25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

UKATA WAIKABILI EAC

Na ABRAHAM GWANDU – ARUSHA

KIKAO cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kinatarajiwa kufanyika Aprili 6, jijini hapa huku kukiwa na taarifa za ukata unaodaiwa kusababisha ishindwe kutekeleza baadhi ya majukumu yake.

Taarifa kutoka chanzo cha kuaminika, zinadai kuwa hali hiyo imesababishwa na kusuasua kwa baadhi ya nchi wanachama katika kutekeleza wajibu wao wa kuwasilisha michango kwa wakati, huku wafadhili walioahidi kutoa fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 nao wakitajwa kutowasilisha michango yao.

“Tofauti na miaka iliyopita, hali ya jumuiya kifedha si nzuri hata kidogo. Wafanyakazi walizoea kusafiri nje ya Arusha karibu kila mwezi kulingana na kitengo na kazi anayokwenda kufanya, bila kujali ni ndani au nje ya mipaka ya nchi wanachama.

 “Wapo waliokuwa wakienda Ulaya na Amerika kujifunza masuala mtambuka kwa manufaa na tija ili nasi tuboreshe jumuiya yetu, lakini sasa hakuna, hakuna mikutano iwe nje au katika jengo la Makao Makuu hapa Arusha, posho zimefyekwa na hata mishahara hadi tunaulizia jambo ambalo hatukulizoea,” kilisema chanzo hicho.

Kilisema kuwa kutokana na ukosefu wa fedha, baadhi ya wafanyakazi waliozoea posho za safari wameanza kuzungumzia hata kuacha kazi kwa madai maisha yao yanazidi kuwa magumu.

Akizungumza mjini hapa hivi karibuni kuhusu taarifa hizo zilizohojiwa katika mkutano wake na waandishi wa habari  baada ya kuzindua shindano la ubunifu lililoandaliwa na Taasisi ya Global Impact Challenge, Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberatus Mfumukeko, alimwagiza Meneja Uhusiano wa EAC, Richard Owora, kutoa ufafanuzi.

“Pamoja na hayo mnayosema, lakini hapa  hakujakauka kabisa, kazi zetu zinaendelea ila ufafanuzi zaidi mtapata kutoka kwa Owora baada ya kujadiliana na watu wetu wa fedha,” alisema Mfumukeko huku akiondoka katika eneo la mkutano.

Hata hivyo, Owera alieleza kwa ufupi mchanganuo jinsi nchi wanachama zilivyotoa michango yao katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 ambapo Uganda peke yake imevuka nusu ya mchango wake wa Dola milioni 8.3 za Marekani.

“Uganda imefikia asilimia 89.39 katika kutoa mchango wake wa kuiwezesha EAC ijiendeshe, Kenya imetoa asilimia 52.47, Rwanda imetoa asilimia 47.74 na Tanzania imetoa asilimia 30.47.

 “Kuhusu Burundi kwa sasa sina hesabu yake kamili kwa sababu juzi tu ndiyo waliwasilisha kiasi cha fedha kama mchango wao, lakini si fedha nyingi.

“Sudan Kusini wao bado, suala la wafadhili kama wametoa au hawajatoa tuliache kwa sababu EAC ni mtoto wa nchi wanachama, ni jukumu lao kumtunza na si kutegemea wafadhili,” alisema Owora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles