29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

VIJANA NI RASILIMALI MUHIMU KATIKA UTUNZAJI MAZINGIRA NCHINI

Na Raleigh, Tanzania.


UHARIBIFU wa mazingira ni suala linalopigwa vita na wadau wote wa mazingira duniani kwani licha ya kuharibu mazingira husababisha maafa na uharibifu wa miundombinu.

Yako mazingira mbalimbali yanayosababisha uharibifu wa mazingira kama vile kutotunza vizuri mazingira hao au yale ya asili ikiwamo mafuriko na mabadiliko ya hali ya hewa.

Katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba imeshajitanabaisha kuwa imeanza kulipa uzito unaostahili suala la uharibifu wa mazingira ambao umelikumba taifa kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Taarifa ya siku ya 12 ya ziara waziri huyo ya Oktoba mwaka jana, yenye lengo la kutambua changamoto za kimazingira na kuweka mikakati sahihi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na pia kutengeneza mahusiano ya karibu zaidi katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira kati ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, watu binafsi pamoja na taasisi za Mazingira.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Makamba anakiri kuwepo kwa changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira na alisisitiza juu ya umuhimu wa utunzaji mazingira na ulinzi kwa vyanzo vya maji ikiwamo maeneo ya misitu nchini.

Mathalani, takwimu za kiserikali zinaonesha kuwa kasi ya uvunaji misitu nchini kwa miaka 10 iliyopita ni kati ya hekta 300,000 hadi 400,000 kwa mwaka.

Kwa mujibu Injinia Mwihava, Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Muungano na Mazingira, kasi hii ya uvunaji misitu ikiendelea, taifa litapoteza eneo la misitu linalolingana na ukubwa sawa nchi ndogo ya Rwanda.

“Hali hii inatokana na kukosekana kwa uwiano kati ya kasi ya ukataji na upandaji miti nchini, na kwa kiasi kikubwa imechangia kutokea kwa athari kubwa za mabadiliko tabia nchi katika ngazi ya taifa,” anasema.

Je, taifa linatumiaje rasilimali zake katika kuhakikisha kuwa suala la utunzaji wa mazingira linafanikiwa?

Katika mkutano wa wakuu wa nchi na wadau wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa uliopitisha malengo 17 ya maendeleo endelevu (Development Goals) mwaka 2015 ulitambua kuwa vijana ni rasilimali kubwa na muhimu dunia iliyonayo kwa sasa.

Licha ya utambuzi huo lakini katika sehemu nyingi duniani wamekuwa hawathaminiwi na wakidhaniwa kuwa hawawezi kutimiza baadhi ya malengo.

Nchini Tanzania, vijana wenye umri wa kati ya miaka 15-35 ni zaidi ya asilimia 36, kwa mujibu wa Sensa ya Idadi ya watu na makazi ya mwaka 2012, likiwa ni kundi kubwa zaidi katika idadi ya watu nchini.

Mathalani, baadhi ya vijana kupitia taasisi za kijamii na mashirika yasiyo ya kiserikali wamekuwa wakifanya jitihada kubwa za kuhamasisha utunzaji mazingira na upandaji miti nchini, kwa mfano kampeni ya upandaji wa miti milioni 50 ifikapo mwaka 2020 nchini iliyoanzishwa na kusimamiwa na shirika lisilo la kiserikali la Raleigh International Tanzania kupitia kwa vijana Zaidi ya 1000 nchini kote sio jambo la kupuuzwa. Raleigh International, yenye makao yake makuu nchini Uingereza na Morogoro kwa Tanzania ilianza kampeni hii kwa kushirikiana na vijana waliokwisha kujitolea na shirika hilo, shirika ambalo kila mwaka huchukua wastani wa vijana 500 na kuwawezesha na mafunzo mbalimbali na kwenda kujitolea kusaidia jamii maeneo ya vijijini hasa yale ambayo hayafikiki kirahisi.

Kwa kushirikiana na vijana hao wanaounda Jumuiya ya Vijana ya Raleigh, waliona umuhimu wa kushirikiana na katika kuleta maendeleo endelevu katika sekta ya mazingira hasa kutokana na uharibifu mkubwa ambao umekwishafanyika nchini.

Hadi sasa wameshashirikiana na serikali za mikoa mbalimbali nchini, shule za msingi na sekondari, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na wadau wengine wa maendeleo, lakini juhudi hizi hazitatosha kama hakutakuwa na juhudi za taifa zima kuunga mkono.

Kampeni hii mahsusi ya upandaji miti milioni 50 imechukua wazo la uwepo wa Watanzania wapatao idadi hiyo na hivyo idadi ya miti inayopandwa inapaswa kulingana na idadi ya watu nchini.

Kwa taarifa zilizopo kwa kipindi cha miezi mitatu tu kuanzia Desemba mwaka jana zaidi ya miti 12000 imepandwa na vijana hawa bila kulipwa, kwa njia za kujitolea tu.

Kampeni hii ya upandaji miti inashirikisha jamii na kila Mtanzania mpenda mazingira na ikiwa lengo hili litafikiwa kwa kupanda miti milioni 50 ndani ya miaka mitatu ijayo kufikia 2020 basi ni dhahiri kuwa tuna nafasi kubwa ya kubadilisha hali ya kimazingira nchini na kupunguza madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.

Serikali na idara zake zinaunga vipi mkono mawazo na juhudi za namna hii? Ni wazi na dhahiri kuwa serikali kupitia wizara ya mazingira na wadau wengine wa maendeleo endelevu wanapaswa kuwekeza nguvu kubwa zaidi katika kulinda mazingira nchini, na kwa sasa rasilimali muhimu zaidi ya kutumia ni vijana ambao wameshajiunga katika vikundi au taasisi ndogo ndogo zilizopo nchini kote.

Kwa mfano, serikali isaidie vijana katika kuanzisha vitalu vikubwa vya miti nchini kote katika kila wilaya au jimbo na miti hiyo itolewe kwa bei nafuu au bure kabisa bila ukiritimba wala urasimu kwa jamii ili kuleta hamasa ya upandaji miti. Kwakuwa utunzaji mazingira ni kama falsafa, mpango kama huu ukianzishwa ndani ya miaka mitatu ijayo tutaona jamii ikibadilika na kutambua umuhimu wa ukijani na ukuaji wa kijani nchini.

Lengo la kuleta hamasa ya upandaji wa miti milioni 50 haliwezi kuwa la taasisi moja, au kikundi cha vijana wachache. Ni lengo linalohitaji uungwaji mkono wa serikali, taasisi na sekta binafsi na wadau wote wa maendeleo. Vijana waungwe mkono na wawezeshwe katika kusaidia kuleta maendeleo katika taifa letu hasa kwenye maswala ya kimazingira na uhamasishaji wa uchumi wa kijani ambao ni ufanyaji wa shughuli za maendeleo kwaajili kupunguza umasikini kwa kuzingatia utunzaji na ulindaji wa mazingira ya asili kwaajili ya kizazi cha leo na cha baadae. Muhimu zaidi, serikali na wadau binafsi wahakikishe kuwa wanaunga mkono juhudi kama hizi kwa kusaidia pale vijana wanapokwama kwani mipango kama hii kwa vijana siyo ya kibinafsi bali ni ya kijamii na ya kitaifa kwa maendeleo ya sasa na ya baadae.

Katika mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter na Instagram, kampeni hii inaendeshwa kwa alama ya reli na maneno #50MillionTrees na #Youth4GreenGrowth

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Maoni yangu ni kwamba sapoti ya serikali katika upatikanaji wa mbegu na viriba vya kuoteshea miti ni mdogo sana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles