26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

MTUHUMIWA AKIRI KUSHIRIKI MAUAJI YA DK. MVUNGI KWA UJIRA WA SH 30, 000

Na Kulwa Mzee – Dar es Salaam

MSHTAKIWA Paulo Mdonondo anayetuhumiwa na wenzake sita kumuua aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Dk. Sengondo Mvungi, anadai alishiriki katika tukio na alilipwa ujira wa Sh 30,000 kwa kazi aliyofanya.

Hayo yalibainika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati Wakili wa Jamhuri, Patrick Mwita, aliposoma ushahidi wa mashahidi 30 wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo Mahakama Kuu.

Mwita alidai mshtakiwa Paulo alipohojiwa Polisi, alikiri kushiriki katika tukio hilo na kwamba kazi yake ilikuwa kulinda majirani wasifike kutoa msaada kwa Dk. Mvungi wakati uvamizi ukifanyika.

Inadaiwa mshtakiwa huyo alikaa nje akiwa na mawe kuzuia majirani, alifanikiwa na akalipwa Sh 30,000 na tukio lilipomalizika alienda kupanda daladala kuelekea katika shughuli zake Kariakoo.

Mwita alidai kwa mshtakiwa Msigwa Matonya ushahidi unadai alikiri kushiriki katika tukio na ndiye aliyempiga mapanga Dk. Mvungi maeneo ya utosini.

Alidai kuwa baada ya tukio hilo, Matonya alikwenda kuyaficha mapanga matano Kibaha Maili Moja karibu na Hoteli ya Njuweni.

Kwamba alipokamatwa na kuhojiwa, aliwafikisha polisi mahali alikoficha mapanga hayo na yalikutwa katika mfuko wa salfeti.

Mahakama hiyo ilipokea ushahidi dhidi ya mshtakiwa John Mayunga anayedaiwa alikamatwa akiwa Jangwani katika Klabu ya Yanga alipokuwa akifanya mazoezi baada ya polisi kupata taarifa kuwa alikuwa na bastola ya marehemu.

Inadaiwa kuwa baada ya kukamatwa, alihojiwa na kukiri kuwa na vitu vya marehemu na polisi walipokwenda kupekua nyumbani kwake maeneo ya Kiwalani, walifanikiwa kukuta bastola moja iliyotengenezwa Marekani ikiwa imeficha juu katika tofali la kenchi ya nyumba, risasi 21 na unga wa baruti ukiwa umefungwa katika pakiti ya nailoni.

Wakili Mwita alisema ushahidi unadai kuwa mshtakiwa Chibago Chiligati alikuwa akitumia simu ya marehemu Dk. Mvungi kwa kutumia namba nyingine huku akiwasiliana mara kadhaa na Hamad Kitabu.

Kupitia Hamad, polisi walifanikiwa kumkamata Chiligati Novemba 6, 2013 saa mbili usiku.

Chiligati anadaiwa katika mahojiano alikiri kuiba simu ya marehemu, kushiriki katika tukio na wenzake aliowataja na kuwaongoza askari jinsi ya kuwapata.

Inadaiwa kwa msaada wa mshtakiwa huyo, polisi walifanikiwa kuwakamata washtakiwa walioshiriki katika uvamizi huo maeneo ya Vingunguti Relini baada ya kuwekewa mtego.

Mke wa marehemu Dk. Mvungi, katika ushahidi wake alidai kuwa Novemba 3, 2013 saa saba usiku, wakiwa wamelala nyumbani kwao Mbezi Msakuzi na mumewe, walisikia kishindo na wakaamka.

Akidai kuwa mumewe alielekea jikoni na yeye alielekea upande mwingine ambako hakukuta kitu, lakini wakati anarudi alikutana na majambazi sita.

Inadaiwa majambazi hao walikuwa vifua wazi, huku usoni wakiwa wamejificha kwa vitambaa.

Wakili Mwita alisema kuwa shahidi huyo alidai kuwa alimkuta mumewe jikoni hajitambui akiwa amekatwa mapanga utosini.

Inadaiwa majambazi hao walimlazimisha mama huyo kutoa fedha, na alitoa Sh milioni mbili, kisha walichukua simu yake na mbili za marehemu na bastola moja katika droo ya kitanda.

Naye aliyekuwa mfanyakazi wa marehemu, Eliya Alex, katika ushahidi wake alidai kuwa marehemu alikatwa panga kichwani na katika makalio.

Mfanyakazi huyo alidai kuwa jambazi mwenye lafudhi ya Kisukuma alichukua simu yake na kwamba anaweza kuwatambua kwa sababu walikaa muda mrefu ndani ya nyumba hiyo.

Hakimu Simba alipowauliza washtakiwa kama wanataka kuzungumza chochote mahakamani, wote walidai watakwenda kuzungumza Mahakama Kuu.

 Jalada hilo linahamia Mahakama Kuu kwa kuanza kusikilizwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Msigwa, Chiligati, Mianda Mlewa, Mdonondo, Longishu Losingo, Juma Kangungu na Mayunga ambao wanadaiwa kwa kukusudia walimuua Dk. Mvungi kwa kumkata mapanga kichwani.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles