30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

WATUMISHI TRA WATAJWA ORODHA DAWA ZA KULEVYA

Na AGATHA CHARLES

WATUMISHI wawili wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), wamekamatwa katika operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kusaidia kupitisha kemikali bashirifu za ephedrine zinazotumika kutengenezea dawa za kulevya aina ya heroine.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Mamlaka hiyo zilizoko Upanga, Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni hiyo, Mihayo Msikhela, alisema pamoja na hao, wapo watumishi wengine wawili wa TRA ambao nyendo zao zinafuatiliwa.

“Wakati wa kukabidhiwa majina ya watu wanaojihusisha na dawa hizo nilitamka kuwa wapo watumishi wa umma wanaosaidia kuingiza hasa kemikali bashirifu,” alisema.

Kuhusu watumishi hao waliokamatwa ambao hata hivyo hakuwa tayari kuwataja kwa majina, alisema taratibu zinafanyika na wakati wowote watafikishwa mahakamani.

Kamishna Msikhela alisema tayari operesheni hiyo inayofanyika mikoa mbalimbali ya Tanzania bara kwa kukamata wasambazaji, wauzaji, watumiaji na kuharibu dawa za kulevya zilizoko mashambani, imeonyesha mafanikio ndani ya siku nne za mwanzo.

 “Dawa za kulevya ziko katika makundi mawili, kundi la kwanza ni dawa za kulevya zilizoko mashambani na kundi la pili ni dawa za kulevya za viwandani. Na dawa za kulevya za mashambani kwa kiwango kikubwa ndio kero iliyopo kwa wananchi wetu. Matokeo haya ni operesheni ya siku nne tu hadi jana (Alhamisi),” alisema Kamishna Msikhela.

Alisema Mkoa wa Simiyu umeongoza kwa kuteketeza ekari 40 za bangi ukifuatiwa na Mkoa wa Kipolisi Tarime na Rorya kwa ekari 36 huku Lindi ukiongoza kwa kukamata dawa za viwandani aina ya heroine ambazo ni kete 50.

Kamishna Msikhela alitaja mikoa mingine iliyofanya vyema katika operesheni hiyo kuwa ni Tanga ambayo ilikamata mirungi kg 44, bangi puli 3, Morogoro (bangi kg 18, heroine kete 3),  Shinyanga (bangi kg 10 na gramu 136), Kagera (bangi ekari 14, mirungi ekari 1), Njombe (bangi nusu ekari na gramu 20), Songwe (heroine kete 274, mirungi kg 3), Tabora (bangi kilo 6, mbegu kg 18),  Singida (bangi misokoto 203, heroine kete 1), Rukwa (bangi kete 105), Mbeya  (bangi kg 5), Kigoma bangi nusu ekari na Ruvuma bangi gramu 300.

Kamishna huyo alisema watuhumiwa hao ni wengi na wanaendelea kuhojiwa ambapo baadaye utafanyika utaratibu wa kisheria kuwafikisha mahakamani.

“Kama tutaendelea na mlipuko huu ambao umeongezewa mafuta, nina uhakika dawa za kulevya mashambani zinaweza kupungua kwa kiwango kikubwa. Tuunganishe nguvu na kuhakikisha vita hii inapiganwa kila sehemu,” alisema Kamishna Msikhela.

Akijibu swali la waandishi kuhusu kutaja na kushughulikia majina 97 wakiwemo wanaodaiwa kuwa ni vigogo na watoto wa vigogo, Kamishna Msikhela alisema kila aliyetajwa ataguswa.

“Yeyote aliyetajwa kwenye orodha hiyo ambayo ni orodha yenye fumbo ataguswa, hatutazami kwamba kigogo ni yupi na yupi si kigogo, yaliyomo mle ni majina ya wahalifu kama wahalifu wengine,” alisema Kamishna Msikhela.

Alisema orodha hiyo ambayo haina muda mrefu tangu ikabidhiwe kwao, ufuatiliaji umeanza na hivyo atatoa taarifa.

Akijibu swali lingine kuhusu orodha za awali zilizowataja kwa majina watuhumiwa huku ile ya majina 97 wakifichwa, Kamishna Msikhela alisema ni mfumo unaotumika.

“Ni mfumo uliotumika, yapo makosa ya mtaani hayaendelei kusumbua tena. Yapo makosa yaliyo wazi na yapo makosa yaliyojificha. Kwa hiyo yaliyo wazi tutajua yalikuwa katika hatua ipi na yaliyojificha yako kwenye hatua ipi na yanafanywa vipi,” alisema Kamishna Msikhela.

Kamishna Msikhela alisema:

“Vita ina mifumo mbalimbali ya upiganwaji, kwa hiyo mifumo yote itatumika ilimradi itakupelekea kwenye mafanikio na ukatoka umetangazwa you’re a hero (shujaa) yote huwa inatumika.”

Alisema vita ya dawa za kulevya ilianza miaka ya nyuma na kinachofanyika hivi sasa ni mwendelezo kama ilivyo upambanaji duniani kote.

“Huu ni mwendelezo kama ilivyo dunia nzima inavyopiganwa na sisi tunawajibika kupigana hii vita mpaka dunia itakapoweza kuipunguza kabisa au kuimaliza,” alisema Kamishna Msikhela.  

Kamishna Msikhela alisema pamoja na Mamlaka hiyo iliyotangazwa hivi karibuni, lakini pia kuna vyombo vya ulinzi na usalama na hasa Jeshi la Polisi ambavyo utaratibu wa kuripoti na kufanya majukumu yake uko pale pale.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles