NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
KITENDO cha mama kumnyonyesha mtoto mdogo huku akiwa amekunywa pombe, kinatajwa kuwa ni hatari kwa afya.
Kitendo hicho kinatajwa kuwa ni hatari kwa sababu mtoto hunyonya kilevi hicho kupitia maziwa ya mama yake na baadaye huathiri afya ya ubongo wake.
Hayo yalisemwa na bingwa wa magonjwa ya akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Plaxeda Swai wakati wa mahojiano na MTANZANIA Jumapili mapema wiki hii.
“Unywaji pombe ni hatari kwa mjamzito na mama anayenyonyesha, mjamzito haruhusiwi kutumia kilevi cha aina yoyote, pombe huathiri afya ya mtoto aliyepo tumboni na anaweza akazaliwa akiwa na hitilafu kuanzia mfumo wa fahamu, kuzaliwa na uzito mdogo, kichwa kidogo na madhara mengine mengi.
“Wapo wanaofikiri kwamba madhara hujitokeza wakati wa ujauzito pekee na wanapojifungua hawajali wakati wa kunyonyesha wanalewa, mama anayenyonyesha akiwa amelewa, mtoto wake naye hulewa kwa sababu hupata pombe kupitia maziwa ya mama yake.
“Hatua hiyo ni mbaya kwa afya ya mtoto, kwa sababu kilevi huenda kuathiri afya ya ubongo wa mtoto na matokeo yake anaweza hata kupata mtindio wa ubongo,” alisema Dk. Swai.
Alisema unywaji wa pombe kupita kiasi hasa zile zilizo kali, ni hatari kwa afya ya mtumiaji kwa sababu anakuwa katika uwezekano mkubwa wa kupata tatizo la kifafa baadaye katika maisha yake.
“Asilimia nne ya watu wanaokunywa pombe kali huishia kupata kifafa, asilimia 50 hadi 75 ya watu wanaokunywa vilevi kupita kiasi huishia kupata matatizo ya kiakili na asilimia 20 hadi 25 ya watu wenye matatizo ya akili huwa wametumia aina moja au nyingine ya kilevi,” alisema Dk. Swai.
Pia alishauri watu waliofikia hatua ya utegemezi wa vilevi na wanahitaji kuondokana na hali hiyo ni vema wakawahi mapema kufika hospitalini kwa matibabu.
“Tafiti zinaonyesha asilimia 80 ya watu ambao wamefikia kiwango cha utegemezi wa pombe hupata tatizo la sonona na hofu iliyopitiliza,” alisema.