25.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 5, 2024

Contact us: [email protected]

VITA DAWA ZA KULEVYA: BAADA YA MAJARIBIO UKOMAVU UNAHITAJIKA

 

VITA dhidi ya dawa za kulevya ni kubwa na ni kali kwani wale wanaofanya biashara hiyo wananufaika sana na wanapenda kuendelea kufaidika.

Yeyote anayejaribu kuwafuatilia huwa shakani kabisa. Tumeona jinsi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alivyoamua kulivaa suala hili kwa nguvu sana.

Wapo walioona juhudi hizi kuwa ni kujaribu kukwepa masuala yaliyokuwa mbele yetu kama matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ambayo yalionyesha Dar es Salaam kutofanya vizuri kama ilivyotarajiwa na masuala mengine yaliyokuwa katika mjadala wakati huo kama uhaba wa chakula au njaa n.k .

Hata hivyo Makonda alitaja orodha ya kwanza na baadaye akataja ya pili ya watu wanaoshukiwa kuhusika na biashara hiyo kwa njia moja au nyingine.

Pamoja na hisia mbalimbali amepongezwa na baadhi ya watu kwa uthubutu huu ambao mwenyewe aliuelezea kama wajibu wake kwa Mungu, kwani akifika huko aweze kuwa na cha kumjibu Mungu.

Kitu nilichojifunza kwa Makonda ni kile alichokisema mwenyewe kuwa yeye bado yuko katika umri wa kujaribu, kwa hiyo aachiwe kujaribu.

Ni kweli kabisa upo wakati au umri  wa kujaribu na huwa mtu akiwa katika umri huo huruhusiwa au huachiwa ajaribu kwani akijaribu hujifunza na baadaye huwa na ujuzi na uzoefu zaidi.  

Mfano kuna mjukuu wangu ambaye   alipokuwa na umri wa miaka saba alinihoji nilivyoingia ndani ya runinga aliponiona nikiongea  kwenye runinga wakati tupo wote hapo. Nilimueleza kwa kadiri nilivyoweza inavyokuwa.

Kutokana na umri wake hakunielewa ila alisubiri siku ya nafasi akachukua mti akapiga ile runinga kwa kutaka kujua watu wanaingiaje mle. Hapa alijaribu na alikuwa kweli katika umri wa kujaribu.

Badala ya kukuta watu runinga ile ilikuwa imeharibika. Hapo aliweza kupata jibu. Hata hivyo sina uhakika umri huu wa majaribio huenda mpaka lini ila tafiti zinaonyesha hakuna umri sahihi kwani wapo wenye umri mdogo wanaoweza kuwa wamepita muda huo wakati wapo walio na umri mkubwa lakini bado wanajaribu. Kila mara bila kujali umri majaribu huweza kuleta matokeo chanya au hasi.

Katika vita hii ya dawa za kulevya tumeona jinsi hali ilivyokuwa baada ya majina kutajwa, kuna waliosifia, wapo waliolaumu na wapo waliotahadharisha kuwa njia hiyo huenda ikasababisha wale wanaotajwa na hata ambao hawajatajwa kujificha au kuficha ushahidi.

Pia wapo walioumizwa kwa kuona wametajwa wakati hawahusiki na wapo waliodhamiria kwenda mahakamani kwa vile wameona wamevunjiwa heshima yao.

Watetezi wa haki za binadamu nao walionya kuwa kwa kutaja majina kwa njia hiyo huenda haki za watu na utu wao ukaingiliwa kinyume na vipimo vya haki za binadamu vinavyohitaji.

Kitu kikubwa ambacho tunaweza kusema katika jaribio hili kuwa ni chanya ni pale palipokuwa na itikio katika mikoa mingine, bungeni, viongozi wa dini  na hatimaye Rais akateua Kamishna wa Tume ya Kudhibiti  Dawa za Kulevya.

Iwapo Makonda asingeanza kwa sababu yoyote ile sijui ni lini tungesikia katika  mikoa mingine wakikamata walima bangi, wakikamata mihadarati na watumiaji na wauzaji?

Ni wazi kuwa kabla ya tajataja hiyo suala la sheria iliyopo tangu mwaka 2013 ya Kudhibiti Dawa za Kulevya halikutajwa, hata uwepo wa Tume na kuwa Kamishna alikuwa hajateuliwa  halikufahamika au halikushughulikiwa.

Sasa tumemsikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akikiri kuwa sheria hiyo ni kama ilikuwa imefichwa na hata wajumbe wa tume hiyo iliyoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu walikuwa hawafahamu iwapo ni wajumbe na wana wajibu gani.  Majaribio ya Mkuu wa Mkoa wa Dar  yameibua mengi.

Awamu ya tatu ya kutaja majina ilibadilika na majina hayakutajwa bali idadi yao na orodha ya majina ilikabidhiwa kwa Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ambaye alikuwa ameteuliwa na Rais siku si nyingi.

Idadi ilikuwa ni 97. Jambo lililotokea katika siku hiyo ni watoto wadogo kuonyeshwa hadharani na kutoa ushuhuda wa uhusika wao katika dawa za kulevya na pia hali ya afya zao pia ilielezwa.

Hili nalo limekaa kama ni ile hali ya kujaribu  pamoja na kuwa ni kinyume na haki za watoto wale na pia sheria ya mtoto ya Mwaka 2009. Bahati mbaya pia ni kosa kwa mujibu wa sheria hiyo ya mtoto.

Hapo alipofikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pametosha, na ni vyema kuwa sasa chombo husika kimechukua nafasi yake. Kamishna alipokabidhiwa yale majina alisema bayana kuwa hatayataja bali atafanya kwanza upelelezi pakiwa na ushahidi wa kutosha atawapeleka wahusika mahakamani.

Pia alitanabahisha kuwa upo umuhimu wa kuwa na uangalifu kwani huenda majina yakatajwa kwa nia ovu. Kwa kuongeza ukomavu katika zoezi hili zito na gumu Waziri Mkuu katika uzinduzi wa Tume hiyo ya Kudhibiti  Dawa ya Kulevya alitoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wote wanaoshughulikia suala hilo kuhakikisha hawataji majina ya watu bila kuwa na uhakika wa ushiriki wao.

Hii ni vita na vita yoyote pamoja na kuwa husemekana vita haina macho kila vita lazima ipambanwe kwa ustadi wa hali ya juu. Niliwasikia watu mbalimbali wakionya kuwa suala hili lisipoangaliwa vyema badala ya kufanikiwa itakuwa balaa.

Mbinu za ukamataji, mbinu za upepelezi na mbinu za kushughulika na wanaoshukiwa lazima ziwe za ufundi na ukomavu wa hali ya juu kama kweli tunahitaji ushindi katika vita hii.

Bila kumlaumu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na majibu ya kimajaribio anayoyatoa ushauri unavyotolewa, ni kuwa  amelianzisha likadakwa vyema, tunasihi waliopokea silaha hiyo wafanye kazi hii kwa kumaanisha na kwa ukomavu ambao tumeanza kuuona.

Tunajua Kamishna mstaafu wa Tume ya Kudhibiti  Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alifanya mengi na hayakuwa yakiwekwa hadharani bali matokeo ya ukamataji yalionekana kwa kiasi chake.

Waliopokea kijiti inabidi wajifunze kutoka kwa watangulizi. Pia waangalie ugumu wa vita hii. Kabla ya kushusha lawama kwa baadhi ya watu wajifunze pia hali ilivyo.

Ni kweli huenda kukawa na watu wanaocheza au waliocheza mchezo wa kuwasaidia wahalifu lakini hili haliwezi kuwa ni blanketi kuwa mahakama kwa mfano ionekane kuwa ilishindwa kazi yake au polisi wasemekane walishiriki kuharibu ushahidi kwa ujumla wao.

Kinachotakiwa kama alivyosema Kamishna ni kufanya uchunguzi na mazingira halisi yaliyosababisha hukumu zinazotia shaka. Hata katika shaka hiyo majaji nao wapewe nafasi ya kueleza mazingira yao ya kazi wanaposhughulikia kesi za aina hii.

Kwa kasi iliyoanzwa tunategemea haitakomea njiani panapozuka jambo jingine hapa nchini bali vita hii itakuwa endelevu na itashughulikiwa kiuweledi ili kudhibiti biashara na matumizi ya madawa haya ya kulevya ambayo yasipodhibitiwa kwa wakati na kwa ukamilifu kama taifa tutaingia hasara kubwa sana hasa kwa nguvu kazi itakayotokomea katika janga hili.

Mungu Ibariki Tanzania  na watu wake.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles