28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KAMPUNI YENU IKIAMUA KUPUNGUZA WAFANYAKAZI, UTABAKI SALAMA?

Na ATHUMANI MOHAMED

KUNA baadhi ya watu hufanya mambo yao ilimradi siku zinakwenda, hawana mipango madhubuti ya kuangalia ili kuona namna ya kuzidi kusogea kwenye mafanikio.

Somo la mafanikio ni pana, lakini ijulikane wazi kuwa mafanikio ni pamoja na mchakato mzima wa maisha ya kila siku. Wakati fulani, hali za uendeshaji wa makampuni mbalimbali huwa siyo nzuri.

Biashara zikiwa chini kidogo, hulazimika kupunguza baadhi ya wafanyakazi katika baadhi ya idara. Si habari njema sana kwa wafanyakazi. Kupunguzwa kazi, maana yake kutasababisha baadhi ya waajiriwa kukosa ajira.

Si lengo la mada hii kujadili hilo kwa undani, lakini swali la kujiuliza kwako wewe uliyeajiriwa ni je, ikiwa ofisi yako itaamua kupunguza wafanyakazi kwa sababu yoyote ile, utabaki salama?

Tunajadili mada hii kutokana na ukweli kwamba, baadhi ya wafanyakazi maofisini wamekuwa wategaji, wakitumia uzoefu wao, umaarufu wao na kujulikana kwao kugeuza ofisi kama vijiwe vya kupumzikia tu.

Je, unadhani umaarufu wako ndiyo ufanyaji kazi wako? Je, unaamini kujulikana kwako na mabosi ndipo kutakapokubeba? Majibu ya maswali haya yanaweza kuwa ndiyo kwa watu wenye tabia hizo, lakini jibu sahihi ni siyo kwa kampuni zinazoamua kupunguza wafanyakazi wake.

SABABU ZA KAMPUNI KUPUNGUZA WAFANYAKAZI

Zipo sababu nyingi za makampuni kuamua kupunguza wafanyakazi wakati fulani, lakini kubwa zaidi ni kupanda kwa gharama za uendeshaji huku uzalishaji ukishuka.

Hii ni kanuni ya kawaida ya makampuni mengi; kwamba kwa sababu gharama za uendeshaji zimekuwa juu maradufu wakati kinachoingia kikiwa chini, uongozi kwa nia njema huamua kupunguza wafanyakazi ili kunusuru kampuni.

Jambo kubwa na la muhimu wanalozingatia ni kuchuja wale wafanyakazi hodari ambao hufanya kazi kwa weledi, ubunifu, wasionung’unika, wanaojituma, wanaojiongoza – hawa kampuni huondoka nao ili kuvuka katika kipindi kigumu.

Kampuni huangalia zaidi wafanyakazi ambao wana uwezo wa kufanya kazi ya zaidi ya watu wawili kwa wakati mmoja. Katika hili mwenye spidi ya kazi na nidhamu huangaliwa zaidi.

TABIA ZINAZOWEZA KUKURUDISHA NYUMBANI

Kampuni ikishakuwa katika hali hiyo, jambo la kwanza kuzingatia wakati wakiangalia watu wa kuwapunguza kazi ni kwenye daftari la mahudhurio.

Kama una tabia ya utoro, uchelewaji kazini au kuingia na kuondoka baada ya muda mfupi, utakuwa kwenye hatari ya kuondolewa kazini.

Wale wenye tabia za uvivu, kufanya kazi kwa kutegea wanakuwa kwenye hatari kubwa ya kupunguzwa kazi. Kwa kawaida katika kipindi kigumu cha kampuni, ofisi itahitaji kuvuka na wale ambao uvivu kwao ni mwiko kabisa.

  • Fitina, uchonganishi

Vidomodomo na wachonganishi wana hali mbaya. Hii humaanisha kuwa, hata wale ambao ni wachapakazi wazuri, sifa ya kuchukua maneno sehemu moja na kupeleka kwa wengine, inatosha kumwondoa kazini.

Muhimu kuzingatia ni kwamba, kuwa na bidii kazini pekee hakuna maana ikiwa una tabia ya kufitini na kuchonganisha watu.

  • Kutoheshimu mamlaka

Watu wenye tabia hii huonekana hatari hata kama wana uwezo mkubwa kazini. Mfanyakazi ambaye haheshimu mamlaka yaliyo juu yake – ambaye hamshimu bosi wake au mkuu wake wa idara yupo kwenye hatari kubwa sana ya kupunguzwa kazi.

Kampuni hufikiria mara mbili kuhusu mtu ambaye haheshimu mamlaka, hata kama akiwa mchapakazi kiasi gani, akiachwa anaweza kuhamasisha migomo au mgongano kwa wafanyakazi dhidi ya wanaowaongoza.

Wapo wale wasiokubali kuelekezwa, kukosolewa. Hawa huamini zaidi akili zao kwa kila kitu. Watu wa namna hii huogopwa maofisini maana huamini zaidi akili zao.

Katika kipindi cha mpito, ambacho kampuni huzingatia zaidi kupunguza matumizi, hufikiria zaidi watu hawa kuowaondoa ili kuiacha kampuni salama ikiwa na watu wenye fikra zinazorekebishika.

MUHIMU:

Kazi ni muhimu sana, unaweza kuiona haina maana kwa sababu unayo, lakini ukiwa nje ya geti la waajiriwa utaona umuhimu wake. Fanya kazi kwa bidii huku ukiepuka mengi (kama yanavyosomeka hapo juu) na mengine ambayo unayaona wazi kuwa ni kinyume na taratibu za kazi.

Kumbuka kwamba unafanya kazi na watu, hivyo zaidi ya kufanya kazi kama kutimiza majukumu, tambua kwamba uhusiano mwema bila kuzingatia cheo, dini, rangi wala kabila ni muhimu zaidi kuliko yote!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles