BAADA ya kuhangaika nayo tumboni kwa miezi tisa, hatimaye siku ya siku imefika kwa mtoto mtarajiwa kukaribia kuzaliwa.
Baada ya kero, adha, usumbufu na kila aina ya mahangaiko yanayotokana na ubebaji huo wa mimba, hiki ni kipindi kingine japo kifupi lakini kichungu zaidi ya hicho cha uleaji mimba.
Ni kipindi hiki kinachoonekana kuogopwa zaidi na wengi, kiasi kuwa wale, ambao hawajawahi kushika mimba unaweza kuwasikia wakijiuliza namna watakavyoweza kukihimili kutokana na simulizi za kweli au uongo walizowahi kuzisikia.
Si wanawake hao tu, ambao hawajawahi kuonja mimba bali pia wanaume wanaosikiliza simulizi hizo au waliowahi kushuhudia kwa macho yao wake zao wakijifungua hupigia saluti ujasiri wa kina mama waliopitia hali hiyo.
Ni kwa sababu hiyo kina baba watatu walijitokeza kujaribu kuonja kile, ambacho wake zao na wanawake wengine duniani hukutana nacho wakati wa kubeba mimba na huo wakati wa kujifungua.
Hatimaye, zoezi likafanyika, kina baba hao walishuhudiwa wakilalamika kuhusu matiti yao kuvimba, hitaji la mara kwa mara la kwenda haja ndogo na usingizi wao kukatishwa nyakati za usiku.
Lakini pia wanaume hao, ambao walikubali kuonja uchungu wa kubeba mimba, walienda mbali zaidi kupitia jaribio linalofanana na hali wanayokutana nayo wanawake wanapojifungua.
Wakurugenzi wa uchapishaji Jason Bramley, Steve Hanson na Jonny Biggins walibeba matumbo bandia yenye uzito wa ‘stone’ 2.5 sawa na kilo 15.8 kila moja kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Wakati wakikubali kuvaa suti zenye mimba hizo bandia kuelekea Siku ya Mama nchini Uingereza, ambayo mwaka huu iliangukia Jumapili ya Machi 15, walidhani zitawakilisha maumivu na machungu wanayokumbana nayo wanawake wakati wa kubeba mimba.
Lakini mashabiki wao kupitia blogu yao ‘3pregnantdads.com’ waliwaambia bado hawajafikia kilele cha uchungu ule wanaopata wanawake wajawazito.
Waliwashauri watumie mashine ya kielektroiniki, ambayo inaingiza vichocheo vinavyotengeneza mazingira sawa na anayopata mwanamke wakati wa kujifungua.
Baada ya zoezi hilo la pili, sasa wamekiri iwapo kubeba tumbo zito kutakufanya uone kile wanachokumbana nacho wanawake wajawazito kumbe ni ‘cha mtoto’, basi mashine hii itakuaminisha uchungu wa kujifungua .
Jonny, 45, kutoka Surrey, baba wa watoto wawili; Enzo, mwenye umri wa miaka mitano na Leo mwenye mtoto mmoja na mkewe Mafer, alichukuliwa picha wakati wa ‘kujifungua’ na aliweza kuonekana akigugumia na kuugulia maumivu kwa uchungu.
Aliandika katika blogu yake: “Hivyo ili kufikia kilele cha uchungu, tuliweka mashine ya umeme inayotengeneza mazingira au hali bandia kuwa katika ile ya uhalisia wa kujifungua.
Hii inahusisha kulowesha mwili majini ili kuhakikisha mkondo wa umeme unapenya katika tishu za misuli na kuvaa jaketi maalumu linaloshikiza hadi mikono, miguu na makalio na kisha kuunganisha kwenye mfumo wa umeme.
“Baada ya mchakato wa awali kuwa nafuu, mkondo wa umeme unaongezeka hadi unapokuwa huna uwezo wa kudhibiti mwili wako. Unaweza kupambana nao au kusalimu amri mwenyewe kwa nguvu za voltage,”anasema.
Mwishowe baada ya zoezi, unajikuta ukihisi kwa namna ya ajabu kufarijika kwamba kumbe bado unaishi, maana wakati wa zoezi hisia zinakujia kuwa roho inaachana na mwili, anasema.
Linachopitiwa ni uchungu mtupu wa kugugumia, kuugulia na kulia maumivu hadi mwisho.
Katika tukio hilo Jason (44) alijikuta akijikojolea.
Jason, ambaye ana mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na mkewe Mondrey, alizungumzia kipindi alichopitia: “nilijisikia kana kwamba nimegeuka kichwa chini miguu juu. Hapa nilipo nimechoka na kihisia na nimepoteza nguvu zangu zote najisikia mdhaifu.”
Wakati huo huo, Steve, 46, kutoka Doncaster, ambaye ni mume wa Kate na mtoto mwenye umri wa miaka 12, Saul, alisema kujifungua kumempotezea furaha aliyokuwa akiihisi kuhusu mtoto kuzaliwa.
Alisema: kwa kweli sikuwa mzuri kuweza kuhimili maumivu. Na ndiyo najua kuwa niliyopata hayafaikii walau nusu ya hali halisi wanazokumbana nazo wanawake. Lakini bado hapa sijisikii furaha.”
Lakini ijapokuwa hawakupewa ‘mtoto wa kujifungua’ kwa kuhimili zoezi hilo, kina baba hao kutoka Uingereza, lakini ambao wanafanya kazi mjini Barcelona, Hispania walipewa zawadi nyingine – kuachana na mimba zao bandia.
Na wanafurahi kuyavua matumbo hayo bandia, na wanasema maisha yamerudi kama kawaida baada ya kuwa nayo kwa mwezi mmoja na kupata kero, adha na kila aina ya usumbufu huku Jason akisema hana hamu nayo tena.
Matumbo bandia waliyovaa yalilenga kutoa mbinyo katika kibofu, tumbo na mapafu na kusababisha matatizo ya tumbo na hali ya kutojisikia vyema kimwili na kiafya.
Waliyavaa kipindi chote hicho walalapo, waendapo kazini, baa isipokuwa tu pale wanapooga.
Wanaume hao, ambao wako nyuma ya kitabu kipya cha Siku ya Mama kiitwacho Book Of Mum, waliamua kuvaa suti hizo kusherehekea wanawake wa maisha yao na mama zao wakati wakiufanyia kazi mradi wao huo wa kitabu.
Baada ya kupitia uchungu huo, wote watatu wamekubaliana kuwaheshimu wake na mama zao kwa namna walivyo jasiri kukabiliana na hali walizozionja.