Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimejipanga na kitampatia mawakili wa chama Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe katika hatua yake ya kumfungulia kesi ya kikatiba na ya madai Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Februari 8 mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitaja majina 65 kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya akiwamo Mbowe na kuwataka kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.
Lakini siku moja baadaye Mbowe aliitisha mkutano na waandishi wa habari akiwa mjini Dodoma ambapo alieleza kutofika polisi kwa wito wa Makonda akisema hana mamlaka hiyo isipokuwa pale tu taratibu za kisheria zitakapofuatwa.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni aliweka bayana nia yake ya kumfungulia mashtaka ya madai Makonda kwa kumkashifu na kumchafulia jina.
Akitoa maazimio ya kikao cha kamati ndogo ya Kamati Kuu ya Chadema jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Abdalah Safari alisema kamati hiyo inaunga mkono hatua ya Mbowe kumfungulia kesi ya kikatiba Makonda.
“Katika hili tumejipanga kweli kweli…tutaungana na Mbowe katika kesi hii na tutampatia mawakili wa chama akiwamo mimi na tuko wengi,”alisema.
Profesa Safari aliwataka wote ambao walitajwa na wanaamini kuwa walionewa kujihusisha na biashara au utumiaji wa dawa za kulevya wafungue mashauri mahakamani.
“Tunatoa wito kwa wale wengine wote ambao walitajwa na wanaamini kuwa walionewa, kuchafuliwa majina na au kudhalilishwa wafungue mashauri mahakamani, kwani hii ndio njia pekee ya kuzuia wengine wasifanyiwe uonevu kama huu siku zijazo,”alisema Profesa Safari.
Pamoja na mambo mengine, Profesa Safari alisema tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu 2015 viongozi na wanachama wa Chadema wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya kubambikiziwa kwa kisingizio cha uchochezi.
Alisema mpaka sasa jumla ya wanachama na viongozi 215 wamefunguliwa kesi zaidi ya 78 nchi nzima.
“Kati ya hao wengi wao wamenyimwa dhamana bila sababu za msingi huku wale ambao walipatikana na hatia walipewa adhabu za vifungo bila kupewa fursa ya faini.
“Kutokana na hilo, hivi sasa tunaandaa orodha kamili itakayoainisha kesi zote za jinai ambazo ziko mahakamani na kuonyesha aina ya mashtaka na vifungo vilivyotolewa ambayo itawekwa wazi kwa vyombo vya habari na taasisi za ndani na nje ya nchi kuthibitisha kuwa kuna mpango wa kuwafunga viongozi wa upinzani kwa kusudi ili kuwadhoofisha,”alisema Profesa Safari.
Katika hatua nyingine Profesa Safari aliwaomba marais wastaafu, mawaziri wakuu wastaafu na majaji wastaafu kuzungumza na Rais John Magufuli kutokana na yanayoendelea na kwamba wasiogope kwani wao hawatatumbuliwa.
“Marais wastaafu Ali Hassani Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wanaogopa nini? Kwanini wasimwambie Rais Magufuli kuwa na wao waliapa kuilinda Katiba ya nchi hivyo na yeye afanye hivyo.
“Mawaziri wakuu wako wapi? Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba, Dk. Salim Ahmed Salim huyu amekuwa kimya kabisa na alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Majaji wastaafu nao wako kimya. Tunaomba waache uoga wajitokeze wao hawatatumbuliwa,”alisema Profesa Safari.