AGATHA CHARLES- Dar Na
MUHAMMED KHAMIS (UoI) -ZANZIBAR
HATUA ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kutoa siku 14 kwa wadaiwa sugu ikiwamo Serikali ya Zanzibar kuhakikisha wanalipa deni vinginevyo itawakatia nishati hiyo, imeleta mzozo baina ya shirika hilo na Serikali ya Zanzibar.
Mbali na mzozo huo, bajeti ya visiwa hivyo inaonyesha deni hilo si rahisi kulipika kwa mara moja kama Tanesco ilivyoagiza na endapo hilo litawezekana shughuli nyingine za uendeshaji wa Serikali zitasimama.
Juzi Rais Dk. Ali Mohamed Shein, alipoulizwa juu ya visiwa hivyo kukatiwa umeme alisema: “Ngoja basi uzimwe kama nyie mna wasiwasi, mimi najua hawawezi kuzima, kwa sababu ya deni? Deni hatukuanza kudaiwa leo sisi, miaka 20 iliyopita tunadaiwa.
“Hivyo mimi sitaki niseme sana kwenye hili, nasema kama utazimwa, basi tutawasha vibatari vyetu, hatuna tatizo sisi, lakini sidhani Tanzania iliyo makini kama itafanya namna hii, hilo sidhani na sina hakika magazeti yameandika vizuri,” alisema.
Jana Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, alisema kuna haja ya kuangaliwa upya makubaliano ya malipo ya deni la umeme ambalo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inadaiwa na Tanesco.
Alisema hatua hiyo inapaswa kutekelezwa kwa sababu Zanzibar iligharamia mfumo mzima wa utoaji umeme Dar es Salaam hadi visiwani humo bila ya mchango wowote kutoka Tanesco wala Serikali ya Muungano.
“Kutokana na hali hii haiwezi kuwa sawa kwa Zanzibar kuendelea kulipa umeme kama wanavyolipa wateja wengine, lazima kuwepo na punguzo ukizingatia gharama zetu tulizotoa,” alieleza Aboud.
Alisema anaamini huduma hiyo haiwezi kusitishwa kwa Zanzibar kwa sababu deni hilo lipo kwa miaka mingi.
Ugumu wa kulipika kwa deni
Kwa mujibu wa bajeti ya Zanzibar ya mwaka 2016/17, visiwa hivyo vinatarajia kukusanya Sh bilioni 841.5.
Kati yake ni fedha za ndani ambazo mara nyingi ndizo zenye uhakika kupatikana ingawa si kwa asilimia 100, Mamlaka ya Mapato Zanzibar inatarajiwa kukusanya Sh bilioni 188.8 na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ikitarajiwa kukusanya Sh bilioni 237.4.
Endapo taasisi hizo mbili zitakusanya fedha hizo kwa asilimia 100, mapato yake yatakuwa Sh bilioni 426.2 hivyo basi wakilipa Sh bilioni 127 wanazodaiwa na Tanesco watabaki na Sh bilioni 299.2 ambazo itakuwa vigumu kuendesha Serikali.
Kutokana na hali hiyo, Mbunge wa Jimbo la Magomeni visiwani Zanzibar, Jamal Kassim Ally (CCM), aliliambia MTANZANIA Jumamosi jana kuwa kuna mambo matatu yanayofanya Zanzibar kushindwa kulipa deni lake kwa wakati.
Jambo la kwanza alilitaja ni kitendo cha Tanesco kuiuzia Zeco umeme kwa bei ya juu ukilinganisha na wateja wengine.
Alisema Tanesco inaiuzia Zeco unit moja ya kVA kwa shilingi 16,550 huku wateja wengine wa viwandani kwa Tanzania Bara wakiuziwa kwa Sh 13,200 hadi 15, 000.
“Ukiangalia katika biashara, huyu mteja mkubwa tulitarajia kuona bei yake ikiwa ndogo kuliko hawa wadogo,” alisema Jamal.
Alisema pia kuna gharama ambazo Zeco inatozwa na Tanesco ambazo hazistahili, akitolea mfano tozo ya Wakala wa Kupeleka Umeme Vijijini (REA).
“Gharama hii inaisaidia Tanesco katika kusambaziwa umeme na kuongeza wigo wa wateja wake lakini pia Zeco imekuwa ikiibeba bila yeye kunufaika na chochote. Pia tujue Zeco anatumia gharama kubwa katika kuusambaza umeme na maintenance (matengenezo) ya miundombinu ya umeme ambayo Tanesco haichangii chochote katika gharama hizo tofauti na wateja wengine wote wa Tanesco,” alisema Jamal.
Jamal alisema kwa kipindi kirefu, Zeco ilishindwa kutoza bei stahiki kulingana na gharama ya umeme kutoka Tanesco kutokana na maelekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Hilo lilitokana na hali ya uchumi wa Zanzibar na purchasing power (nguvu ya manunuzi) ya wananchi. Kwa hiyo Zeco ilijikuta ikilipwa kidogo,” alisema Jamal.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na ujenzi ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi (CCM), Hamza Hassan Juma, alisema kiwango cha deni la Zanzibar kilichotangazwa na Tanesco hakiko sahihi.
Alisema deni wanalolijua wao ni Sh bilioni 82 na kwamba anashangaa leo jambo kama hili kuwekwa hadharani licha ya nchi hizi mbili kuungana na kufanya mambo kwa ushirikiano.
“Hatujawahi kupata hata siku moja mapato ya nishati ya gesi licha ya kuwa umeme wa Tanesco kwa asilimia kubwa sasa unatokana na nishati hiyo, hili nalo mbona hawalisemi,” alihoji Hamza na kuongeza:
“Mimi nikiwa kama mjumbe, tumekwenda Tanzania Bara kuzungumza na viongozi wa Tanesco na kukubaliana kuunda kamati maalumu ya kushughulikia jambo hili, leo nashangaa kusemwa hadharani.”
Alisema kwa makusudi Tanesco imekuwa ikiitoza gharama kubwa Zeco kama vile ni wakala wao wakati ni shirika kama yalivyo mengine.
Alisema anaamini Tanesco inafanya haya kwa makusudi maana wanajua Zeco hutumia gharama zao wenyewe kuleta umeme Zanzibar na kusambaza vijijini.
Kutokana na hayo, alisema imefika wakati sasa Serikali ya Zanzibar kujitathmini na kuanzisha kituo cha kuzalisha umeme wenyewe kwa lengo la kuondoa changamoto za aina hii.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, Suleiman Sarahani Sadi, alisema waliotoa taarifa hiyo walipaswa kufikiria zaidi kabla ya kuutangazia umma.
“Zanzibar si nyumba ya mtu, ni nchi kama nchi nyingine na ni mshirika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo ni busara zaidi jambo hili kuzungumzwa kiuongozi kuliko kuamua tu,” alifafanua mwakilishi huyo.
Kauli ya Tanesco baada ya hali kuchafuka
Akizungumza jana kwa njia ya simu, Msemaji wa Tanesco, Leila Muhaji, alisema hawezi kusema chochote kuhusu kauli ya Dk. Shein.
“Yaani no (hapana), siwezi ku-comment (kusema) kwenye hilo kwa sababu aliyezungumza ni Rais, sidhani kama ni vizuri ni-comment kuhusu statement (kauli) ya Rais wa Zanzibar si sawa. Kwa hiyo sina comment katika hilo,” alisema Muhaji.
Hata mwandishi alipotaka kujua iwapo siku 14 zilizotolewa zikipita kama Tanesco itaikatia umeme Zanzibar, Muhaji alisisitiza kuwa hana cha kuzungumza.
Juzi Kaimu Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, alitoa siku 14 kwa wizara, taasisi za Serikali na makampuni binafsi yanayodaiwa na shirika hilo kulipa madeni yao kabla ya kukatiwa huduma hiyo.
Dk. Mwinuka alisema mashirika mengine ya Serikali, wizara na taasisi yanadaiwa Sh bilioni 52, huku kampuni binafsi na wateja wadogo wakidaiwa Sh bilioni 94.
Chadema nao watia neno
Jana Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, alisema kitendo cha Tanesco kuwapa wiki mbili Zeco kulipa deni hilo kabla ya kuwakatia umeme, si kizuri kwa mustakabali wa nchi hizi mbili.
Alisema pia madeni hayo hayalipiki hivyo kauli ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ally Mohammed Shein, kusema kisiwa hicho kitatumia vibatari ipo sahihi.
“Kimsingi madeni haya hayalipiki, unapomdai mtu kitu kisicholipika unafikiri atasema nini, mimi namwona kajibu sahihi kabisa,” alisema Dk. Mashinji.
JPM alivyoipa Tanesco meno
Machi 5, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli, aliipa Tanesco meno baada ya kuiagiza kukata umeme kwa wadaiwa sugu wote wakiwamo Zanzibar akisema hata kama Ikulu ya Magogoni inadaiwa pia ikatiwe.
“Hata Ikulu kama inadaiwa we kata, najua pia kuna deni la Sh bilioni 162 kule Zanzibar, nako kama hawatalipa kateni umeme. Tunataka Tanesco iharakishe kusambaza umeme kwa wananchi, sasa wasipolipwa madeni watawezaje kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi?” alihoji Rais Magufuli.