29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

USIKIMBILIE KUSAINI MKATABA, TAFAKARI KWANZA

Kwa muda mrefu sana wasanii wetu wanalia kuhusu masilahi yao. Tangu zamani wasanii wetu wamebakia kuwa na majina tu, lakini mafanikio sifuri.

Ni kama wanarithishana kizazi hadi kizazi. Kwa wasanii wa zamani ambao kwa bahati nzuri mpaka sasa bado wapo hai, wengi wana hali mbaya kiuchumi. Hawana uhakika na hatma ya maisha yao.

Ukiambiwa huyu ndiye msanii fulani aliyeimba nyimbo zilizoipaisha Tanzania unaweza usiamini. Waliotangulia mbele za haki, wamekufa kinyonge. Wamefariki kwa mateso.

Waimbaji wa bendi zetu za zamani wanaweza kuwa mfano mzuri. Sina haja ya kutaja bendi tulizonazo ambazo bado zipo, lakini nenda kawatembelee uone maisha yao yalivyo magumu.

Tuachane na muziki wao wa sasa, tuangalie michango yao waliyoitoa wakati wakiwa vijana. Je, wanatuzwa au wamepotezewa?

Hawa ni wale walioimba nyimbo za kuhamasisha kampeni mbalimbali za kitaifa. Waliojitolea kwenye sikukuu muhimu za taifa letu, lakini leo hii wapo choka mbaya. Tunawajua na tunawaacha tu.

Ikitokea la kutokea, ndiyo matamko yanaanza. Rambirambi na salamu kutoka taasisi mbalimbali. Wanasahau kabla ya mauti, msanii huyo alikuwa na uhitaji. Alisaidiwa nini wakati wa uhai wake?

Mchango wake ulitambulika vipi? Hayo ni mambo ya msingi kutafakari. Huu ndiyo ukweli, kwamba wasanii wetu wanateseka, wananyonywa.

Angalau wasanii wa siku hizi wana pa kuanzia, tena ni kwa sababu walijiongeza na kujitahidi kwa juhudi zao wenyewe angalau kujikimu mahitaji yao muhimu, lakini ukweli ni kwamba bado.

Pamoja na hayo, wapo ambao mambo bado si mazuri. Kwa mfano wasanii wetu wa filamu, sasa hivi wana hali mbaya, lakini ukiangalia sababu utagundua kuwa kikwazo ni mikataba!

Msanii akishindwa kuwa makini kabla ya kusaini mkataba wake ndipo balaa linapoanzia. Wasambazaji wa filamu za Kibongo ndiyo wanaonufaika zaidi kuliko wasanii, ndiyo maana wengi wapo hohehahe.

Soko linaporomoka. Wapo wasanii wa muziki wa Bongo Fleva, wanalia sana kuhusu malipo wanayopewa kwenye matamasha. Narudia tena, tatizo ni mikataba.

Wasanii msiwe wepesi wa kusaini haraka mkataba kabla ya kutafakari. Umeitiwa dili, chukua mkataba, omba muda upitie na utafakari, kisha ukiamua ndipo usaini.

Si ajabu katika nusu saa utakayopitia mkataba huo utagundua upungufu sehemu kadhaa na kuomba marekebisho, mambo yakaenda sawa. Tafakari kabla ya kusaini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles