Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam
ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaa, Suleiman Kova amesema marafiki wengi wa viongozi si marafiki wa kweli bali ni marafiki wa viti vyao.
Kova alisema hayo mwishoni mwa wiki katika uzinduzi wa Chuo Cha Fursa (APEC) kilichopo maeneo ya Ukonga ambapo mkurugenzi wa chuo hicho alimualika kuhudhuria hafla hiyo.
“Mkurugenzi wa APEC, Respicius Timanywa, alikuja ofisini kwangu mwaka 2010 akitaka ushauri na kupata maelekezo kuhusu mtaala wa kufundishia bodaboda, tuliandaa pamoja naye, leo amenikumbuka kanialika katika uzinduzi wa chuo.
“Ni watu wachache sana wanaoweza kukumbuka, wengi ni marakifi wa kiti chako sio wewe,ukitoka katika kiti ukimpigia simu hapokei na mwingine anaitika kisha anazima kabisa,”alisema Kova na kuwataka wengine kuiga mfano wa Timanywa.
Kamanda huyo alisema kwa sasa anajishughulisha na kutoa ushauri wa masuala ya maafa, majanga na uokoaji.
Alisema amefungua taasisi inaitwa Kova Foundation inayoshughulikia hayo kwa ushirikiano na ofisi ya Waziri Mkuu katika kuratibu na kufundisha.
Chuo cha APEC kilichozinduliwa kinatoa mafunzo ya udereva wa pikipiki, uchimbaji visima virefu na usambazaji maji safi na salama, mafunzo ya uanzishwaji wa viwanda vya kufyatua matofali, utunzaji wa mazingira na kozi nyingine mbalimbali za muda mfupi na mrefu.
Timanywa anaomba Serikali iwape usajili wa muda mrefu mara tu baada ya usajili wa muda mfupi kumalizika baada ya miezi mitatu.