25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MABADILIKO CCM: JPM KUIPATA CCM ANAYOIMUDU?

Mwenyekiti wa CCM Rais Dk. John Magufuli akiongoza moja ya vikao vya chama hicho

NA EVANS MAGEGE,

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo wanatarajiwa kuwa na kazi kuu moja ya kubariki mtazamo mpya wa mabadiliko ya muundo wa utendaji wa chama, ili kuendana na kasi inayotakiwa na chama hicho chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Rais John Magufuli.

Matarajio ya mabadiliko hayo pia yanaweza kuwa tofauti kama wengi wanavyodhani, ikiwa wajumbe wa mkutano mkuu wataamua kukataa mapendekezo ya mabadiliko hayo, ambayo yameridhiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC), Desemba 13, mwaka jana.

Kwa jinsi utamaduni ulivyo ndani ya chama hicho, ni wazi kuwa, mtazamo mkubwa si rahisi kwa wajumbe wa mkutano huo kukataa mapendekezo yanayopitishwa na NEC, lakini lolote linaweza kutokea na kushangaza wengi, kwa sababu  mkutano mkuu ndio mkutano wa mwisho wa kutoa uamuzi ndani ya chama hicho.

Kama wajumbe wa mkutano mkuu watakuwa katika mwelekeo chanya kwa kukubaliana na mapendekezo ya kufanya mabadiliko yaliyopitishwa na NEC, hilo litakuwa jambo jema ‘bingo’ kwa kiongozi wa CCM, Rais John Magufuli, ambaye dhamira yake ya kuiongoza CCM anayoimudu itakuwa imetimia.

Kupitishwa kwa mabadiliko hayo unaweza kutafsiri kama kutoboa tundu jipya la mkanda ili Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli akiuvaa mkanda umtoshe, tayari kwa safari yake ya miaka mitano ya mhula wake wa kwanza wa kukiongoza chama hicho.

Kwa watu wanaoifahamu CCM kindakindaki wanaamini kuwa leo mabadiliko lazima yapitishwe na wajumbe wa mkutano mkuu,  ingawa kiuhalisia baadhi ya wana-CCM hawayapendi.

Tayari Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humprey Polepole ametanabaisha kuwa mabadiliko yanayotarajiwa kupitishwa leo na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho yamelenga kuifanya CCM kuwa mfano katika kuzingatia maadili, kusikiliza shida za wananchi, uchapakazi, kusimamia mali za chama na umma kubaki kwenye mikono salama.

Polepole alikaririwa na gazeti moja la kila siku (Si Mtanzania) akisema mabadiliko ya muundo na mfumo wa uongozi ndani yake yamekusudia kupinga umangimeza na ubinafsi wa baadhi ya viongozi wenye kutoa uamuzi wenyewe  katika mtazamo wa masilahi yao binafsi.

CCM ya leo inahitaji kuondoa umangimeza pekee?

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana anasema umangimeza si tatizo wala  si ugonjwa pekee unaokisumbua CCM.

Profesa Bana anasema mtazamo wa mabadiliko ujikite zaidi kuondoa fikra mgando jambo ambalo ni muhimu kwa chama.

“ Umangimeza utabaki lakini ubaki ule unaojielekeza katika kuleta ufanisi si vinginevyo,  CCM ni taasisi haiwezi kuondokana na umangimeza na urasimu hivyo vitakuwapo tu lakini umangimeza uwe ni ule wa lazima wenye kuleta tija kwenye chama,” anasema Profesa Bana.

Anasema mabadiliko yanayofanyika ni kukiwezesha chama kutoa uamuzi wa haraka na kutumia gharama kidogo za kutoa uamuzi wa kuwa na muda wa kuyatekeleza kwa kupima mafanikio.

Kwanini Mwenyekiti anahitaji mabadiliko?

Kuna mitazamo tofauti inayoangalia dhima nzima ya mabadiliko ambayo Mwenyemkiti wa CCM, Rais John Magufuli na baadhi ya makada wa chama hicho wanayahitaji.

Mtazamo wa wengi unaangalia kwamba, mabadiliko yaliyodhamiriwa leo ni kujenga msingi au kuweka rekodi ya kwamba kiongozi mkuu wa chama hicho, Rais Magufuli, ndani ya kipindi chake amefanya mabadiliko fulani ndani ya chama hicho.

Hoja kama hiyo Profesa Bana anaichangia kwa kusema: “Nadhani kiongozi yeyote ambaye watu watamkumbuka kwa historia ni kiongozi ambaye amesimamia au kuasisi mabadiliko, akayasimamia hatimaye watu wakapima matokeo ya mabadiliko hayo, kama yatakuwa na tija. Hivyo watu wataona kama ni kiongozi anayewafaa, kama mabadiliko yatazidi  kuwachosha basi uongozi wake unaweza ukawa na dosari,” anasema Profesa Bana.

Mabadiliko yataongeza nguvu ya chama?

Kwa makada wa CCM wanaelewa vizuri jinsi hali ya nguvu ya chama ilivyokuwa siku za nyuma, kwa miaka ya hivi karibuni au kwa CCM ya sasa.

Wanayatazama mabadiliko yanayotarajiwa kupitishwa leo kwa fikra mbili ambazo ni rahisi kimtazamo, kwamba yanaweza kuongeza nguvu kwa wale watakaoyakubali kuyaishi, mtazamo wa pili, CCM kama taasisi kubwa wapo wanachama ambao hawataweza kuyaishi mabadiliko hayo, ingawa watajificha chini ya kundi la watiifu.

Yapo mazingira na matukio kadha wa kadha yanayoweza kutumika katika kutathmini hali halisi ya nguvu ya chama ilipofikia sasa, japokuwa wana-CCM wenyewe si wepesi wa kutoka hadharani kuelezea wapi waliteleza na badiliko lipi halifai kupitishwa na lipi linahitajika sasa.

Pamoja na mtazamo wa jumla kuonyesha kuwa mabadiliko ambayo Rais Magufuli anatarajia yataungwa mkono na wajumbe wa mkutano mkuu, yanaweza kuleta nguvu ya chama.

Wadadisi wa mambo kutoka ndani ya chama wanadokeza kuwa, nguvu hiyo inaweza kujijenga katika misingi ya fedha pekee,  kwa maana ya chama kupunguza matumizi makubwa ya fedha za mikutano na si ushawishi wa itikadi kwa wanachama wake.

Mtazamo huo wa wadadisi unatoa picha kuwa, mabadiliko hayo yanaweza kukipa nguvu chama kutoka mikononi mwa tabia ya ombaomba kwa wafanyabiashara wakubwa, kisiasa inawezekana chama kikapata shida kidogo kama kutakuwa na kundi kubwa la wanachama ambao ama watahisi kujeruhiwa na mabadiliko au kufuata mkumbo wa wale ambao hawako tayari kuyaishi mabadiliko hayo.

Msingi huo unajengwa kwa picha ya historia kuwa mambo ya sasa si kama ilivyokuwa zamani kwa mfumo wa chama kimoja kilichoshika hatamu, kwa sasa watu hawajitambulishi kwa picha ya chama, bali ni kutokana na mambo yalivyobadilika sana.

Hivi sasa ni nadra kukutana na wanachama wanaojitambulisha kwa taswira ya chama, lakini ni rahisi kukutana na wanachama wanaojinadi kuwa chama chao kina nini na kinaongozwa na watu wenye mwelekeo upi.

Maisha ya kisiasa ya leo yanazungukwa na vyama vingi vya kisiasa, ingawa havishiki hatamu, hata hivyo, ni lazima uongozi uliopo ujitofautishe na hali ilivyokuwa chini ya mfumo wa chama kimoja kwa maana ya mazoea ya siku za nyuma.

Leo hii watu wanamwangalia Rais Magufuli si tu kama nguzo ya CCM, bali chachu ya mabadiliko. Chachu hiyo inaweza ikakifanya chama kiwe na mvuto kwa wananchi kwa sababu wanamwangalia kiongozi kuliko mipango yake au itikadi zake.

Pia, wana-CCM wanamwangalia Magufuli kwa hoja kuwa anakipeleka wapi chama au anakiongoza vipi, je, anaondoaje makovu au anaondoaje magamba?

Ukijikita katika hoja ya kuondoa makovu inatia shaka kidogo kama anaweza kuyaondoa kwa mkupuo, lakini atakuwa ameanzisha safari ya kukisafisha chama na kujijengea uwezo wa kifedha kuweza kuendesha kampeni zake bila kutegemea wafadhili.

Kwa msingi wa faida ya chama kuwa ni watu, basi manufaa ya mabadiliko ni kubaki na watu wanaoendana naye kifikra (wana-CCM watakaoyaishi mabadiliko), lakini wale ndumila kuwili au mamluki ambao walihujumu chama katika uchaguzi mkuu wa mwaka juzi wanaweza kuondoka.

Mtazamo wa mabadiliko

Mtazamo wa kuhitaji mabadiliko hayo ulizaliwa na mkutano wa NEC  uliofanyika Desemba 13, mwaka jana, jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulipokea taarifa ya Tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, baada ya kuitafakari taarifa hiyo, Halmashauri Kuu iliamua kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao na idadi ya vikao vya chama katika ngazi mbalimbali, ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa chama na kuongeza muda wa viongozi wa chama kufanya kazi za chama kwa umma badala ya kutumia muda mwingi vikaoni.

Muundo huo mpya wa mabadiliko yaliyopendekezwa na NEC umekusudia kupunguza wajumbe wa NEC kutoka 388 hadi 158.

Mchanganuo wake

Wenyeviti wa mikoa ya Bara ni 26 kwa maana ya kila mkoa kuwa na mwenyekiti mmoja. Wenyeviti wa mikoa Zanzibar ni 6 kila mkoa kuwa na mwenyekiti mmoja.

Wajumbe wa NEC wa mikoa ya Bara ni 26 kila mkoa mjumbe mmoja, kwa upande wa Zanzibar wenye mikoa sita wajumbe watakuwa 24 kila mkoa utatoa wajumbe wanne.

Wajumbe wa NEC wa Taifa kutoka Bara watakuwa 15 na kutoka Zanzibar 15, huku nafasi za Mwenyekiti ni saba.


Wajumbe wa NEC wa Jumuiya kama Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ni watano, Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) watano na Jumuiya ya Wazazi watakuwa wajumbe watano.

Kwa upande wa wajumbe wa NEC kutoka bungeni watakuwa watano, Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CC, Wajumbe watatu wa NEC kutoka Baraza la Wawakilishi na Katibu wa Kamati ya Wawakilishi.

Pia mchanganuo huo unawalenga wajumbe wa NEC wanaotokana na nyadhifa zao, ambao ni Mwenyekiti wa CCM, Makamu Mwenyekiti Bara, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Wengine ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi , Katibu Mkuu (UWT) na  Katibu Mkuu wa UVCCM.

Mbali na mchanganuo huo, mabadiliko mengine yanayotarajiwa kupitishwa leo ni pamoja na vikao vya kawaida vya Halmashauri Kuu ya Taifa kufanyika kila baada ya miezi sita badala ya miezi minne kama ilivyo sasa, isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalumu inapohitajika.

Pia, wajumbe wa Kamati Kuu wawe 24 badala ya 34 kwa mchanganuo wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) na
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar).


Wengine ni Makamu wa Rais, Katibu Mkuu wa CCM, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Waziri Mkuu, Makamu wa Pili wa Rais (Zanzibar) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Mwenyekiti wa UWT, Mwenyekiti wa UVCCM, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Oganaizesheni na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Itikadi na Uenezi.


Katika kundi hilo wamo Katibu wa  Halmashauri Kuu ya Taifa wa Uchumi na Fedha, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Wajumbe watatu wa kuchaguliwa na Halmashauri Kuu kutoka Tanzania Bara na Wajumbe watatu wa kuchaguliwa na Halmashauri Kuu kutoka Zanzibar.

Mabadiliko mengine ambayo wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wanatakiwa kuyafanyia uamuzi ni kupunguza vikao vya kawaida vya Kamati Kuu, kwamba vifanyike kila baada ya miezi minne badala ya miezi miwili, ila vinaweza kufanyika vikao maalumu inapohitajika.

Kupunguza wajumbe wa kamati za siasa za mikoa kwa kuondoa wajumbe watatu ambao ni katibu wa uchumi na fedha wa mkoa, wajumbe wawili wa halmashauri ya mkoa.

Aidha, wanatakiwa kufanya mabadiliko katika muundo wa vikao vya kawaida vya kamati ya siasa ya mkoa kwamba vifanyike kila baada ya miezi mitatu, badala ya kila mwezi kama ilivyo sasa, hata hivyo, vinaweza kufanyika vikao maalumu inapohitajika.

Kwa upande wa wilaya nako wajumbe wa mkutano mkuu wanatakiwa kutoa uamuzi wa mabadiliko juu ya wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya kuwa wapunguzwe kwa kuwaondoa katibu wa uchumi na fedha wa wilaya, katibu wa kamati ya madiwani, wajumbe wanne wa kuchaguliwa na Halmashauri Kuu ya Wilaya.

Mabadiliko mengine yanayotakiwa kufanyika ni vikao vya kawaida vya kamati ya siasa ya wilaya vifanyike kila baada ya miezi mitatu badala ya kila mwezi, isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalumu inapohitajika.

Pia, mabadliko hayo yamekusudia kuweka muundo wa wilaya kichama uendane na muundo wa sasa wa Serikali kwa maana ya kata, tawi na shina, kwamba idadi ya kuanzisha shina iwe wanachama 50 hadi 300.

Idadi ya kuanzisha tawi iwe wanachama kuanzia 301 hadi 1,000. Hata hivyo, idadi hii izingatie eneo la kijiografia na wingi wa wanachama katika eneo hilo.

Mabadiliko hayo yanalenga vikao vya kawaida vya kamati za siasa za ngazi hizo viwe vinafanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu, inapobidi vinaweza kufanyika vikao maalumu.

Katika muktadha huo huo, nafasi za uongozi
mwanachama anatakiwa kuwa na nafasi moja tu ya uongozi wa kazi za muda wote kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za uchaguzi wa chama toleo la 2012 kifungu cha 22 na 23, ambazo zimetajwa kuwa; mwenyekiti wa tawi, kijiji au mitaa.

Mwenyekiti wa kata, mwenyekiti wa jimbo, wilaya na mkoa. Makatibu wa halmashauri kuu wa ngazi zote zinazohusika, mbunge, mwakilishi na diwani.

Mabadiliko mengine ambayo wajumbe wa mkutano mkuu wanatakiwa kuyafanyia uamuzi leo ni viongozi wa kuchaguliwa waepuke kuwa watendaji, badala yake waongoze na kusimamia shughuli za chama kwa kuzingatia katiba na kanuni.

Vyeo ambavyo havijatamkwa kwenye Katiba ya CCM haviruhusiwi katika chama au jumuiya zake, mfano umoja wa makundi mbalimbali kama wenyeviti wa ngazi mbalimbali (mfano: mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, makamanda wa UVCCM, washauri UWT na walezi wa Jumuiya ya Wazazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles