31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KUWE NA CHOMBO CHA KUSIMAMIA VYOMBO VYA USALAMA

KATIKA siku za karibuni kumekuwa na  masuala yanayoibuka ambayo yamekuwa yakileta maswali mengi.

Unaweza kujiuliza kwamba hivi hiki ni kipindi gani ambacho tunakipitia kutokana na mambo mageni mengi na kama si mageni basi yameonekana bayana kuliko ambavyo tulizoea huko nyuma.

Kisa cha ‘askari kanzu’ kumtolea bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye kimezua mjadala na taharuki miongoni mwa jamii hasa baada ya tukio hilo kufuatiwa na lile la chombo cha habari kuvamiwa wakiwemo askari wenye silaha.

Hizi silaha huwa hazitumiki kiholela na watumiaji huwa wana mamlaka kamili ya kufanaya hivyo na hasa wakiwa ni askari wa jeshi lolote nchini.

Niliposhuhudia tukio hilo la kuchomolewa kwa silaha mbele ya kadamnasi ya watu na mtu aliyekuwa Waziri saa chache zilizopita akilengwa na silaha ile niliamini nchi iko katika hali tofauti na mpya kuliko tunavyoweza kuielewa.

Tukio hilo lilinipeleka mbali kidogo na kunifanya nitafakari. Nikaukumbuka mchakato wa Katiba Mpya uliokuwa unaendelea nchini. Wakati wa mchakato huo tulipata fursa ya kutoa maoni mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba. 

Moja ya mapendekezo yalihusu uwepo wa chombo maalumu cha kuliangalia Jeshi la Polisi. Hii dhana niliipata nilipotembelea nchi moja huko ulaya.

Huko tulikutana na mkuu wa chombo maalumu ambacho kinaangalia mwenendo wa polisi nchini humo. Mkuu huyo alitupa historia ya kuwepo kwa chombo hicho. Hiyo historia ndio ilinivutia na nikaona matokeo yake hata hapa kwetu yangefaa.

Mkuu huyo alitueleza kuwa kuna siku askari wawili walikuwa kazini na mbele yao akaletwa mtu ambaye alikuwa mhamiaji haramu kwa lugha ya huku kwetu. Alikuwa si mtu wa ulaya bali ni wa Taifa jingine na askari mmoja wapo akamtishia yule ndugu kwa bastola akimwambia kuwa atamfumua ubongo wake.

Yule mtu aliogopa sana, alionekana kutetemeka kwa hofu kuu. Ile bastola ilikuwa haina risasi lakini aliyetishiwa hakujua kuwa haina risasi hivyo aliogopa mno. Yule askari mwingine hakupendezewa kabisa na kitendo kile kwa hiyo alipeleka taarifa kwa mkuu wao wa kazi.

Yule mkuu wa kazi alifanya uchunguzi na ilipothibitika yule askari aliachishwa kazi. Taarifa ya kitendo kile kilitolewa taarifa kwenye vyombo vya habari. Mkuu wa  huduma ya polisi nchini aliamua kujiuzulu kutokana na tukio hilo.

Naona huku watu watashangaa kuwa kwani ni yeye ndiye alimtuma. Tuliambiwa kuwa mkuu huyu wa Polisi aliamua kuachia ngazi akisema kuwa hawezi kuwa kiongozi iwapo alishindwa kuwa na askari wenye maadili na weledi kazini.

Aliona kuwa uwepo wa askari asiye na utu kiasi kile ni aibu kwake kama kiongozi na akajiuzulu.Tuliokuwa tunasikiliza kisa kile tulishangaa na hivi wote tulitoka nchi za kiafrika kila mtu alisema lake.

Matokeo ya kujiuzulu mkuu yule na kisa kizima hicho kikawa chimbuko la kuunda chombo cha kuimulika polisi.(Policing the Police). Yaani polisi wasiwe wanafanya kazi wakidhani kuwa wanayofanya wao hayawezi kuangaliwa na mtu zaidi yao.

Wasipofanya kazi kwa weledi na maadili basi waweze kumulikwa na kuchukuliwa hatua. Chombo hicho kiliundwa na watu ambao ni wastaafu wa polisi waliojulikana kwa uadilifu wao.

Kila polisi katika nchi ile alipewa jukumu la kuwa mwangalizi wa polisi mwenzake na akiona hafanyi ipasavyo au anafanya vitendo viovu basi atoe taarifa. Hii ilionekana kuwasaidia sana polisi wa nchi ile kutofanya vitendo vinavyovunja maadili na weledi wa kazi na hata uvunjifu wa haki za raia.

Nilitamani na sisi tuwe na chombo kama hicho. Tume haikukubali wazo letu na kwa hali hiyo hata kwenye Katiba Pendekezwa haikuwepo.

Kwanini ninakumbuka sana hiki chombo? Ni kutokana na hali ya matumizi ya silaha hapa nchini na hasa watu wanaosemekana kuwa ni polisi wanavyotumia silaha hizo kwenye matukio mbalimbali. Tukio Nape Nnauye lilikuwa dhahiri kabisa mbele ya kadamnasi na vyombo vya habari ambavyo vingine vilikuwa na kamera na vikionesha moja kwa moja.

Hapakuwa na mantiki au hata sababu ya mtu yule aliyoonekana kuwa na mamlaka ya kumzuia aliyekuwa Waziri kwa kumtolea silaha kwa aina ile. Kile kilikuwa kitendo cha kutishia uhai wa mtu na hata wale waliokuwa wako hapo kwenye eneo la tukio.

Iwapo silaha ile ingefyatuka maana yake wangeweza kudhurika hata watazamaji tu. Haya yalishatokea kwa mwandishi wa habari kule Nyololo Iringa tukampoteza kwa hali ambayo haikuwana na sababu.

Lile la Iringa pamoja na kuwa kuna mtu aliyechukuliwa hatua lakini viongozi wake hawakuwajibika wala kuwajibishwa kama tulivyosikia kwa yule kiongozi mkuu katika  nchi ile niliyemzungumzia hapo juu.

Kwa hili lililojitokeza tena kwa hali kama hii tunadhani ipo sababu kubwa sana ya kuona umuhimu wa kuunda chombo kitakachokuwa na mamlaka ya kufuatilia matukio kama haya ambayo polisi  wanawaza kuwa wanatumia vibaya mamlaka yao.

Hadi sasa kama raia hatujajua yule mtu wa silaha iwapo alikuwa ametumwa kufanya vile na aliyemtuma ni nani na kwa sababu gani. Pia hatujaona au kusikia zipo hatua zozote ambazo tayari zimechukuliwa. Hatujasikia pia iwapo mtoa silaha yule alikuwa ni mwana usalama au la.

Kila tukiongea, tukizunguka tunarudi pale pale kuwa tunahitaji chombo huru katika eneo hili. Polisi hawawezi kujidhibiti wenyewe, kujionya wenyewe. Ipo hali ya kulindana, kuoneana huruma na kadhalika.

Iwapo nchi iliyoendelea kama hiyo nilioitaja imeweza kuwa na chombo cha kuisimamia polisi kwanini nasi tusifuate mfano huu? Si kila mfano ni wa kufuata lakini kwa hali inavyokwenda hapa kwetu  tunahitaji kabisa chombo hicho.

Pamoja na kuwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora bado kingefaa kiwepo maalumu kwa polisi na wana usalama wengine hasa wanohusika na raia.

Mchakato wa Katiba ukirudi inatubidi tujenge hoja kiupya ili pawe na uwezekano wa kuwepo na mabadiliko na kuwa na chombo cha kuiangalia polisi. Uzuri wa chombo hiki pia kinaweza kuwasaidia polisi pale ambapo wameonewa au wamesingiziwa.

Lakini pia itakuwa hakuna vitendo kama hiki kilichotokea kwa Nape vitakavyoachwa vipite tu bila kufanyika kwa uchunguzi na kuwajibika kwa mhusika na kwa aliyemtuma iwapo itathibitika kuwa alihusika katika kulea hali kama hiyo.

Inabidi tufike mahali tuone umuhimu wa kuthamini utu wa mtu mwingine na kuheshimu kazi na kuzifanya kazi hizo si kwa kuonyesha ubabe bali kwa uangalifu na kwa weledi na maadili makubwa ya kazi.

Ninadhani kuna jambo linaloendelea ndani ya Jeshi la Polisi kwa haya matukio mawili ya hivi karibuni. Kikubwa tunachotahadharisha ni kuwa nchi hii yenye demokrasia iendeshwe kwa misingi ya sheria na utawala wa sheria lakini kikubwa ni heshima ya utu wa mtu yeyote, tena yeyote yule.

Kila mtu ameona jinsi ambavyo yeyote anavyoweza kukutwa na dhahma tuliyoiona hivi karibuni. Wote tuitishe uwepo wa chombo hicho muhimu kwa Tanzania.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles