25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU KENYA: SIASA ZA USHINDANI AMBAZO MOI HAKUZIONJA ZINAVYOLETA HOFU KENYA

Na JOSEPH HIZA,

KATIKA miaka yake yote 50 ya kuwa katika siasa, Rais mstaafu wa Kenya, Daniel arap Moi kamwe hakuwahi kuonja joto kali la siasa za ushindani kama, ambalo linashuhudiwa tangu astaafu siasa mwanzoni mwa miaka ya 2002. 

Daima Mzee Moi, aliyejipachika jina la utani la profesa wa siasa, kutokana na kudumu muda mrefu madarakani na werevu wake kisiasa licha ya kutokuwa na elimu kubwa, alikuwa akijitwalia wadhifa huo wa juu bila kizingiti chochote kila uchaguzi ulipofika. 

Katika matukio machache wakati kulipokuwa na upinzani daima alikuwa na faida kubwa ya vyombo vya dola.

Hata baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1991, Moi alikuwa bado rais mwenye nguvu na ushawishi.

Vigogo wengi wakiwamo waliopaswa kuwa wapinzani wake aliwawekea mtego uliowanasa na kujiunga naye akiwamo Raila Odinga.

Licha ya kwamba upinzani ulikuwa ukiimarika, mchuano wa urais haukuwa ukichukuliwa kwa uzito mkubwa miongoni mwa Wakenya.

Joto pekee alilokuwa akikumbana nalo Moi ni harakati za uasi ikiwamo jaribio la 1982 la mapinduzi, ambalo lilishuhudia wengi wakikamatwa, kuteswa na hata kuuawa mikononi mwa vikosi vyake vya siri.

Kipindi chake hicho, sehemu kubwa ya Wakenya hawakuwa wakifahamu maana ya siasa za ushindani.  

Siasa za ushindani ni zile zilizomuacha mgombea urais wa Chama cha Democratic nchini Marekani, Hilary Clinton amwage machozi kiasi cha kushindwa kuzungumza baada ya ushindi wa kushtusha wa mpinzani wake kutoka Republican, Donald Trump. 

Siasa za ushindani zimekuwa zikishuhudiwa visiwani Zanzibar, ambako pande mbili hasimu kisiasa huweza kuchinjana, kususiana shughuli za kijamii na kiuchumi. 

Siasa za ushindani za Kenya ni mbaya zaidi.

Watu hupiga wapinzani wao hata kusababisha vifo, hushambulia wake zao na kuwapiga makofi maofisa wa uchaguzi na kadhalika.

Hapo inahusisha pamoja na chaguzi za wabunge na zile nyingine. 

Mwaka 2007  Kenya ilitumbukia katika machafuko makubwa, ambayo itachukua muda mrefu kuyasahau. Lakini yote hayo yalichagizwa na siasa za ushindani. 

Ushindani huo haukuwepo wakati wa uchaguzi wa 2002, ambapo Mwai Kibaki kutoka muungano wa Rainbow alimshinda Uhuru Kenyatta kutoka kile kilichokuwa chama tawala cha KANU. 

Ni kwa vile ulikuwa uchaguzi wa baina ya mwanasiasa mchanga na mzoefu na zaidi; wote walitokea kabila moja. 

Mwaka 2007 ulikuwa na ushindani mkali mno kwa vile ulihusisha wagombea wawili wanaoongoza kutoka makabila tofauti; Mwai Kibaki na Raila Odinga.   

Ni jamii ya Kikuyu dhidi ya Luo, ambazo uhasimu unaanzia tangu wakati wa utawala ulioasisi Uhuru chini ya Mzee Jommo Kenyatta, baba wa Uhuru na Jaramogi Odinga, baba wa Raila. 

Kwa mwaka huu wakati tayari mgombea urais wa upande wa muungano tawala wa Jubilee akiwa anajulikana; Rais uhuru Kenyatta anayetoka jamii ya Kikuyu yule wa muungano mkubwa wa upinzani wa NASA anaweza kutokea kabila la Luo iwapo Raila atapitishwa. 

Hata kama Raila hatapitishwa na kuamua kuwaunga mkono vinara wenzake wa NASA; kina Kalonzo Musyoka kutoka Kamba au Musalia Mudavadi Kutoka Luhya mpambano baina ya jamii hizo mbili utakuwa palepale tena wenye ushindani mkali. 

Katika ushindani huo mkali, kutabakia maswali haya; Je, uchaguzi huo utakaofanyika Agosti mwaka huu utakuwa huru na wa haki? 

Uwe ni huru au wa haki je, wagombea urais watakuwa tayari kukubali matokeo? Iwapo hawatakubali watafuata taratibu za kisheria kuupinga au kuruhusu wafuasi kuzusha vurugu na machafuko?

Wasiwasi kutoana na mwenendo huo, ndiyo unaowaweka Wakenya na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla roho juu kwa hofu ya machafuko kama ilivyotokea mwaka 2007.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles