28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

SABABU VIFO VYA GHAFLA ZATAJWA

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

KUZIBA kwa mishipa ya damu kumetajwa kuwa chanzo kikuu kinachosababisha vifo vingi vya ghafla ambavyo mara nyingi hutokea mtu akiwa usingizini.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili juzi, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Pedro Pallangyo, alisema tatizo hilo linazidi kuongezeka hasa katika nchi zinazoendelea.

“Mshipa wa damu ukiziba husababisha mtu kupata mshtuko wa moyo na inapotokea hali hiyo mtu akiwa usingizini, hufariki dunia,” alisema.

Alisema zipo sababu hatarishi nyingi zinazochangia kuziba kwa mishipa ya damu, ikiwamo ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, unywaji pombe kupita kiasi, uvutaji sigara, uzito mkubwa na kutokufanya mazoezi.

“Hizi ni sababu ambazo mtu anao uwezo wa kuziepuka, lakini zipo sababu nyingi kwa mfano ugonjwa wa kisukari au shinikizo la damu wakati mwingine huwa yanarithiwa,” alisema.

Dk. Pallangyo alisema kiwango cha mafuta kikiwa kikubwa katika damu kuliko inavyotakiwa, huenda kuziba mishipa ya damu na kwamba athari huanza kuonekana mtu anapofikisha umri wa miaka 40 hadi 45.

“Lakini kadiri miaka inavyokwenda mbele, tatizo linazidi kujitokeza zaidi katika kundi la vijana, hapa JKCI kwa siku tunachunguza kati ya watu watatu hadi watano kujua kama wana tatizo hili.

 “Kwa wiki tunaona wagonjwa wapatao 35 ambao ukikadiria kwa mwezi ni kati ya wagonjwa 140. Mwaka 2015/16 tuliwachunguza takribani watu 400 katika mtambo wetu maalumu wa ‘cath lab’,” alisema.

Daktari huyo alisema asilimia 45 kati ya watu hao waliochunguzwa afya zao, walikutwa mishipa yao imeziba na hivyo kuhitaji kufanyiwa upasuaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles