27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI ITAFITI  UFUNGAJI WA BIASHARA NA KUTOA TIBA

WAKATI ripoti za taasisi mbalimbali zikionyesha kuwa uchumi kwenye sekta mbalimbali unakua na mapato ya kodi yanaongezeka, mitaani biashara zimekuwa zikifungwa kila leo, chanzo kikielezwa kuwa ni ukame wa wateja.

Soko la Kariakoo, Dar es Salaam, ni moja ya masoko makubwa nchini, ambalo mbali na kuhudumia Watanzania, pia wafanyabiashara kutoka nchi jirani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi, Burundi na maeneo mengine, hufika kila siku kununua bidhaa ambazo huenda kuziuza kwenye mataifa yao.

Kwa ufupi, Kariakoo ni sawa na Dubai ya nchi nyingi zinazoizunguka Tanzania.

Philimin Chonde, ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wanaoendesha biashara zao kuzunguka soko hilo, anasema asilimia kubwa ya wafanyabiashara wa eneno hilo wanafanya shughuli zao katika mazingira magumu.

Kutokana kupungua kwa wateja, anasema baadhi ya wanachama wake wameshindwa kulipa kodi za pango; na hadi sasa maduka 80 yamefungwa.

Anasema wamiliki wa maduka hayo ni kati ya wanachama wao 2,000.

Meneja Mipango na Shughuli za Biashara wa soko hilo, Mrero Mgeni, anasema kutokana na mzunguko wa fedha kuwa chini, wafanyabiashara wengi wameshindwa hata kulipa kodi.

Kwa kawaida kila mfanyabiashara hapa anatakiwa kulipia kodi ya pango kila mwisho wa mwezi, lakini kwa sasa inapofika tarehe 30 wengi wao wanashindwa kulipa, yote hii ni kwa sababu biashara ni mbaya.

Mfanyabiashara wa duka la jumla na rejareja lijulikanalo kama Baygon Shop, lililopo eneo hilo, Zuberi Saidi, anasema kabla ya mwanzoni mwa mwaka 2016, biashara ilikuwa nzuri, lakini kwa sasa mambo ni tofauti, wateja ni wachache sana.

Kwamba biashara ni mbaya kupita maelezo, yaani wafanyabiashara wanatamani miaka  irudi nyuma wajikute katika hali iliyokuwapo mwanzo.

Wateja wengi ni wale wenye maduka mikoani ambao kwa miaka ya nyuma walikuwa wakinunua vifaa vingi sana katika soko la Kariakoo.

Kwa siku katika soko hili mteja alikuwa  anaingiza hadi Sh 2,000,000. Sasa hivi wateja ni wachache, siku biashara ikiwa nzuri sana mteja anapata Sh 300,000 tu, na hapa hii fedha si wanapata yote, sehemu kubwa wanatoa mizigo kwa malikauli, wafanyabiashara wakauze kisha ndipo walipe.

Mbali na hali ngumu ya wateja, wateja wanalalamikia mlolongo wa kodi bandarini wakati wa kutoa mizigo, na hii ni changamoto nyingine inayozidisha ugumu wa biashara kwao.

Kwa upande wa nafaka, mfanyabiashara Alhaj Kidula, anasema bei hazijashuka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Anasema mchele kilo moja ni kati ya Sh 2,000 hadi 2,500; na gunia moja la kilo 100 huuzwa kwa Sh 200,000 hadi 250,000.

Kwamba pamoja na bei hizo kubakia hivyo, bado wateja ni wachache sana tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Katika hotuba yake ya hali ya uchumi aliyoisoma bungeni mwaka jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema ripoti ya hali ya uchumi katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana inaonyesha kuwa biashara nyingi zilifungwa.

Tunasema Serikali sasa ifanye tathmini kuhusu suala hili na kutoa tiba kabla ya mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai 1 (mwaka huu).

Tunasema hivyo kwa sababu watu inabidi wafanye biashara kujipatia mapato na kuendelea kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles