Na JANETH MUSHI-ARUSHA
WANAWAKE wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha, wametakiwa kuacha tabia ya kushiriki matendo ya kikatili yanayohatarisha maisha ya watoto wa kike, ikiwamo ukeketaji na utoaji wa mimba.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Olmotonyi, Paulina Masoka, katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Alisema kuwa, wanawake wengi wamekuwa wakishiriki katika unyanyasaji wa kijinsia na hivyo kuhatarisha maisha ya watoto wa kike.
"Wanawake wanapaswa kupiga vita vitendo vya ukeketaji na utoaji mimba, kwani katika jamii wanawake wamekuwa wakihusika kwa namna moja au nyingine na vitendo hivyo vya kikatili,” alisema Masoka.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, ambaye pia ni Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ngaramtoni, Sophia Shoko, aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kukemea na kupiga vita mimba za utotoni.
Pia, alisema kwamba, ili kuweza kujikwamua kiuchumi, wanawake wanapaswa kutokomeza mila na desturi zinazowanyima mgawanyo wa rasilimali wanazotakiwa kupata.
Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Getrude Darema, aliwataka wanawake katika halmashauri hiyo kuhakikisha wanajiunga kwenye vikundi ili kuweza kupata mikopo itakayowakwamua kimaisha.