27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

NCHI 13 ZAKUBALIANA KUBORESHA ELIMU

Na PATRICIA KIMELEMETA

NCHI 13 za Afrika zikiwamo za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimekubaliana kuboresha sekta ya elimu katika nyanja mbalimbali ikiwamo kuweka mifumo bora ya utoaji wa elimu na kutatua changamoto zinazowakabili walimu ikiwamo mishahara na kupanda kwa madaraja.

Akizungumza Dar es Salaam juzi katika kongamano la nchi hizo lililokuwa linajadili elimu jumuishi, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema kwa upande wa Tanzania, Serikali itashirikiana na wizara mbalimbali hapa nchini.

Profesa Ndalichako alisema katika makubaliano hayo, wamepanga kuweka mifumo bora ya utoaji elimu, kuboresha mazingira ya utoaji elimu, kusimamia posho za walimu, mishahara na wale wanaotakiwa kupanda madaraja.

Pia alisema kwa sababu elimu bora huanza kwa mwalimu, hivyo wamekubaliana kuwajengea uwezo wa kufundisha, kuwapa semina elekezi na kubadilishana uzoefu utakaowasaidia kutoa elimu bora.

Alisema ili kuhakikisha kuwa makubaliano yanafanikiwa, wataanzisha mfumo wa kusimamia na kupima utekelezaji wa makubaliano hayo kuanzia elimu ya awali ya umri wa miaka minne hadi sita huku wakiwapima wanafunzi kwa kutumia matokeo ya mitihani ili wale waliofeli zaidi waweze kuangalia namna ya kuwasaidia.

“Katika mfumo huo pia tutaangalia utoaji wa elimu kwa watoto bila ya kujali mazingira yao huku tukiangalia namna ya kuwasaidia watoto wenye vikwazo au matatizo mbalimbali ili waweze kupewa mikakati ya kufaulu,” alisema.

Ndalichako alisema mfumo huo pia wataweza kuangalia utoaji wa elimu ya watu wazima na mtoto wa kike na kuweka mikakati mingine ya uboreshaji wa elimu.

“Tumekubaliana kusimamia kwa ukaribu zaidi mafunzo ya ufundi stadi ili vijana wanaofeli elimu ya juu waweze kujiunga na kupata maarifa zaidi ya elimu ya vitendo, jambo linaloweza kupunguza tatizo la ajira,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema wanafunzi watajengewa uwezo wa kujiendeleza pamoja na kusimamia upatikanaji wa takwimu sahihi na kuzifanyia uchambuzi.

Alisema mkakati wa nchi hizo za EAC ikiwamo Somalia, Mauritius na Djibouti ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanatapa elimu bora kwa maendeleo ya taifa na nchi hizo jambo linaloweza kuwasaidia kuingia katika soko la ushindani wa ajira ndani na nje ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles