Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WAKAZI zaidi ya 200 wa eneo la Ilazo Extension, Kata ya Nzuguni B, Manispaa ya Dodoma, wamemuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, kufika katika kata hiyo ili kusikiliza kilio chao cha kudhulumiwa mashamba yao.
Wakazi hao wamedai kuwa mashamba hayo waliyatumia kwa kilimo kwa zaidi ya miaka 100, lakini wamepokwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).
Wakizungumza na waandishi wa habari juzi katika eneo hilo, walisema kinachowauma wamekuwa wakilima kwa muda mrefu katika maeneo hayo, lakini wakashangaa CDA walipowaambiwa wasilime.
Mdala Mazengo alisema wameamua kufikia uamuzi huo wa kumwomba Lukuvi akasikilize kilio chao kutokana na kushindwa kupata msaada katika ngazi mbalimbali za Serikali.
“Tumelima kwa miaka mingi, lakini tunashangaa tunatolewa, tumeitafuta haki yetu bila mafanikio yoyote, tunamwomba anayehusika atusaidie,’’ alisema Mazengo.