wabunge wa CCM kupitisha wabunge wa Chadema kwa sababu za kisiasa, huku wenzao wa Rwanda, wakiwachagua Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mawaziri wawili kwenda katika Bunge hilo, jambo lililotokana na kuangalia zaidi masilahi ya taifa lao kuliko vyama.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Sophia Mwakagenda, alisema kupitishwa kwa wagombea wa CCM na CUF na kuachwa wale wa Chadema ni kazi bure kwa sababu sasa hawataapishwa hadi mgogoro uliopo uishe.

MASHA AWASHANGAA CCM

Aliyekuwa mgombea ubunge wa EALA, Masha, amewashangaa wabunge wa CCM kwa kile alichosema ni kupiga kura za chuki kuwakwamisha wenzao wa upinzani, akisema wameonyesha kiwango cha juu cha siasa zisizozingatia masilahi ya taifa.

Masha alisema hayo jana mjini Dodoma baada ya kutakiwa kutoa maoni yake juu ya mvutano ulioibuka kwenye uchaguzi huo, ambao umesababisha kutopatikana washindi wa chama chake baada ya kupigiwa kura nyingi za hapana na wabunge wa CCM.

Alisema anashindwa kuelewa yeye na Wenje wamepungukiwa sifa gani hadi kunyimwa kura.

“Kilichotokea jana kimenisikitisha sana, sioni kwanini mimi kuwa mwana Chadema ama kuhama CCM iwe sababu ya kuwa na wasiwasi na uzalendo wangu.

“Chama tawala kilitakiwa kuona watu makini wa kupeleka EALA, siyo kukwamisha uchaguzi. Wabunge wa Chadema walipiga kura kwa hao wa CCM na CUF, kwa kuangalia uzalendo na masilahi ya nchi, CCM wao wamefanya kitu cha aibu sana kwa nchi.

“Hawajui hicho walichokifanya kitasababisha hata hao waliochaguliwa hatokuapishwa katika Bunge la EALA bila kutimia kwa akidi halisi inayotakiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za bunge hilo,” alisema.

KASORO ZINAZOLALAMIKIWA

Baadhi ya kasoro ambazo CUF na Chadema wanalalamikia, ni pamoja na kulazimisha kuwapigia kura wagombea wake wawili wakati walipaswa kupita bila kupingwa.

Mbowe alisema katika mabunge mengine, pale nafasi zinazogombewa zinapolingana na idadi ya wagombea waliofikishwa bungeni, hupita bila kupingwa, lakini juzi Bunge lilikataa utaratibu huo.

Pia upande huo wa upinzani unasema kwa kawaida karatasi ya kura huwa inatakiwa mtu apigiwe kura kwa kuweka alama yoyote ile kwa mtu wanayemtaka, hivyo kitendo cha kuweka alama ya X na vyama kwenye wagombea wote wawili wa Chadema, inamaanisha kuwa kura za wagombea wote zimeharibika.

Kwa upande wa CUF, wanasema awali walikata rufaa kupinga uchaguzi wa nafasi moja ya chama hicho usifanyike na Bunge liliwapa barua ya kukubali ombi hilo.

Hata hivyo muda mfupi baada ya kikao cha uchaguzi kuanza, msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Bunge, Dk. Kashililah, alitangaza kufuta pingamizi zote.

Pia walisema mmoja wa wagombea wa CUF, alitangaza kujiuzulu kwa maneno wakati wa kujinadi ilihali kanuni zinataka kama mtu anataka kujiuzulu aandike barua kwa Katibu Mkuu wa chama chake siku moja kabla ya uchaguzi.

WALIOCHAGULIWA

Kwa mujibu wa matokeo hayo, kundi la wanawake CCM linawakilishwa na Happiness Lugigo aliyepata kura 196 na Fancy Nkuhi (197).

Wajumbe wa CCM kundi la bara, washindi ni Adam Kimbisa (266) na Dk. Ngwaru Maghembe (287), huku kutoka Zanzibar ni Dk. Abdullah Hasnu Makame (254) na Maryam Ussi Yahya (195).

Kundi la vyama vya upinzani, wagombea wa Chadema, Wenje alipata kura 124 za ndio 174 za hapana huku Masha akipata kura za ndio126 na hapana 198.

CUF inawakilishwa na Mhandisi Habibu Mnyaa aliyepata kura 188.

KAULI YA BUNGE

Mkuu wa Kitengo cha Habari Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya, akizungumza na moja ya kituo cha redio jana, alisema Chadema bado wanayo nafasi ya uwakilishi katika Bunge hilo kupitia nafasi hizo mbili.

Alisema kama Chadema wataamua kuwarejesha wagombea hao ili wapigiwe kura ni juu yao kuongeza nguvu za kuwashawishi wajumbe ili wawachague, huku akisisitiza kuwa kama kuna jambo la ziada Bunge litatoa taarifa.

WATOTO WA VIGOGO WAANGUKIA PUA

Katika hatua nyingine, uchaguzi huo uliofanyika juzi umeshuhudia watoto wa wanasiasa na waasisi wa taifa, Makongoro Nyerere na Zainabu Kawawa wakiangukia pua.

Katika uchaguzi huo, Makongoro ambaye ni mtoto wa baba wa taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere alipata kura 81 na kushika nafasi ya tatu ilihali kundi lake la wanaume bara likiwa na nafasi mbili.

Naye Zainabu ambaye ni mtoto wa waziri mkuu wa zamani, hayati Rashid Kawawa, pia alikuwa wa tatu baada ya kupata kura 137 huku kundi lake pia lilikuwa na nafasi mbili.

Dalili ya Zainabu kutofanya vyema zilianza mapema wakati akijieleza.

Zainabu alionekana kupata shida ikilinganishwa na wagombea wenzake na mara kwa mara alionekana kulalamika kwamba wabunge wanapiga kelele.

Naye Makongoro tofauti na alipoomba nafasi hiyo kwa mara ya kwanza miaka minne iliyopita, safari hii alionyesha unyonge, huku akilazimika kuomba msamaha kutokana na kauli zake alizotoa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, ambazo alisema yawezekana ziliwaumiza baadhi ya wabunge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles