25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

KINGUNGE: WATU WAMEBANWA WATAKAPOPUMUA LITAKUWA GHARIKA

NA EVANS MAGEGE,

“WATU watakuwa wamebanwa hata kupumua wanashindwa, siku watakapopumua litakuwa ni gharika, kwa hiyo lazima tufanye mabadiliko ambayo ni chanya na si hasi,” hii ni kauli ya mwanasiasa mkongwe nchini ambaye pia ni mwasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale- Mwiru.

Katika toleo la Jumapili iliyopita gazeti hili liliandika habari  iliyotokana na mahojiano maalumu na mwanasiasa huyo ambaye alizungumzia mambo mbalimbali, ikiwamo mustakabali wa Taifa.

Msingi wa mahojiano hayo ilikuwa ni kupata ufafanuzi wa nchi inakoelekea, kikubwa ni mabadiliko ya kikatiba yaliyofanywa hivi karibuni na CCM.

Mbali na mambo mengine, Kingunge aliyaeleza mabadiliko hayo ya kikatiba ndani ya CCM kuwa si jambo jipya, bali ni mwendelezo wa makosa yaliyofanywa wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka juzi.

Bila kumung’unya maneno aliwataja Mwenyekiti Mstaafu, Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, kuwa wanapaswa kubeba lawama za usaliti ndani ya chama hicho.

Aligusia hoja ya baadhi ya makada kuvuliwa uanachama, akiwamo Sophia Simba, kwa kosa la usaliti.

Mengine ni uamuzi wa kamati kuu wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais, madaraka ya kiimla pamoja na mtazamo wake juu ya CCM kujiingiza mahali pagumu.

Endelea kufuatilia sehemu ya pili ya mahojiano haya. Mzee Kingunge anahitimisha hoja yake kwa kuwatia moyo waliovuliwa unachama, uhitaji wa mabadiliko kama nchi, ikiwamo maoni yake juu ya dhana ya utumbuaji pamoja na mshangao wake kuhusu kutofautiana kwa kauli kati ya Rais na waziri wake juu ya  tangazo la ulazima wa kuwa na vyeti vya kuzaliwa kabla ya kufunga ndoa.

Kupingana ni dhambi?

Wakati wa mahojiano hayo amezungumzia hoja ya usaliti kwa kirefu, huku akihoji mara kwa mara kwamba nani aliyesaliti wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM.

Kingunge anasema wakati wa mchakato kila mwanachama alikuwa na mgombea wake na kila wagombea walikuwa na wadhamini wao.

Anahoji: “Nani alikuwa anampinga mwenzake? Na kupingana kwani ni dhambi? Tangu lini kupingana ukawa ni usaliti? Amesalitiwa nani? Na CCM hakiwezi kudai kwamba kilisalitiwa chenyewe kwa sababu hakikuhusika.

“Ndani ya CCM mkutano mkuu ulimchagua Magufuli mwishoni. Sasa wawatafute wale waliompinga Magufuli kwa ngazi ya mkutano mkuu, lakini na wao vilevile hawawezi kuitwa wasaliti, wale ambao hawakumpa kura Magufuli katika ngazi ya mkutano mkuu huwezi ukawaita wasaliti,” anasema.

Awatia moyo waliovuliwa uanachama

Katika hatua nyingine, Kingunge anawatia moyo watu waliovuliwa uanachama wa chama hicho pamoja na wale waliopewa onyo, akiwamo Emmanuel Nchimbi na Adam Kimbisa.

Anawataka wasibabaike kwa sababu kama bado wanaipenda CCM waombe warudishwe, aliongeza kwa kusema dunia si CCM, kwa sababu kabla ya CCM kulikuwa na TANU, akahoji kwani wakati hapakuwapo TANU binadamu hawakuishi?

“CCM ni yangu kwa maana ile tuliyoijenga, lakini haiwezi kuwa yangu kwa maana ya CCM hii. Yale malengo tuliyokubaliana katika CCM yanabaki kuwa malengo yangu …kwa hiyo marafiki zangu hawa wafurahi tu kwa sababu hii dunia ni ya kwetu wote, mtu unaweza kuishi bila chama na ukiona lazima ujiunge na chama vyama vipo vingi na vingine ni vizuri tu na vinaungwa mkono na watu, wala hakuna sababu ya kusononeka, maana mtu unapoonewa wewe ndio shujaa, mwonezi yeye ndiye mwenye matatizo,” anasema.

Nchi inahitaji mabadiliko

Kingunge anakwenda mbali zaidi kwa kusema nchi inataka mabadiliko makubwa kwa sababu kila kukicha mambo yanaonekana.

Anasema nchi lazima ibadilike kwa sababu pasipokuwapo na mabadiliko inaweza kufika pabaya.

“Watu watakuwa wamebanwa hata kupumua wanashindwa, siku watakapopumua litakuwa ni gharika, kwa hiyo lazima tufanye mabadiliko ambayo ni chanya na si hasi,” anasema.

Katika mtazamo huo anasema hana uhakika kama dhana ya utumbuaji majipu inayotekelezwa na Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli ni mabadiliko chanya au hasi.

“Nina matatizo sana, unajua madaktari huwa wanatumbua majipu kwa kuliangalia kwanza kama limeiva analitumbua, anasafisha kwa kutoa uchafu wote kisha kidonda anakitia dawa na kukishona. Lakini haya majipu yanayotumbuliwa kila siku sijui, kama kazi yenyewe ni kutumbua tu huwezi kuwa na uhakika kama ule usaha unakwenda wapi.

“Kwa hiyo kutumbua ni jambo moja, lakini la pili ni kubwa zaidi, ni kutibu. Hili ni kama vile jengo bovu, jengo bovu lazima libomolewe, ndiyo hatua ya kwanza, ukishabomoa ndio unajenga sasa, lakini kama wewe kazi yako ni kubomoa tu hufiki kwa sababu mwisho wa yote wote watakuwa hawana nyumba.

“Kwa hiyo tutumbue sawa, lakini mtaanza lini kujenga, maana kila siku nasikia kutumbua tu, utumbuaji unanoga sana lakini je, baada ya kutumbua unafanya nini? Kwa hiyo kwa upande mmoja naunga utumbuaji, lakini kwa upande wa pili nasema kutumbua pekee hakutoshi, uanze na kujenga,” anasema.

Anasema kama watu wangekuwa huru kufanya mikutano yao ya hadhara na maandamano, kungesaidia kupata mawazo mapya ya kuboresha.

“Leo hii watu hawana haki ya kukusanyika, kujadili maendeleo ya nchi yao, wakati mwingine wana mambo yanawakera, wanakuwa ni watu wamenuna tu, wanatembea barabarani wamenuna hawasemi kitu, si umeishawanyima haki zao halafu kesho unataka uendeshe nchi sijui ukalete viwanda, sasa unamletea nani na wakati watu hawazungumzi?

“Lazima watu watumie haki, maana yake haki hii hatupewi na viongozi wa sasa na hatukupewa na viongozi waliopita na wala hatukupewa na Mwalimu Nyerere, hizi ni haki za kuzaliwa kwetu,” anasema.

Anasema binadamu anazaliwa na haki ya kuwa mtu, hivyo watu wasifikirie kwamba haki ni ya mtu mmoja kuwa yeye ndiye atoaye ruhusa au ana haki ya kunyima ruhusa; “mkifika hapo hamuitakii mema nchi yenu,” anasema.

Amshangaa Dk.Mwakyembe

Katika hatua nyingine, Kingunge alishangaa tangazo alilolitoa (aliyekuwa) Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, ambalo lilikuwa na maudhui ya katazo la kufunga ndoa kama huna cheti cha kuzaliwa.

Dk. Mwakyembe alitoa tangazo hilo ambalo lilitenguliwa kesho yake na Rais Dk. John Magufuli.

Katika maelezo yake, Kingunge alihoji sababu za Dk. Mwakyembe kutoa katazo hilo kuwa lililenga kumfurahisha nani?

“(Kicheko)… Mwakyembe amekwenda so low (chini sana) kwanini? Anataka kumfurahisha bwana mkubwa? Lakini hawa watu mara nyingine kama huna mambo unayoyaamini katika dunia hii mara nyingine unakuwa na ubabaishaji babaishaji tu eh! ndio hivyo, lakini Mwakyembe ni disappointing kweli (amevunjika moyo), kuna kauli nyingine alisema sometime headlines (wakati mwingine ni vichwa vya habari), siwezi kukumbuka vizuri …lakini ilifika mahali nilihoji ni Bwana Mwakyembe huyu huyu ninayemfahamu?

“Unajua ni mwanasheria wa CCM…eh! nilikuwa naye mle, tulikuwa katika bodi moja …(kicheko tena)…sasa anasema hamna kufunga ndoa mpaka uwe na cheti cha kuzaliwa, hivi kwanini sasa amefanya vile, pengine kavurugwa sana?

“Kwa sababu namjua Mwakyembe ni aina ya mtu intelligent (mwenye akili nyingi)…sasa watu wangapi wanahangaika na mambo ya vyeti vya kuzaliwa? Unajua kwa sasa watu wengi wanahangaika na maisha yao tu.

“Ala! Lakini ndio nchi yenyewe hii, ndio Tanzania yenu nyie vijana na hawa ndio viongozi wetu (kicheko). Wakati mwingine Magufuli amenifurahisha sana kwa uamuzi huo eh!  watu kama hawa anawaaibisha (kicheko) mpaka Kyela watasikia hiyo,” anasema Kingunge.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles