Na LEONARD MANG’OHA
MWELEKEO wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 uliotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, hivi karibuni unaonyesha kuwa bajeti hiyo imeelekezwa zaidi katika miradi ya maendeleo hususan ya ujenzi wa reli, miradi ya gesi na makaa ya mawe Liganga na Mchuchuma.
Kuelekezwa kwa fedha nyingi kwenye miradi ya ujenzi, kunagusa dhamira ya Rais Dk. John Magufuli kuhusu ukamilishaji wa miradi ya maendeleo itakayosaidia kuinua sekta ya viwanda.
Kuimarika kwa sekta ya viwanda kutapunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza bidhaa nje ya nchi ambazo zinaweza kuzalishwa nchini sambamba na kutoa ajira kwa wazawa.
Kutajwa kwa mradi wa Linganga na Mchuchuma kama moja ya vipaumbele, kunaibua matumaini mapya kwa Watanzania walio wengi ambao wamekuwa wakingoja kukamilika kwa mradi huo japo si mara ya kwanza kutolewa maneno ya matumaini kuhusu maendeleo yake.
Mradi wa Liganga na Mchuchuma
Kwa mujibu wa Meneja Mawasiliano wa Shirika la Maendeleo Tanzania (NDC), Abel Ngapemba, mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu hadi mitano, huku ukitarajiwa kugharimu zaidi ya Sh trilioni 6.564.
Anasema mikataba ya mradi huu ilikwishasainiwa na utafiti kiasi cha chuma na makaa ya mawe yaliyopo na teknolojia itakayotumika wakati ya uchimbaji tayari vipo wazi.
Anaeleza kuwa, uchimbaji wa chuma cha Liganga unahitaji teknolojia maalumu kutokana na chuma kinachopatikana eneo hilo kuwa na sumaku tofauti na madini ya aina hiyo yanayopatikana sehemu nyingine duniani.
Anasema ujenzi wa mradi huo unachukua muda mrefu kutokana na kuhusisha miradi mitano ambayo ni pamoja na migodi miwili ya makaa ya mawe na chuma, kinu cha umeme wa makaa ya mawe, kiwanda cha kutengenezea bidhaa za umeme na ujenzi wa njia ya kusafirishia nishati kutoka Mchuchuma hadi Liganga.
Megawati 600 za umeme kuzalishwa
Ngapemba anasema mradi huo utakaotekelezwa na Kampuni ya Kichina ya Sichuan Hongda Cooperation Limited, utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme Megawati 600 ambapo kiwanda cha chuma kitatumia Megawati 250 na zitakazosalia zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Kati ya hizo Megawati 250 zitatumika katika kiwanda cha kufua chuma kitakachojengwa Liganga, huku Megawati 350 zikitarajia kuingizwa katika gridi ya Taifa.
“Umeme huu utapelekwa katika ‘sub-stantion’ ya Makambako hivyo ni wazi kuwa utapunguza tatizo la kukosekana kwa umeme na kusaidia kuanzisha kwa viwanda vingine na unaweza kuongezeka baada ya kuanza uzalishaji,” anasema Ngapemba.
Mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu za makaa ya mawe na tani milioni moja za chuma kwa mwaka, hivyo ni wazi kuwa itapunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza chuma kutoka nje ya nchi.
Kuwainua wananchi kiuchumi
Anasema katika kuhakikisha wanainua kiwango cha uchumi kwa wananchi wa maeneo ambayo mradi huo unatekelezwa ambapo tayari wamekuwa wakiwapa semina kuhusu namna ya kutumia fursa zinazopatikana kutokana na utekelezaji wake.
“Tumekuwa tukiwashawishi wananchi kujihusisha na shughuli za uzalishaji, kuwaweka kwenye makundi na kuwawezesha ili waendeshe shughuli zao kwa urahisi.
“Hii itawasaidia kupata fedha kwa kutumia fursa za mahitaji kwa watu watakaokuwa wakifanya kazi hapa. Kwa mfano wakati wa hatua hizi za uchunguzi, wananchi walifanya biashara ya kuuza kuku kwa wingi,” anasema Ngapemba.
Ngapemba anasema ili kuhakikisha wananchi wananufaika na mradi huo, wameamua kuwajengea wale ambao maeneo yao yataingizwa kwenye mradi badala ya kupewa fedha ili kuwawezesha kupata makazi bora.
“Tutahakikisha tunaanzisha kijiji kwa kuwajengea na kuweka huduma muhimu kama shule kwa gharama ya mradi na kwa wale watakaochukuliwa maeneo au mazao yao pia watafidiwa,” anasema.
Ngapemba anasema mradi huo unalenga kuwezesha kuanzishwa kwa miradi mingine kwa kuipa nishati na kufungua fursa nyingine za uwekezaji.
Kuchochea maendeleo ya sekta nyingine
Mtaalamu wa uchumi na mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Kilimo (SUA), Profesa Damiani Gabagambi, anasema kukamilika kwa mradi huo pamoja na kutoa faida za moja kwa moja kama nishati na ajira, pia utatoa matokeo zaidi (multiplier effect) kwa sekta nyingine.
Anasema kwa wafanyakazi watakaoajiriwa, watanunua bidhaa mbalimbali kwa matumizi yao binafsi, hivyo kukuza biashara katika maeneo ya karibu na mradi.
Anasema wakulima wataweza kuuza mazao yao ya kilimo na mifugo, hivyo nao watainuka kiuchumi.
Bila shaka sekta za hoteli na nyumba za wageni zitaimarika kutokana na kuongezeka kwa mwingiliano wa watu katika eneo hilo.
Kuimarisha Bandari ya Mtwara
Kukamilika kwa mradi wa Mchuchuma na Liganga kutaongeza ufanisi wa Bandari ya Mtwara ambayo Serikali imeanza juhudi za kuiboresha, hivyo wafanyabiashara wataweza kupitisha mizigo yao wanayoagiza kutoka nje ya nchi.
Kuimarika kwa shughuli za bandari hii kutachagizwa zaidi na uwapo wa reli ya kiwango cha kimataifa (standard gauge) inayotarajiwa kujengwa katika ya Bandari ya Mtwara hadi Mbambabay, Mchuchuma na Liganga ambapo tayari upembuzi yakinifu umekamilika na Kampuni hodi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) wakiwa kwenye mchakato wa kumtafuta mshauri wa fedha ili kufahamu kiasi kitakachotumika kujenga mradi huo.
Bandari hiyo inaweza kuimarika zaidi ikiwa nchi jirani za Kongo DRC, Zambia na Malawi zahitaji kutumia reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,000 ambako kutakuwa na gharama nafuu ikilinganishwa na Bandari ya Dar es Salaam ambapo hulazimika kusafiri umbali mrefu zaidi.
Kwa muda sasa, Bandari ya Mtwara imekuwa hoi kutokana na meli kubwa kutotia nanga bandarini hapo kwa kukosa gati kubwa linalostahimili mahitaji wa meli hizo.
Mapema mwezi uliopita akiwa ziarani mkoani Mtwara, Rais Dk. Magufuli aliwataka wakandarasi waliosaini mkataba wa kupanua bandari hiyo kuanza kazi mara moja na kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya miezi 20.
Bila shaka maboresho hayo yatafungua fursa za usafirishaji ambapo wafanyabiashara wa mikoa ya kusini na Kusini Magharibi wataingiza mizigo yao kupitia huko.
Kwa jitihada zinazooneshwa na Serikali ikiwa zitapewa nguvu inayostahili na miradi ya aina hii kutekelezwa kwa weledi, utaleta tija katika ukuaji wa uchumi wa nchi.